Tafuta

Tanzania ni mwenyeji wa mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA unaonogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Tanzania ni mwenyeji wa mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA unaonogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.”  

Maaskofu Katoliki Tanzania: Mkutano Mkuu 20 wa AMECEA

Tanzania ni mwenyeji wa mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA. Kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Inachota maudhui yake kutoka katika “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote." Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa kiikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi; Njia za kupanga na kutekeleza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, kuanzia tarehe 8-18 Julai 2022 kwa muda wa siku 10 Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati linaloundwa na Nchi 8 ambazo ni: Zambia, Malawi, Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia na Eritrea, AMECEA, litafanya mkutano wake mkuu wa 20. Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji. Huu ni mkutano ambo hufanyika kila baada ya miaka minne. Itakumbukwa kwamba, mkutano wa 19 wa AMECEA uliadhimishwa Addis Ababa nchini Ethiopia. Tanzania ni mwenyeji wa mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA unaonogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui yake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, unaozungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa kiikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ikolojia na maisha ya kiroho.

Mambo makuu matatu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga anabainisha kwamba, maadhimisho haya ni fursa makini kwa Maaskofu katika umoja, ushiriki na utume wao watatembea pamoja katika sala, tafakari na hatimaye, kuibua sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa Ukanda wa AMECEA. AMECEA ilizaliwa kwa lengo la kuwa na mbinu mkakati wa pamoja katika shughuli za kichungaji kwa maslahi mapana zaidi ya watu wa Mungu Ukanda wa AMECEA. Miongozo ya Mababa waanzilishi wa AMECEA ilikuwa kuimarisha Imani Katoliki na maendeleo endelevu na fungamani ya jamii kwa kuwa na Mpango Mkakati wa muda mrefu AMECEA ilizaliwa kwa lengo la kuwa na mbinu za kichungaji kwa maslahi ya watu wa kanda ya AMECEA.

Utunzaji bora wa mazingira ni wajibu wa kimaadili, kidini na Kikristo.
Utunzaji bora wa mazingira ni wajibu wa kimaadili, kidini na Kikristo.

Miongozo ya Mababa waanzilishi wa AMECEA ilikuwa kuimarisha Imani Katoliki na maendeleo endelevu na fungamani ya jamii kwa kuwa na Mpango mkakati wa muda mrefu uliowekwa katika Mkutano Mkuu wa AMECEA uliofanyika Julai 1961, kwenye Ukumbi wa Msimbazi Center, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Dhamira kuu ilikuwa: “Kesho ya Kanisa la Bara la Afrika.” Tangu wakati huo, AMECEA kimekuwa ni chombo madhubuti za shughuli za kichungaji katika mchakato wa ujenzi wa umoja, udugu wa kibinadamu, ushirikiano na mshikamano sanjari na maboresho ya huduma za kichungaji kwa watu wa Mungu Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Kumekuwepo na mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwa AMECEA. Kati ya matunda haya ni pamoja na uundwaji wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo. Kusimama kidete katika mchakato wa kutetea haki, amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kulea dhamiri nyofu ili watu watende kadiri ya mapenzi ya Mungu pamoja na utekelezaji wa dhamana na wajibu wa waamini katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga anawaalika watu wa Mungu nchini Tanzania kushikamana na kushirikiana kwa moyo mmoja, nguvu na sauti moja katika maandalizi na hatimaye maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA. Yote yaanze na hatimaye, kuhitimishwa vyema. Shukrani za pekee kwa Jimbo kuu la Dar es Salaam kujisadaka katika kuchangia maandalizi ya mkutano huu, mfano bora wa kuigwa na majimbo pamoja na watu binafsi. Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo kiwe ni kiini cha kuratibu shughuli nzima za kuchangia Mkutano mkuu wa AMECEA. Mchango huu unaweza kutolewa kwa njia ya huduma za kibenki na huduma za kimtandao. Lengo ni kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kuwaelimisha watu, huku wakiongozwa na dhamiri kuu ya AMECEA kwa Mwaka 2022. Utunzaji bora wa mazingira unapania ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kama anavyo bainisha Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo ni shule ya imani, sakramenti, maadili na sala.
Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo ni shule ya imani, sakramenti, maadili na sala.

Kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya maji hali ambayo imepelekea hata ubora na usalama wa maji ambayo ni uhai kupungua sana na hivyo kuhatarisha usalama na maisha ya viumbe hai. Kumbe, Mama Kanisa anataka kujikita katika malezi ya dhamiri, ili kutoa mwelekeo chanya, endelevu na fungamani katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ikumbukwe kwamba, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni wajibu wa kiimani na Kikristo kuhusu ushiriki wa utunzaji bora wa mazingira, kielelezo cha kazi ya uumbaji. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni sehemu muhimu sana ya Kanisa Mahalia; mahali ambapo Wakristo wanasali, wanasikiliza na kutafakari Neno la Mungu; wanashiriki adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu wanalolimwilisha katika: imani, matumaini na mapendo ya mapendo “koinonia.” Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni mahali pa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Hapa ni mahali ambapo imani ya Kikristo inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji yaani “Diakonia” Lengo kuu ni kuwawezesha Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.

Kimsingi, Jumuiya ndogo za Kikristo ni chombo makini cha uinjilishaji, zinazosaidia kujenga na kuimarisha ujirani mwema, udugu na upendo wa Kikristo. Ni mhimili wa maisha na utume wa Kikristo katika kujenga imani, maadili na utu wema. Ni sehemu ya muundo wa Kanisa Mahalia Barani Afrika, katika maisha na utume wake. Ni mahali pia pa kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zinakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anakaza kusema, Jumuiya ndogondogo za Kikristo ni jukwaa la uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni kikolezo cha majadiliano ya kidini na kiekumene; mahali pa ujenzi wa umoja, mshikamano na upendo wa kijamii. Ni mahali pa majiundo na malezi ya kina kuhusu Neno la Mungu. Ni shule ya awali na endelevu ya: makuzi, malezi na majiundo ya Kikristo. Ni mahali muafaka pa katekesi makini inayosimikwa katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Ni mahali ambapo majiundo endelevu yanaweza kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa, ili kukuza na kuimarisha imani, matumaini na mapendo. Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo ni shule ya dini na chachu ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.

AMECEA Tanzania 2022

 

12 March 2022, 15:31