Tafuta

WAWATA Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, tarehe 14 Novemba 2021 limezindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wa WAWATA ngazi ya Parokia. WAWATA Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, tarehe 14 Novemba 2021 limezindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wa WAWATA ngazi ya Parokia.  

WAWATA Jubilei ya Miaka 50 Parokia Kiabakari, Musoma, Wawasha Moto wa Jubilei!

WAWATA Parokia ya Kiabakari Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, imezindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA kunako mwaka 1972 kwa semina maalum iliyoendeshwa na Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti WAWATA Taifa. Ibada ya Misa Takatifu na uzinduzi wa Ujenzi wa Jengo la Kitega Uchumi, WAWATA Parokia ya Kiabakari! Hadi raha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anatambua usawa na utofauti uliopo kati ya mwanamke na mwanaume na kwamba, kimsingi wote hawa wanakamilisha, ili kuondokana na dhana ya mfumo dume unaowakandamiza na kuwanyanyasa wanawake. Uwezo wa mwanamke kuzaa ni kanuni na utambulisho maalum kwa wanawake ambao wamejaliwa uwezo wa kuendeleza zawadi ya uhai: kwa kuilinda, kuidumisha na kuiendeleza. Kanisa linapenda kuwapongeza wanawake kwa mchango wao katika medani mbalimbali za maisha ya mwandamu; kwani wamekuwa mstari wa mbele katika masuala ya elimu, malenzi na majiundo makini. Wanawake ni washiriki wazuri katika maisha na utume wa Kanisa mahalia na kwamba, wao wanaonesha ile sura ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni watu wanaojisadaka bila kujibakiza kwa njia ya sadaka na majitoleo yao katika huduma; kwa kuonesha ukarimu, kimsingi, wanawake ni sawa na tumbo la Kanisa linalopokea na kuzaa maisha. Mwili wa mwanamke ni kielelezo cha maisha, lakini kwa bahati mbaya, unaharibiwa hata na wale ambao walipaswa kuwalinda na kuwasindikiza katika maisha! Kuna mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, biashara ya ngono na vitendo vya ukeketaji; mambo ambayo Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuyavalia njuga, ili kusitisha vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya wanawake duniani, kiasi cha kuwageuza kuwa kama bidhaa inayouzwa sokoni, bila kusahau umaskini unaosababisha wanawake wengi kuishi katika mazingira: duni, magumu na hatarishi; kiasi hata cha kunyanyaswa, kielelezo cha utamaduni usiojali wala kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wengine.

Baba Mtakatifu Francisko anapopembua kuhusu wanawake, maisha na utume wao ndani ya Kanisa anakiri kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatoa fursa zaidi kwa wanawake kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, wanawake wanashiriki kwa ukamilifu zaidi katika utekelezaji wa dira na mikakati ya shughuli za kichungaji ndani na nje ya Kanisa. Wanawake ni wadau wakuu katika kukoleza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia na kijamii; ni watu wenye utajiri mkubwa, wanaoweza kusaidia upatikanaji wa amani na utulivu; wito na utume maalum kwa wanawake. Ziwepo juhudi za makusudi ili kuwahamasisha wanawake kushiriki katika maisha ya hadhara, katika medani mbalimbali za maisha: mahali panapotolewa maamuzi na utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuliki za kichungaji kwa Makanisa mahalia. Wanawake wajengewe uwezo wa kufanya maamuzi machungu katika maisha, kwa kuwajibika barabara katika jamii na katika maisha na utume wa Kanisa.

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ambacho ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika”. Katika mahojiano maalum na Vatican News, Padre Wojciech Adam Koscielniak, Paroko wa Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, muasisi wa Parokia na Kituo cha Hija cha Kiabakari Jimbo Katoliki Musoma, chemchemi ya huruma ya Mungu anabainisha yale yaliyojiri katika uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA. Kilele chake ni mwezi Septemba 2022. WAWATA pamoja na mambo mengine, inapania kumjengea mwanamke uwezo wa kujikomboa yeye na familia yake, ili aweze kuwakomboa watu wengine wenye shida, yatima na wasiojiweza. WAWATA inataka kumwendeleza mwanamke: Kijamii, kielimu na kiujuzi ili aondokane na giza la kiroho, ujinga wa akili na aendeleze wengine sanjari kumwezesha mwanamke katika masuala ya kiuchumi ili kutegemeza familia, Kanisa na kuwategemeza wengine.

Mama Evaline Malisa Ntenga Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, Jumamosi tarehe 13 Novemba 2021 ameongoza Semina kuhusu Mpango Mkakati wa WAWATA kwa Mwaka 2018-2022: Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” kuanzia tarehe 19 Machi 2021 hadi tarehe 26 Juni, 2022, Siku ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2021 na Mwaka wa Mwaka wa Mtakatifu Yosefu. Amegusia maana ya uongozi ndani ya Kanisa, kwa kubainisha sifa kuu za kiongozi yaani: Uwezo, ujasiri, nguvu ya kimtandao katika utekelezaji wa majukumu, sera na vipaumbele. Aina za viongozi na mitazamo yao. Lakini zaidi amekazia uchaji wa Mungu, ukweli, uaminifu, uadilifu kama nguzo kuu katika uongozi. Mwishoni, ametaja baadhi ya “wanawake wa shoka” mifano bora ya kuigwa kutoka katika Maandiko Matakatifu. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA yananogeshwa na kauli mbiu "Miaka 50 ya WAWATA: Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji."

Padre Wojciech Adam Koscielniak anasema, Jumapili tarehe 14 Novemba 2021 Siku ya V ya Maskini Duniani, ilitengwa maalum kwa ajili ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA katika ngazi ya Kiparokia. Kulikuwepo na wajumbe kutoka Jimbo Katoliki la Bunda na WAWATA Jimbo Katoliki la Musoma. Ibada ya Misa takatifu imeongozwa na Padre Godfrid Maruru, Mwalimu na Mlezi kutoka Seminari ya Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma aliyetafakari Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya 33 ya Mwaka B wa Kanisa na kuwataka WAWATA kuonesha utayari wa kufanya tathmini ya maisha na utume wao katika Kipindi cha Miaka 50 iliyopita, tayari kumkaribisha Roho Mtakatifu ili aweze kupyaisha maisha na utume wao, kwa ari, imani na matumaini kwa siku za usoni! WAWATA saba walibeba vichwani mwao, nyungu zenye moto uliokuwa unawaka, alama ya Mapaji Saba ya Roho Mtakatifu. 1. Hekima ni kipaji cha Roho Mtakatifu cha kutusaidia tupende na kufurahia mambo ya Mungu. 2. Akili ni mwanga wa Roho Mtakatifu wa kutusaidia tumjue zaidi Mungu na ukamilifu wake pamoja na kuelewa ufunuo wake.

3. Shauri nii kipaji cha Roho Mtakatifu kinachotuelekeza kuchagua siku zote mambo yenye kufaa zaidi kwa sifa ya Mungu na kwa wokovu wetu. 4. Nguvu nii kipaji cha Roho Mtakatifu kinachotutia moyo wa kushika sana amri za Mungu na mambo ya utumishi wake tusiogope watu wala matukano wala mateso wala kufa. 5. Elimu ni kipaji cha Roho Mtakatifu kinachotutia maarifa ya mambo ya ulimwengu huu, kwa kutambua mapungufu yake pamoja na mitego, werevu na udanganyifu wa shetani akitujaribu mwenyewe au kwa kupitia vitu kama watu. 6. Ibada nii kipaji cha Roho Mtakatifu kinachotufanya tumpende Mungu kama Baba yetu mwema na watu wote kama ndugu; kwa msingi huo kutimiza utumishi wa Mungu na yote yale yenye kumpa Mungu sifa na heshima. 7. Uchaji wa Mungu ni kipaji cha Roho Mtakatifu kinachotutia hofu ya kumchukiza Mungu kwa dhambi kama vile mtoto mwema aogopavyo kumtia baba yake uchungu. Padre Wojciech Adam Koscielniak anakaza kusema, hii ilikuwa ni sehemu muhimu sana, kwa WAWATA kujiaminisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wao, tayari kuanza upya na kutembea kama Kanisa la Kisinodi wakijikita katika: Umoja, Ushiriki na Utume. Huo ndio mwamko mpya wa kitume kwa WAWATA Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma.  

Mwishoni mwa Ibada, waamini wamefanya maandamano kwenda kubariki Uwanja wa Ujenzi wa Jengo la Kitega Uchumi cha WAWATA Kiabakari “WAWATA JUBILEE COMPLEX”. Uwanja umebarikiwa na Padre Godfrid Maruru na Mama Evaline Malisa Ntenga akaweka jiwe la msingi la ujenzi huu ambao tayari umekwisha kugharimu takribani milioni 10 na hadi kukamilika kwake, Mwezi Novemba 2022 linatarajiwa kuwa limegharimu zaidi ya milioni 250 hadi 300. Parokia iliendesha harambee na jumla ya milioni 10 zilipatikana. Jengo hili litakuwa na maduka, ofisi za kupangisha na ukumbi wa chakula. Lengo ni kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi, ili kupambana na hali pamoja na mazingira yao hadi kieleweke!

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, WAWATA TAIFA, Kiabakari, Musoma!

FAMILIA KANISA DOGO LA NYUMBANI: Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Mama bora hufanya “make up” ya ubongo wa watoto wake kwa kupanda mbegu bora za akili, adabu, uwajibikaji na kwa kupanda elimu ya kumtambua Mwenyezi Mungu na jirani tangu wangali wakiwa wadogo. Mtoto aliyekosa make up ya ubongo toka kwa wazazi wake huwa na tabia mbaya ukubwani.

Baba bora mwenye hekima, busara, maarifa na uchaji wa Mungu ni chanzo cha faraja na nguzo ya kuegemea katika nyakati za shida na raha kwa mtoto, wakati Mama bora ni mzizi wa wema, unyenyekevu, adabu, upole, na kisima cha amani, upendo na mshikamano kwa watoto wake. Mama ni faraja na mwalimu wa kwanza wa tunu na maadili mema. Nawasihi sote tuungane na baba paroko katika kuwavuta Watoto wetu wa kike na wa kiume pia kukimbilia kanisani badala ya kutumia muda wao mwingi mtaani na kwenye mitandano. Mruhusu binti yako aungane na Watoto wenzake katika kuutafuta na kuumbata utakatifu wa maisha.

SIKU YA MASKINI DUNIANI 12 Nov 2021 “Maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi” Mk 14:7 ‘Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa.’ Luka 4:18. Baba Mtakatifu Francisko amegusia wasifu wa Mt. Francisko wa Assisi, umuhimu wa sala, ukarimu na utamaduni wa watu wa Mungu kukutana. Ni wakati wa kuondokana na tabia ya ubinafsi, umimi, kutowajali wengine na kuanza mchakato wa wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi.  Kumbe, kwa njia ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu, vikwazo vingi vinaweza kuvukwa na hivyo kujikwamua kutoka katika dimbwi la upweke hasi, majonzi na huzuni moyoni! Parokia ya Kiabakari Jimbo Katoliki la Musoma itajengwa na Wanakiabakari kama tukiungana pamoja, tukaweka nguvu, vipaji na rasilimali zetu pamoja na kuacha kusengenyana, kusemana vibaya na kunyoosheana vidole. Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwa namna ya pekee kuhusu ukombozi wa wanawake, ili kuwajengea nguvu ya kiuchumi tayari kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

MWAKA WA MTAKATIFU YOSEFU BABA MLISHI WA YESU: Bila shaka mtakumbuka kwamba, Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ulizinduliwa tarehe 8 Desemba 2020 na utahitimishwa tarehe 8 Desemba 2021. Waraka wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ni, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu”: Papa Francisko anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu kuwa ni “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika unyenyekevu Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika wa Bwana. Hizi ni sifa ambazo tunapaswa kuzimwilisha katika maisha, malezi na makuzi ya watoto wetu. Kuna maendeleo makubwa ya sayansi ya mawasiliano ya jamii yanayojidhihirisha kwa namna ya pekee katika matumizi ya: luninga, internet pamoja na mitandao ya kijamii, yanayochangia kwa kiasi kikubwa katika kulea dhamiri za watoto wadogo na vijana.

Matumizi mabaya ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii ni hatari sana katika kuunda dhamiri za watoto na vijana. Wazazi tujitahidi sana kuwa karibu na watoto wetu na hasa wale ambao wanatumia muda mrefu zaidi wakiwa mashuleni. Tujitahidi kuwafahamu vyema marafiki wa watoto wetu, ili tuweze kuwasaidia kukua katika njia njema inayozingatia kanuni maadili na utu wema! Wazazi tuwe mstari wa mbele kuwarithisha watoto wetu tunu msingi za Kiinjili, Imani na Mafundisho makuu ya Kanisa. Wazazi tukumbuke kusali na kuwaombea watoto wetu kwa Mwenyezi Mungu si tu wakati wa shida, bali uwe ni utamaduni wetu ili waweze kuwa ni watu wema; tuwafundishe pia kusali kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya utakatifu, haki, amani, upendo, msamaha na maridhiano.  Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walichangia kwa kiasi kikubwa malezi na makuzi ya Mtoto Yesu, dhamana na wajibu unaopaswa kuendelezwa na kutekelezwa na wazazi hata katika ulimwengu mamboleo. Mtoto Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli, kumbe alihitaji malezi ya kiutu katika ubinadamu wake; Baba na Mama walifanya kazi yao. Kumbe, wazazi na walezi tunapaswa kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya watoto wetu katika hatua mbalimbali, hasa wakiwa wangali wadogo, kwani waswahili husema, “Samaki mkunje angali mbichi, akikauka hakunjiki tena”. Wazazi na walezi wakiwekeza vyema kwa watoto wao hapana shaka kwamba, hata maisha yao huko mbeleni, yatakuwa ni ya heri na baraka tele

AMORIS laetitia: Katika Injili ya Marko12:29-31 inasema upendo ni “amri ya kwanza”. Katika kitabu cha Mathayo 22:36-40 biblia inasema upendo ni “amri kuu”. Tunaona upendo ni kitu cha msingi sana katika maisha yetu ya Kikristo! Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” kuanzia tarehe 19 Machi 2021 hadi tarehe 26 Juni, 2022 yanaongozwa na kauli mbiu “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu. Ni wakati wa kukuza na kuhamasisha wito wa kimisionari ndani ya familia, kwa kuwajengea wazazi na walezi uwezo wa kufundisha na kuwarithisha watoto wao: imani na tunu msingi za Kiinjili; kwa kuwaandaa kikamilifu tangu awali kushiriki na kujisadaka katika maisha ya ndoa na familia, bila kusahau wito wa Daraja Takatifu. Kumbe, maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni muda muafaka wa kuanza kuvuna matunda yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano katika medani mbalimbali za maisha: kikanisa na kijamii. Ni nafasi ya kutafakari changamoto, fursa na matatizo yaliyopo na kuendelea kuzifanyia kazi. Changamoto ni kuubali na kuupokea Wosia ambao umesheheni maneno ya ujasiri, chachu ya mabadiliko pamoja na mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi na watu wa Mungu.

Nukuu za Maneno ya wahenga: Sharon Farley alisema: “Nilipokuwa nazungumza na Mungu asubuhi moja, nilifikiria kile anachohitaji kutoka kwa watu. Hiki ndicho nilichokiandika: Watu watambue uwepo wangu, wanikiri, wajue ambalo nimelifanya, wajue ambalo naweza kufanya. Kunipa muda wao, kunisaidia, kunikubali, kujua kuwa ninakujali, kutotilia maanani lile ambalo hulielewi kuhusu mimi na kuniamini. Na Mungu aliniambia: ‘Sharon, tazama ulichokiandika, kisome mara mbili. Hiki ndicho nahitaji kutoka kwako.” Kwa ufupi sisi tutambue uwepo wa Mungu, tumkiri, tumpe muda wetu, tumkubali. Mungu alituumba tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike mbinguni.“Kutoshukuru ipo siku kunamuua mtunzi wake.” Ni methali kutoka Pwani ya Pembe. Kushukuru hakudhuru. Kudhuru ni kuharibu mwili au afya. Huwezi kuwa na kichomi sababu ya kushukuru. Huwezi kuvimbiwa kwa sababu ya kushukuru. Huwezi kuwangwa kichwa kwa sababu ya kushukuru. Huwezi kuwa na kichefuchefu kwa sababu ya kushukuru. Huwezi kuwa bubu kwa sababu ya kushukuru. Kutoshukuru kunadhuru. “Kutoshukuru ipo siku kunamuua mtunzi wake.”

Mtu asiye na shukrani anawaumiza wahitaji, kwa vile hayuko tayari kuwasaidia. Tunapoona siku yingine tuna sababu ya kushukuru, “tumepokea neema juu ya neema” (Yohane 1:16) Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea na neema juu ya neema. Kuishi mwezi mzima ni neema. Kuishi mwaka mzima ni neema.  Kushukuru kunatusaidia. Katika Kanisa Katoliki kuna sala isemayo, “Wewe huna haja na sifa yetu, lakini sifa hii ni kipaji chako tunachokurudishia kwa shukrani, maana nyimbo zetu za sifa hazikuzidishii kitu, bali zatufanya sisi kupata wokovu, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.” Tendo la huruma liwezekanalo leo lisingoje kesho “Kufikiri muda mrefu kufanya jambo fulani mara nyingine matokeo yake ni kutolifanya,” alisema Eva Young.  Kipaji kinatoka kwa Mungu, nyenyekea. Umaarufu unatoka kwa watu, washukuru. Majivuno yanatoka kwako, kuwa makini,” alisema John Wooden. “Uso wenye tabasamu hufukuza huzuni” (Methali ya Niger). “Kila mara unapokutana na mtu na kutabasamu, ni tendo la upendo, ni zawadi kwa mtu huyo, ni jambo zuri. Tukutane tukiwa tumevaa tabasamu, kwa vile tabasamu ni mwanzo wa upendo,” alisema Mama Theresa wa Calcutta.

Umepewa mdomo na uso mzima kuonesha tabasamu. Upendo unakomaa kwa kutoa. Licha ya kutoa pesa unaweza kutoa tabasamu. Upendo tunaotoa ni upendo tunaobaki nao. Namna ya kubaki na upendo ni kutoa upendo. “Unaweza kutoa bila kupenda lakini hauwezi kupenda bila kutoa,” alisema, Robert Louis Stevenson (1850 – 1894) mshairi kutoka Scotland. Umepewa ili kutoa.  Umepewa uso, midomo na meno basi toa tabasamu. Umebarikiwa kubariki. Kusema kweli haujavaa vizuri kama haujavaa tabasamu. “Kama hauwezi kufanya jambo lingine kumsaidia mtu, tabasamu tu,” alisema Eleanor Kirk. Maisha ni mafupi lakini tabasamu haichukui hata sekunde. Ni methali ya Cuba. Nukuu moja ya Yesu – HERI KUTOA KULIKO KUPOEA - Mdo 20:35. Kutoa ni utajiri. Kupokea ni Umaskini. Toa ukaribishe utajiri, huruma na upendo wa Mungu katika maisha yako! Wakatoliki wengi hatuna utamaduni wa kutoa sadaka kwa ukarimu, bali tunatoa mabaki! Tunapiga hesabu zetu mabaki ndio tunaleta Kanisani.

WAWATA
16 November 2021, 15:07