Tafuta

2021.11.23 Nadhiri za kwanza na za daima kwa Watawa wa Shirika la Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima(BMMMD) katika Parokia ya Kagondo,Jimbo Katoliki la Bukoba,Tanzania. 2021.11.23 Nadhiri za kwanza na za daima kwa Watawa wa Shirika la Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima(BMMMD) katika Parokia ya Kagondo,Jimbo Katoliki la Bukoba,Tanzania. 

Askofu Kilaini:Ufukara ni kuacha moyo wa ubinafsi,kushirikishana pamoja&kusaidiana

Wosia wa Kitume wa baaada ya Sinodi wa ‘Africae munus’ wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alioutia saini rasimi huko Cotounue nchini Benin umefikisha miaka 10.Katika Wosia huo pia unaelezakuwa nadhiri ya usafi wa moyo,ufukara na utii,maisha ya watu wa maisha ya wakfu huwa ushahuda wa kinabii.Ni katika roho hiyo iliyoongoza mahubiri ya nadhiri za kwanza na daima kwa watawa wa Shirika la Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima,Kagondo,Bukoba.

Na Sr. Angella Rwezaula- Vatican & Patrick P. Tibanga – Radio Mbiu.

Tarehe 20 Novemba 2021, Wosia wa Kitume wa baaada ya Sinodi wa ‘Africae munus’, wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI , ukiongozwa na kauli mbiu “ ninyo ni chumvi ya dunia... ninyi ni nuru ya ulimwengu”, alioutia saini rasimi akiwa huko Cotonou nchini Benin barani Afrika, umefikisha miaka 10. Hati hiyo kwa mujibu wa utamaduni wa kisinodi, ilikusanya hitimisho lasinodi ya maaskofu jijini Roma baada ya miaka miwili ya kufanya mchakato wa mang’amuzi wa Sinodi ya pili ya Afrika iliyokuwa imefanyika mwezi Oktoba 2009.

Katika kipengele kinachohusiana watu wa maisha ya wakfu, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI katika wosia huo anadika kuwa kwa njia ya nadhiri ya usafi kamili, ufukara na utii, maisha ya watu wa maisha ya wakfu huwa ushahidi wa kinabii. Kwa maan hiyo wanaweza kuwa mifano katika maeneo ya upatanisho, haki na amani, hata katika mazingira ambayo ni ya wasiwasi mkubwa. Maisha ya jumuiya hutuonesha kwamba inawezekana kuishi kama kaka na dada, na kuunganika licha ya tofauti zetu za kuzaliwa na rangi (rej. Zab 133:1). Maisha ya jumuiya yanaweza na ni lazima yawawezeshe watu kuona na kuamini kwamba leo barani Afrika, wanaume na wanawake wanaomfuata Kristo Yesu wanapata ndani yake siri ya kuishi kwa furaha pamoja: kupendana na muungano wa kidugu, unaoimarishwa kila siku na Ekaristi na sala ya Kanisa.

Ni katika roho hiyo  wakati wa mahubiri, ya Askofu msaidizi wa jimbo Katoliki la Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini katika katika Misa takatifu ya kuweka nadhiri za Kwanza na za daima kwa mabinti wa Shirika la Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima (BMMMD) katika Parokia ya Kagondo Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania mnamo tarehe 21 Novemba 2021 ametoa ushauri kwa wakristo wakatoliki kusaidiana wao kwa wao na kuwa maskini wa kiroho kwa kuacha ubinafsi na mambo ya kidunia badala yake wamtangulize Kristo katika kuutafuta ufalme wa mbinguni. Askofu Kilaini amesema kuwa, ufukara ni kuacha moyo wa ubinafsi, kushirikishana pamoja, kusaidiana na kwamba usafi wa moyo ni chombo ambacho mwanadamu anatumia kwa ajili ya kujishughulisha, kupeleka upendo kwa watu, kuwasaidia wahitaji na wasiojiweza pamoja na kupeleka faraja na matumaini kwa wengine na kujitoa maisha yao kwa ajili ya Mungu na watu wengine.

Askofu Kilaini akiwageukia  watawa wa kike na wakiume amewakumbusha jinsi ambavyo suala la kuwa watii kwa wakubwa na wadogo ni muhimu kwani  kwa kutii ni kuheshimu mahali popote watakapo pangiwa licha ya karama na uweredi walionao katika utume wa Kanisa na kwamba kupendana, kuishi pamoja, kuchukuliana, kubebana na kujaziana pale mwingine anapokosa ni alama na ishara ya ufanisi wa pamoja kuwashauri watawa walioweka nadhiri zao waishi vizuri mahali popote na yeyote watakayekutana naye katika utume wa Kanisa.

Kwa upande wake Askofu Desderius Rwoma wa jimbo hilo wakati wa kutoa shukrani zake aliwaomba Masista wa shirika hili (Shirika la Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima) hasa walioweka nadhiri ili waishi kadiri ya matakwa ya utawa na zaidi vema zaidi na  kuwashukuru wale wote wanaojitoa kwa ajili ya kusaidia na kuwezesha mashirika mbali mbali ya kitawa pamoja na kuwaomba wazazi na walezi kuwaruhusu watoto wao ili kujiunga na mashirika mbali mbali ya Kanisa kwaajili ya kumtumikia Mungu. Katika fursa ya nadhiri hizo, walikuwa wanovisi wawili waliowekwa nadhiri zao za kwanza ambao ni: Triphina Komugisha na Gisela Kokubanza; na walioweka nadhiri za daima ni Sr. Maria Devotha Kokusiima, Sr. Maria Emerenciana Mkaya na Sr. Maria Judith Mkarweikanisa.

Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba katika maadhimisho ya misa ya kufunga nadhiri kwa watawa
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba katika maadhimisho ya misa ya kufunga nadhiri kwa watawa

Katika Wosia wa Africae Munus, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, anasema watu wa maisha ya wakfu waendelee kuishi karama zao kwa ari ya kweli ya kitume katika maeneo mbalimbali yaliyoainishwa na waanzilishi wao! Kwa namna hiyo watakua zaidi na zaidi kuwa makini katika kutunza taa zao zikiwaka! Waanzilishi wa walitaka kumfuata Kristo kwa dhati na kuitikia wito wake. Zile kazi njema mbalimbali zilizo jitokeza kama matokeo ni nzuri kabisa ambazo hupamba Kanisa. Na hivyo ndivyo lazima waziendeleze kwa kufuata kwa uaminifu kadiri inavyo wezekana karama za waanzilishi wao, mawazo yao na mipango yao. Katika hilo alipenda kusisitiza Papa kuhusu mchango muhimu wa watu wa maisha ya wakfu katika maisha ya Kanisa na katika kazi yake ya umisionari. Wao ni msaada wa lazima na wa thamani kwa kazi ya kichungaji ya Kanisa lakini pia ni kielelezo cha uhalisia kwa kina kabisa wa wito wetu wa Kikristo. Kwa sababu hiyo, aliwaalika, watu wa maisha ya wakfu, kuendelea katika muungano wa karibu na Kanisa mahalia na pamoja na Askofu wa Roma.

Papa Mstaafa Benedikto XVI, alisistiza kuwa bara la  Afrika ni hori la maisha ya tafakari ya kikristo. Tangu nyakati za mwanzo katika Afrika ya Kaskazini, hasa Misri na Ethiopia, ilipata mizizi katika Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara wakati wa karne ya mwisho. Aliomba Bwana awabariki wanaume na wanawake ambao wameamua kumfuata bila masharti! Maisha yao yaliyofichika ni kama chachu katika unga. Sala zao za daima zitategemeza jitihada za kitume za maaskofu, mapadre, watu wengine wa maisha ya wakfu, makatekista na Kanisa zima. Maana mbalimbali za mabaraza ya kitaifa ya wakuu wa mashirika na wale wa COMSAM, husaidia kuvuta tafakari zao, sio tu kwa ajili ya  kufanikisha malengo ya hizo taasisi mbalimbali, wakati wanatunza uhuru wa kila mmoja wapo, tabia na roho ya kila moja peke yake, lakini pia ni katika kusaidia kufanya kazi kwa pamoja katika mazingira ya udugu na mshikamano. Inafaa kukuza roho ya kikanisa iliyo na msingi kwenye ushirikiano mzuri na mabaraza ya maaskofu.

ASKOFU KILAINI
23 November 2021, 15:26