Tafuta

Askofu Flavian Matindi Kassala Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amewataka wasomi Tanzania kuendeleza mchakato wa ukombozi wa watanzania katika medani mbalimbali za maisha. Askofu Flavian Matindi Kassala Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amewataka wasomi Tanzania kuendeleza mchakato wa ukombozi wa watanzania katika medani mbalimbali za maisha. 

Askofu Flavian Matindi Kassala Ujumbe Mahususi kwa Wasomi!

Askofu Kassala licha ya dhamana yake ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, ni mtaalamu wa shughuli za kichungaji kwa vijana. Kumbe, amewataka wahitimu kutoka Juco, Morogoro, kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema elimu, ujuzi na maarifa waliyopata kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa taaluma zao, wawaguse watanzania wengi zaidi!

Na Angela Kibwana, - Morogoro, Tanzania.

Wanajumuia wa Chuo kikuu kinachomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa wanapaswa kutambua kuwa wao ni wadau wakuu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo angavu wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Watambue kwamba, Chuo kikuu ni mahali ambapo vijana wanapata mwanga wa kuweza kufukuzia mbali giza la ujinga, ili hatimaye, siku moja wanafunzi hawa waweze pia kuwa ni mashuhuda wa nuru ya ulimwengu ambayo ni Kristo Yesu! Wanafunzi wajifunze kupata ujuzi, maarifa na stadi za maisha kwa kujikita katika upendo na ukarimu, kwani ufanisi wao mwisho wa siku, utapimwa kwa kuzingatia nyenzo hizi. Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, waweze kupata ufunuo wa ukweli wote ambao ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kumbe, kuna haja ya kukazia ari na mwamko wa kimisionari, tayari kutoka na kuanza kufanya tafiti za ukweli, ustawi na maendeleo ya wengi.

Chuo Kikuu kiwe ni mfano bora wa kuigwa katika ukarimu, huduma makini kwa wanafunzi, kwa kutafuta na kuambata mafao ya wengi, sanjari na kupambana na changamoto mamboleo kuhusu: utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, mifumo mbalimbali ya ubaguzi, ukosefu wa haki, amani, maridhiano sanjari na umaskini wa hali na kipato! Ni katika muktadha huu, Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, tarehe 13 Novemba 2021 ameongoza Ibada ya Misa takatifu, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mahafali ya tisa ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, JUCO, kilichoko Jimbo Katoliki la Morogoro. Askofu Kassala licha ya dhamana yake ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, ni mtaalamu wa shughuli za kichungaji kwa vijana. Kumbe, amewataka wahitimu kutoka Juco, Morogoro, kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema elimu, ujuzi na maarifa waliyopata kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wawe tayari kuchakarika kwa kugusa maisha ya watanzania wengi kadiri ya taaluma zao!

Elimu waliyoipata iwe ni chachu ya ukombozi, unaopaswa kuendelezwa katika mapana yake dhidi ya ujinga, magonjwa na umaskini wa hali na kipato! Lakini watambue kwamba, elimu walioipata inapaswa kwanza kabisa kuwapatia wao ukombozi. Huu ni wajibu unaowataka kuzingatia maadili mema, kanuni, sheria na taratibu katika kuihudumia jamii ya watanzania. Elimu hii, iwasaidie kukutana na binadamu wenzao wanaopaswa kuwahudumia kwa upole, nidhamu na moyo mkuu. Wawe ni watu wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, kwa nafasi na mafanikio mbalimbali waliyopata hadi kufikia hapa walipo! Watambue kwamba, si kwa nguvu wala jeuri yao, bali ni kwa neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wahitimu wanapaswa kuzingatia malengo na kamwe wasichanganye mambo! Hupatikanaji wa fursa za ajira ni changamoto pevu na hii isiwe ni sababu ya kubeza vyuo vilivyowalea na kuwapatia elimu. Kamwe wasipoteze mwanga na nuru ya elimu na malezi makini waliyopata wakati wote walipokuwa hapo chuoni asema Askofu Flavian Matindi Kassala. Wanaporejea sasa kwenye jamii, waoneshe ukomavu, uadilifu na utu wema na kamwe wasitake “kujimwambafai” ili watambulike kwa elimu ya juu waliyoipata!

Ipo hatari ya kudharauliwa na kubezwa kama soli ya kiatu, ikiwa kama watatanguliza majivuno, kwani majivuno ni kaburi la utu wema! Wahitimu waendelee kuwa ni watu wa sala na wachamungu, mabalozi wema na waaminifu wa JUCO, Morogoro! Watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwaminifu na mwema siku zote, kumbe, ni wajibu wao kujitahidi kuwa faida zaidi kwa jirani zao! Kwa upande wake, Maria Thomas, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, amewashauri wahitimu kujituma kwa kusoma alama za nyakati na kutumia fursa zilizopo kujitafutia ajira binafsi, ili kutekeleza ndoto zao. Hii itakuwa ni rahisi kuweza pia kulipia gharama za mikopo iliyowawezesha kumaliza masomo! Huo sio wakati wa kutwanga usingizi, vijana wasimame na kuanza kuchapa kazi, kazi isonge mbele, hadi kufikia malengo yaliyowekwa!

Askofu Kassala

 

17 November 2021, 15:41