Tafuta

Kanisa la Kisinodi ndilo wazo kuu la maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kati ya Mwaka 2021 hadi mwaka 2023: Umoja, Ushiriki na Utume ! Kanisa la Kisinodi ndilo wazo kuu la maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kati ya Mwaka 2021 hadi mwaka 2023: Umoja, Ushiriki na Utume ! 

Sinodi ya Maaskofu 2021-2023: Dhana ya Kanisa la Kisinodi!

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho haya yamegawanyika katika awamu kuu tatu kuanzia Mwezi Oktoba 2021-Oktoba 2023. Awamu ya kwanza ni kwa ajili ya Makanisa mahalia pamoja na taasisi zote zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki ni kuanzia tarehe 10 Mwezi Oktoba 2021 hadi Aprili 2022.

Na Padre Gaston George Mkude, Roma.

Amani na Salama! Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 10 Oktoba 2021 alizindua rasmi Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho haya yamegawanyika katika awamu kuu tatu kuanzia Mwezi Oktoba 2021 hadi Oktoba 2023. Awamu ya kwanza ni kwa ajili ya Makanisa mahalia pamoja na taasisi zote zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki ni kuanzia tarehe 10 Mwezi Oktoba 2021 hadi Aprili 2022. Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ni kuanzia Mwezi Septemba 2022 hadi Machi 2023. Awamu ya Tatu, Kanisa la Kiulimwengu ni kuanzia mwezi Oktoba 2023. Baba Mtakatifu anakazia ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, kukutana na kufanya mang’amuzi ya pamoja. Neno la Mungu ni ufunguo wa mang’amuzi na mwanga wa maisha ya kiroho, ili kweli maadhimisho ya Sinodi yaweze kuwa ni sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani. Hili ni tukio la neema na mchakato wa uponyaji unaotekelezwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, Kristo Yesu anawataka waamini kutomezwa na malimwengu; kuwa wazi kwa kuendelea kusoma alama za nyakati ili kuondokana na tabia ya kutekeleza shughuli za kichungaji kwa mazoea, ili hatimaye, kutambua kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka kwa ajili ya Kanisa lake katika nyakati hizi na wapi anataka kulipeleka.

KANISA LA KISINODI, ndio wazo kuu la Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa tarehe 10 Oktoba 2021 na kwa ngazi ya kijimbo, tarehe 17 Oktoba 2021 na hatimaye katika ngazi ya Kanisa zima mjini Roma itakuwa ni Oktoba mwaka 2023. Kwa kweli ni wazo kuu lenye kubeba maneno makuu mawili, yaani, KANISA na SINODI. Na labda yawezekana ni maneno tunayoyasikia na kuyatumia mara nyingi katika misamihati yetu ya kidini, lakini tusiwe na maana kamili ya maneno haya. Kwanza nianze kwa kusema, Kanisa ni “Qahal” kwa Kiebrania na kwa Kigiriki ni “Ekklesia”, zote zikiwa na maana ya kusanyiko la watu wa Mungu, wanaounganishwa na imani moja kwa njia ya Ubatizo, Sakramenti za Kanisa na Neno la Mungu, pamoja na Mapokeo matakatifu. Kanisa ni jumuiya ya wabatizwa, hivyo, hakuna aliye wa muhimu kuzidi mwingine linapokuja swala la Kanisa, tofauti zetu za nafasi za utumishi ndani ya Kanisa, hazitufanyi kuwa wa muhimu au wenye nafasi ya kwanza kuliko wengine. Kanisa sio Baba Mtakatifu, au maaskofu, au wakleri, au watawa au mtu mwingine yeyote yule, bali sisi sote wabatizwa kila mmoja anafanyika jiwe hai katika kuujenga Mwili fumbo wa Kristo, na ndio Kanisa la Kristo.

Neno la pili ninalopenda kulitumia leo ni “Sinodi”, ni neno la Kigiriki linalotokana na muunganiko wa maneno mawili ya lugha hiyo, yaani, “syn” na “hodos”. Maneno haya mawili, “syn” likiwa na maana ya “pamoja” na “hodos” likiwa na maana ya “safari/mwondoko”. Hivyo, Sinodi ni kutembea kwa pamoja, kuwa na mwondoko mmoja kwa pamoja, ni kusafiri kwa kushikana mikono bila kumwacha yeyote yule nyuma. Sinodi, basi, inaakisi maana ya kuwa Kanisa, kama nilivyojaribu kuonesha hapo juu. Kanisa kwa asili yake ni la Kisinodi, maana ni jumuiya, sio mali ya yeyote yule bali sote tunaunganishwa na Mungu Roho Mtakatifu na kufanyika ukoo wa kikuhani na wa kifalme, watu wa milki ya Mungu. Sinodi basi pia ni mkutano au kusanyiko unaoweza kuitishwa katika ngazi ya kijimbo, yaani na Askofu mahalia, au katika ngazi ya Kanisa zima ambapo ni Baba Mtakatifu mwenye uhalali wa kuitisha mkutano kwa Kanisa zima, kama huu unaofanyika kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2023 huko Roma.

Sitaingia katika Taalimungu ya Sinodi wala historia yake katika Kanisa, itoshe tu kutambua kila mmoja wetu anaalikwa kuwa mwanaushirika, mshiriki na pia mmisionari wa kuwa shahidi wa Habari Njema ya Wokovu wetu katika nyakati na ulimwengu wetu wa leo. Baba Mtakatifu Francisko leo anatualika na hasa Dominika tarehe 17 Oktoba, 2021 kuzindua katika ngazi ya Kijimbo Sinodi ya Maaskofu yenye agenda juu ya “Kanisa la Kisinodi”. Ni shauku na hamu ya Baba Mtakatifu kama ilivyokuwa hamu ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kutembea na kuwa na mwondoko wa pamoja kama wabatizwa. Ndio mwaliko wa kila Mbatizwa kuwa mshiriki katika safari yetu kama wanakanisa, asibaki hata mmoja nyuma, na pia asiwepo hata mmoja mbele au peke yake, sote tunaalikwa kuishi kama kaka na dada, kama ndugu na ndio jumuiya ya waamini wanaojaliana na kusaidiana katika nyanja zote za maisha. Tumefanyika ndugu sio kwa damu na nyama bali kwa Ubatizo wetu katika Fumbo Utatu Mtakatifu, kwa kushiriki fumbo lile la Ukombozi wetu.

Kanisa la Kisinodi, ndilo Kanisa la “Koinonia”, neno la Kigiriki likiwa na maana ya “Ushirika/umoja”, kama tunavyoliona Kanisa lile la mwanzo kabisa kama tunavyosoma katika (Kitabu cha Matendo ya Mitume2:42 na 1Yohane 1:3). Baba Mtakatifu Francisko anataka kuamsha ndani mwa kila mwamini mkatoliki wa hali zote popote ulimwengu awe mshiriki muhimu katika Sinodi ya XVI ya Maaskofu, ndio kusema kila mmoja wetu leo anaalikwa kutoa mawazo na mchango wake mintarafu misheni ya Kanisa katika ulimwengu na nyakati hizi zetu. Sinodi ya Maaskofu itakayofanyika mwaka 2023 huko Roma, inapaswa kutanguliwa kwa kusikilizana kuanzia ngazi za familia zetu, jumuiya zetu ndogondogo, vigango, parokia, majimbo na hatimaye Kanisa la ulimwengu mzima. Ndio kusema Baba Mtakatifu anatukumbusha na kutualika kujitafakari tena kuwa Kanisa ni la Kisinodi, ni kusanyiko la wanaotembea kwa pamoja kwani aliye NJIA, UKWELI na UZIMA wetu, ndiye Yesu Kristo mwenyewe. (Yohane 14:6)

Baba Mtakatifu Francisko anatualika kwa pamoja kutafakari janga la UVIKO-19, duniani, anasema dunia ni kama mtumbwi unaosafiri kwa pamoja, shida ya mmoja tumeona inavyogusa ulimwengu mzima. Janga hili si tu limetunyenyekesha na bado linaendelea, lakini tumeweza kutambua hakuna namna hata mmoja anayeweza kuishi peke yake kama kisiwa, mwanadamu anamhitaji mwanadamu mwingine, tunahitajiana bila kujali hali zetu na tofauti zetu mbalimbali. Mwanadamu ni familia moja bila kujali imani zetu, rangi zetu, uchumi wetu na kadhalika na kadhalika. Hivyo ukombozi wa mwanadamu unatutaka sote kushikamana iwe kiroho na hata kimwili (Solidality is indispensable). Na ndio maana Baba Mtakatifu leo anatualika kutafakari kwa pamoja juu ya dhana ya Kanisa la Kisinodi. Kanisa lisilomuacha mtu yeyote nyuma au peke yake awe ni tajiri au maskini, sisi sote hatuna budi kutambua na tunaalikwa kutembea na kuwa na mwondoko wa pamoja katika nyanja zote.

Ni mwaliko wa Baba Mtakatifu Francisko kujihoji kama wanakanisa kwani anasema mwondoko wa pamoja kama Kanisa la Kisinodi ndio jambo tunaloitiwa na Mungu kuliishi katika Milenia hii ya tatu. Wito huu uliosisitizwa sana na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unabaki kuwa ni zawadi kwetu na wakati huu unatudai kuwajibika kwa pamoja, kujitafakari kwa pamoja na kuona njia bora zaidi za kuweza kuishi ushirika, ushiriki na umisionari wetu katika kutekeleza misheni mama ya Kanisa, ndio ile ya kumkomboa kila kiumbe. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kutualika, ni kwa njia ya kumsikiliza Mungu Roho Mtakatifu, kama Kanisa tunaweza kufikia kupata majibu na majawabu ya kuishi wito huu wa Kanisa la Kisinodi, Kanisa linalosafiri na kutembea kwa pamoja kwa mwondoko mmoja. Baba Mtakatifu Francisko anatualika kusoma alama za nyakati, ulimwengu tunaoishi leo na kufanya tathmini ya mambo mazuri na hata yale yanayokuwa hasi pia. Kuona ni kwa namna gani kama Kanisa tunaweza kuishi na kuwa na majibu ya changamoto za leo.  Kusoma alama za nyakati na kupata majibu yake kadiri ya Injili ya Yesu Kristo na kamwe kama Kanisa hatupaswi kuanza kufuata mantiki na matakwa ya ulimwengu huu.

Pamoja na kushindwa kuwa waaminifu kwa Mungu, lakini anazidi kusema Baba Mtakatifu Francisko kuwa Roho wa Mungu kamwe haliachi Kanisa, kwani anabaki kutembea nasi na kutujalia uzima wa kweli. Hivyo, hatuna budi kujifunza kumsikiliza Mungu Roho Mtakatifu anayetusaidia kuujua ukweli wote. Kanisa halina budi kujiangalia tena na hasa kujali waamini wake wanaopitia nyakati ngumu za madhulumu makubwa yanayopelekea hata umwagaji wa damu. Kanisa linapaswa kwa ujasiri wote kuwa sauti ya hawa wanaoteseka na kudhulumiwa. Kanisa linapaswa kuwa sauti ya wasio na sauti, kuwa mtetezi wa wanyonge kwani ndio utume wake na kinyume chake ni kupotoka. Maskini wanapaswa kuwa na nafasi ya kwanza katika huduma za Kanisa na yafaa katika jumuiya zetu, vigango na maparokia na hata majimbo kujitathmini kuhusu mipango gani tunayo kuwasaidia wanaokuwa wahitaji wa kweli wanaotufikia au tunaoishi nao siku kwa siku. Zipo parokia zinazokuwa na mipango maalumu jinsi ya kuwafikia wale wanaokuwa katika hali duni kabisa iwe ni maskini, yatima, wagonjwa na wazee. Tusiwe Wakristo wa Dominika tu bali tuishi Injili ya Kristo katika maisha yetu ya kila siku.

Kanisa la Kisinodi, ni Kanisa la Kimisionari, ni Kanisa linalotumwa kutoka, na hivyo ni Kanisa lenye milango wazi. Ni Kanisa linalojua kusikilizana na kujadiliana na hivi likiongozwa na Roho Mtakatifu na kweli za Injili kuona namna bora zaidi ya kutumiza utume wa kimisionari hapa ulimwengu katika nyakati zetu. Sio Kanisa linalojifungia na kujitenga, linalobaki kuishi nyakati za kale, bali narudia daima kwa kuongozwa na Mungu Roho Mtakatifu, Neno la Mungu na Mapokeo likisafiri kwa pamoja katika kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kanisa la Kisinodi, ndio lile linalobaki katika kusikiliza Neno la Mungu. Ni Mungu anayeliongoza Kanisa lake hata leo, hivyo daima ni Kanisa linalosafiri kwa pamoja katika kuiishi Injili. Kanisa ili liweze kutekeleza misheni yake ya kuwa Kanisa la Kimisionari halina budi kujifunza mara zote bila kukoma Neno la Mungu, kwani ni humo ndio linapokea misheni yake, linapokea Habari Njema ya kwenda kuwashirikisha wengine. Mmisionari anatoka anakwenda kuwashirikisha wengine upendo na huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Ni mmoja anayekutana kwa nafasi ya kwanza na Mungu mwenyewe, na hivyo furaha na shauku ile anatoka nayo na kwenda kuwashirikisha wengine pia.

Kanisa la Kisinodi anasema Papa Francisko, ni Kanisa linalofanya toba na wongofu wa ndani ambao ni endelevu. Ni Kanisa linalotambua madhaifu na madhambi yake, linatambua kuwa bado lipo safarini na hivi kwa pamoja kwa msaada wa Mungu Roho Mtakatifu, linachuchumilia na kuutafuta utakatifu kwa pamoja. Ni Kanisa linalokuwa na lengo moja kuu nalo si lingine bali ni UTAKATIFU KWA PAMOJA. Ni Kanisa linalohubiri na kuwasaidia wote kupata wokovu, ndio kuwa rafiki wa Mungu na jirani. Ni Kanisa linalompenda Mungu na viumbe vyake vyote, ndilo Kanisa linalojali pia utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, kwani Dunia ni mama yetu, ni nyumba yetu ya pamoja anasema Papa Francisko. Baba Mtakatifu Francisko anatualika kuanza kujifunza kwa pamoja kuishi Kanisa la Kisinodi kuanzia katika ngazi za chini kabisa iwe ni familia, jumuiya, kigango, parokia, jimbo mpaka Kanisa zima la Kiulimwengu. Anatupa muongozo wa jinsi ya kuanza kulitekeleza hilo kwa kutupa japo dhana kumi za kufanyia kazi.

Wasafiri wenza: Kila mara na kila mmoja wetu hana budi kuwatambua wale anaopaswa kusafiri nao pamoja ni akina nani. Kusikilizana: Bila kuongozwa na maamuzi mbele katika maisha yetu, hatuna budi kujifunza kuwa watu wa kusikiliza wengine, kuwa wazi ili kujifunza na kupokea kutoka kwa wengine. Kusemezana: Ni baada ya kumsikiliza mwingine nasi tunaalikwa kuwa wawazi na wa kweli katika kuwashirikisha wengine kile kinachokuwa ndani mwetu. Na hapa tunaalikwa kuepuka uoga na unafiki, tusemezane kwa upendo na ukweli. Kuadhimisha kwa pamoja: Hasa Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu. Kanisa la mwanzo lilidumu katika kushika fundisho na katika ushirika wa kuumega mkate kwa pamoja. Kushirikishana utume wa Kanisa: Utume wa Kanisa sio wa watu fulani tu bali ni wa kila mbatizwa. Kujadiliana ndani ya Kanisa na pia na jamii: Kanisa linaalikwa kujadiliana iwe ndani yake lakini pia hata na jamii yetu ya leo inayotuzunguka. Kamwe Kanisa haliitwi kujifungia ndani kwani jamii inaundwa pia na wanakanisa. Ni wajibu wa Kanisa la Kisinodi kujifunza namna njema na nzuri ya kujadiliana ndani na zaidi sana na tamaduni zetu za nje katika jamii zetu.

Majadiliano ya Kiukumene: Waaamini wengine wabatizwa wasio Wakatoliki ambao tunaunganishwa nao kwa Ubatizo mmoja, hatuna budi nao kusafiri nao kwa pamoja kwa njia ya majadiliano na maridhiano. Uongozi na ushirikishaji: Kanisa halina budi kujiangalia na kujitathmini ndani yake juu ya dhana ya uongozi, Je ni utumishi au ni utawala? Kung’amua na Kuamua: Kanisa la Kisinodi linafikia maamuzi yake kwa njia ya kufanya mang’amuzi kwa msaada wa Mungu Roho Mtakatifu. Kujifunza kuishi Kisinodi: Kuishi kwa kutembea kwa pamoja katika ngazi zote. Nisifanye andiko hili kuwa refu bila sababu itoshe kusema tutembee pamoja kama Kanisa na kuzidi kuimarishana katika imani yetu, hatuwezi peke yetu bila neema na msaada wake Mungu katika kuishi kweli za Injili. Ushirika na Mungu kwa nafasi ya kwanza, kwa njia ya Ubatizo na masakramenti na pia ushirika na wabatizwa wengine wote, na ndio ushirika na ushiriki ndani ya Kanisa.

18 October 2021, 08:44