Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni. Kauli mbiu "Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia" Mdo 4:20. Jimbo Katoliki Iringa Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni. Kauli mbiu "Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia" Mdo 4:20. Jimbo Katoliki Iringa 

Siku ya Kimisionari Jimbo Katoliki Iringa Na WAWATA Jubilei ya Miaka 50 ya Utume!

Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa amekazia mambo makuu matatu: Historia ya ukombozi, ushiriki wa Wakristo katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Amezindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ngazi ya Kijimbo! Utume wa walei!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2021 yalinogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tanzania katika maadhimisho haya alikazia mambo makuu matatu: Historia ya ukombozi, ushiriki wa Wakristo katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ametumia Siku hii kama sehemu ya uzinduzi kijimbo wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA. Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa katika mahubiri yake amewakumbusha waamini kwamba, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho anataka watu wote waokoke kutoka katika lindi la dhambi na mauti, wapate kujua yaliyo kweli. Rej. 1Tim 2:4. Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu ameshuka na kukaa kati ya watu wake na hivyo Kristo Yesu amekuwa ni ndugu na rafiki yao. Kristo Yesu ni mpatanishi kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Upatanisho huu umefanyika kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Mdo 4:12.

Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2021 yalinogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa anasema, maadhimisho haya ni sehemu ya utekelezaji wa Agizo la Kristo Yesu aliyewaambia wafuasi wake “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” Mk 16: 14-16. Wakristo wote watambue kwamba, wao ni watume wamisionari na kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wamekuwa mashuhuda na Mitume wa Habari Njema ya Wokovu. Habari Njema ya Wokovu ni chimbuko la upendo, msamaha, uadilifu na utakatifu wa maisha. Huruma, upendo na msamaha wa Mungu unapaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wote pasi na ubaguzi, ili watu wa nyakati zote waweze kuguswa na kweli za Kiinjili. Wakristo ni mashuhuda wa imani tangu Yerusalemu hadi miisho ya dunia. Wanapaswa kuhakikisha kwamba Kristo Yesu anaingia katika historia na maisha ya binadamu kwa kumuishi Kristo kwa njia ya maisha adili na matakatifu. Maisha ya kila mwamini yaweze kumwadhimisha Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Maisha yao adili na matakatifu yaweze kumwinua, kumtukuza na kumpatia sifa na utukufu wake. Waamini katika maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni wanahimizwa kusali kwa ajili ya kuombea mchakato na juhudi za kimisionari ziweze kuzaa matunda ya toba na wongofu wa ndani. Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa amewaalika waamini kuchangia kwa furaha na moyo wa ukarimu kwenye Mfuko wa Pamoja wa Uinjilishaji (Universal Solidarity Fund). Wakumbuke kwamba “Apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu” (2 Kor 9:6.) Kumbe, Sala, Ukarimu na Sadaka zisaidie juhudi za Mama Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji mpya na wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Waamini wajitahidi kumwomba Kristo Yesu ili aweze kuwaondolea upofu wa imani kama ilivyokuwa kwa Bartimayo Mwana wa Timayo. Ili kwamba, wakisha kupata neema ya kuona, waweze kuwa na ujasiri wa kumfuasa Kristo Yesu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA hivi karibuni ilizindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC lilipoanzisha WAWATA kunako mwaka 1972 katika ngazi ya Kitaifa. Jubilei ni kipindi cha kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake kwa WAWATA katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita. Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, ili kuomba msamaha, neema na baraka ya kusonga mbele tena kwa ari na moyo mkuu katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2021 amezindua Maadhimisho haya katika ngazi ya Kijimbo. Amewapongeza na kuwashukuru WAWATA kwa upendo, sadaka na uvumilivu katika maisha na utume wao. Na kwa njia ya fadhila hizi, wameweza kuikumbatia familia na maisha ya binadamu. Amewataka WAWATA kwa upendo wa Kristo waendelee kutumikia na kuwajibika. Kanisa lina deni kubwa la shukrani kwa WAWATA!

Wanawake Wakatoliki wamekuwa mstari wa mbele katika malezi na makuzi ya Jumuiya mbalimbali za Kikristo. Wameendelea kuvumilia, kutumikia na kuwajibika kwa kufuata mfano wa wanawake watakatifu na waadilifu wanaotajwa kwenye Maandiko Matakatifu na katika Historia ya maisha na utume wa Kanisa. Wanawake hawa ni mfano bora wa imani, matumaini, malezi, maisha adili na matakatifu. Lakini kati ya wanawake wote kwenye Maandiko Matakatifu na Historia ya Kanisa, Bikira Maria anang’ara zaidi. Wakristo wanaitwa na kutumwa kujenga Ufalme wa Mungi. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani kwenye ufunuo wa Kristo Yesu.

Jimbo Katoliki Iringa

 

 

26 October 2021, 16:01