Tafuta

Padre John Soranga Massawe AJ. 10 Juni 1932 - 16 Oktoba 2021: Muasisi wa Shirika laWatumishi wa Yesu na Maria! Amewahi kuwa Mkuu wa Shirika na Gambela wa Uru Seminari, Moshi. Padre John Soranga Massawe AJ. 10 Juni 1932 - 16 Oktoba 2021: Muasisi wa Shirika laWatumishi wa Yesu na Maria! Amewahi kuwa Mkuu wa Shirika na Gambela wa Uru Seminari, Moshi. 

Padre John Soranga Massawe, AJ. 1932 - 2021: Muasisi wa Shirika!

Padre John Soranga Massawe, AJ, alizaliwa mwaka 1932 Jimbo Katoliki la Moshi. Tarehe 15 Agosti 1965 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baadaye alijiunga na Shirika la Mitume wa Yesu na kuweka nadhiri za kwanza mwaka 1976 na nadhiri za daima mwaka 1980. Baada ya kulitumikia Shirika la Mitume wa Yesu kama Gambera na Mkuu wa Shirika. Mwaka 1997 akaanzisha Shirika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu.

Mheshimiwa Padre Angelo Betteli, Fdcc, Msimamizi wa Kitume wa Shirika la Mitume wa Yesu, “Apostles of Jesus, AJ.” anasikitika kutangaza kifo cha Padre John Soranga Massawe, AJ. Muasisi wa Shirika la Watumishi wa Yesu na Maria, aliyefariki dunia tarehe 16 Oktoba 2021 kwenye Hospitali ya Mtakatifu Gemma, Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania. Askofu mkuu Beatus Kinyaiya OFM. Cap., wa Jimbo kuu la Dodoma, tarehe 21 Oktoba 2021 anatarajiwa kuongoza Ibada ya mazishi na hatimaye mazishi kwenye Kituo cha Miuyuji alichoakianzisha yeye mwenyewe. Hayati Padre John Soranga Massawe aliwahi pia kuwa ni Mkuu wa Shirika la Mitume wa Yesu. Itakumbukwa kwamba, Padre John Soranga Massawe, AJ, alizaliwa tarehe 10 Juni 1932 Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 15 Agosti 1965 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Moshi. Baadaye alijiunga na Shirika la Mitume wa Yesu lililokuwa limeanzishwa hivi punde na kuweka nadhiri zake za kwanza tarehe 16 Julai 1976. Nadhiri za daima akaweka tarehe 15 Agosti 1980.

Baada ya kulitumikia Shirika la Mitume wa Yesu katika ngazi mbalimbali kwa mfano Gambera na Mkuu wa Shirika, kunako tarehe 18 Septemba 1997 alianzisha Shirika la Watumishi wa Yesu na Maria. Ni mtanzania wa kwanza mzalendo kuthubutu kuanzisha Shirika la Mapadre na Mabruda, ili kujikita katika mchakato wa uinjilishaji hususan miongoni mwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii! Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima”. Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo!

Wanafunzi waliopitia mikononi mwa Padre John Soranga Massawe wakati wa malezi na majiundo yao ya kikasisi alipokuwa Uru Seminari Jimbo Katoliki la Moshi kama Gambera, wanamkumbuka sana kwa malezi na makuzi yake yaliyosheheni upendo wa kibaba! Alikuwa ni Padre mwenye ibada ya pekee sana kwa Bikira Maria, kiasi kwamba, matukio mbalimbali katika maisha na utume wake, aliyafasiri kama sehemu ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Aliwafundisha kusali kwa imani na matumaini. Aliwafundisha na kuwajengea moyo wa kuchapa kazi kwa: bidi, juhudi na maarifa, ili waweze kujitegemea katika maisha. Aliwataka kuwa watiifu, waaminifu, waadilifu na wachamungu. Kwa malezi haya vijana wengi waliopitia mikononi mwake, wakafanikiwa kuwa Mapadre au waamini walei, wanasema, maisha yamewanyookea, yaani ni mazuri na wanaweza kumudu mazingira katika maisha yao!

Padre John Massawe
19 October 2021, 15:04