Tafuta

Siku ya Kimisionari Ulimwenguni kwa Mwaka 2021: Utume wa Wanawake ndani ya Kanisa! Siku ya Kimisionari Ulimwenguni kwa Mwaka 2021: Utume wa Wanawake ndani ya Kanisa! 

Wito na Dhamana ya Wanawake Katika Maisha na Utume wa Kanisa

Mama Evaline Malisa Ntenga anatafakari kuhusu dhamana ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Anabainisha sifa za mwanamke wa shoka! Anatoa mifano ya baadhi ya wanawake ambao wamejipambanua katika utume wa Kanisa kwa kutumia rasilimali fedha, muda na vipaji vyao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia! Yaani!

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, WAWATA TAIFA, - Dar es Salaam.

Wanawake wanapaswa kushirikishwa kikamilifu ili waweze kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Bila mchango wa wanawake, Kanisa litapoteza nguvu yake ya kujipyaisha tena. Dhamana na utume wa wanawake ndani ya Kanisa unajidhihirisha wazi kwa njia ya Bikira Maria, Nyota ya Uinjilishaji mpya. Kumbe, Kanisa linapaswa kushikamana pamoja na “wanawake wa shoka” ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanarithisha: imani, tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii kwa watoto wao.Wanaume na wanawake, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wapendane na kukamilishana; bila kuwadharau, kuwabeza na kuwanyanyasa wanawake. Wanawake washirikishwe pia katika malezi na majiundo ya Majandokasisi. Sauti ya wanawake, inapaswa kusikilizwa ndani ya Kanisa. Mababa wa Sinodi wanasema, wanawake ni rasilimali muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake washirikishwe katika mchakato wa kufanya maamuzi katika maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria awe ni mfano bora katika shule ya ufuasi wa Kristo Yesu. Vijana wawe ni nyota ya Msamaria mwema kwa njia ya huduma; nyota ya umisionari, matumaini na majadiliano ya kidini na kiekumene.

Kimsingi, Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, dhamana na utume wa wanawake katika Kanisa hauna budi kuimarishwa, kwa kukazia zaidi makuzi, malezi na majiundo ya awali, endelevu na fungamani, ili kuondokana na mfumo dume unaowanyima wanawake haki zao msingi. Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni mambo muhimu katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu. Katika makala haya kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Duniani kwa Mwaka 2021 Mama Evaline Malisa Ntenga Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA anatafakari kuhusu dhamana ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Anabainisha sifa kumi na tano za mwanamke wa shoka! Anatoa mifano ya baadhi ya wanawake ambao wamejipambanua katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutumia rasilimali fedha, muda na vipaji vyao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Anauangalia mchango wa baadhi ya wanawake katika Agano la Kale na Agano Jipya pamoja na kutoa ujumbe kwa wanawake wakatoliki kama sehemu ya ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa. Anabainisha aina mbalimbali za Utume zinazoweza kutekelezwa na wanawake katika safari ya maisha yao hapa duniani!

Utangulizi: Mwanamke ni nani? Mwanamke, kama alivyo mwanaume, ni kiumbe wa Mungu mwema sana. Ameumbwa katika sura na mfano wa Mungu (Mwa 1: 26-31). Yeye (pamoja na mwanaume) amepewa wajibu wa kutunza uumbaji ili furaha ya Mungu idhihirike daima. Mwanamke katika utajiri wake amepewa zawadi na Mungu. Zawadi hiyo ni sifa kemkem zinazomtambulisha na kumwelezea katika mapana na marefu yake. Sifa hizo, lakini, hazimfanyi mwanamke kuwa bora zaidi ya mwanaume kama vile pia mwanaume asivyo bora kuliko mwanamke. Kila mmoja anamhitaji mwenzake katika jukumu lao kubwa la kuitunza kazi ya Uumbaji na kuitiisha nchi. Sifa zenyewe ni kumi na tano (15). Kupenda kuzaa na kutunza uhai; kwa sifa hii wanawake hulia sana mtu akifa na huangaika sana wakikosa watoto. Mifano: Sara mkewe Ibrahim, Hana Mama yake Samwel, na Elisabeth. Uvumilivu wa Malezi – kwa sifa hii wanawake wamepewa uwezo mkubwa wa kuketi kwa muda mrefu bila ya kujitingisha tofauti na wanaume. Huvumilia sana maumivu na adha ziambatanazo na ujauzito pamoja na kulea kwa uangalifu mkubwa watoto wachanga. Upole na Amani: kwa sifa hii wanawake hujitahidi kuepusha na kuepuka mambo yote yanayoweza kusababisha fujo, vurugu na kutoweka kwa amani katika familia au jamii waliyomo. Wanaona shida mapema: wana lepe kama mlango wa sita wa fahamu – kwa sifa hii wanawake wamepewa uwezo wa kuhisi na kuona shida au hitaji fulani kabla ya wanaume.

Mfano mzuri ni Mama Bikira Maria kwenda kumtembelea Elisabeth na kumhudumia maana aliambiwa ana mimba ya miezi sita katika uzee wake. Ingawa hakuagizwa kwenda kumsaidia yeye kama mwanamke aliiona shida iliyokuwwa mbele yake binamu yake huyo. Tukio jingine ni kwenye Harusi ya Kana ya Galilaya. Bikira Maria pia aliona tatizo la wageni kuishiwa kinywaji japo yeye alikuwa hanywi. Wanaume walikuwa hawajashtuka juu ya hilo. Mwanamke huyu aliliona tatizo na kusababisha Kristo Yesu kutenda muujiza wake wa kwanza, furaha ya wanandoa iliyoanza kuingia mchanga ikarejea tena! Kutuliza na kufariji,mifano mizuri ni Veronika na Wanawake wa Yerusalemu katika njia ya Msalaba aliyoifuata Yesu. Lakini pengine wanawake hupenda kufarijiwa. Ni mabingwa wa kusikiliza na hasa wakati huu wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, tunahamasishwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini na mfano mzuri ni wa Bikira Maria. Alikuwa akisikiliza kwa makini na kuyaweka moyoni (kutafakari) (Lk 1: 26-38). Hupenda kusimulia – mfano mtu wa kwanza kupewa habari za ufufuko wa Yesu Kristo ni mwanamke. Maria Magdalena alipewa habari za ufufuko na kuzisimulia vizuri (Lk 24: 10) akabahatika kupewa neema ya kuwa ni Mtume wa kwanza kutangaza na kushuhudia Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Wanabidii ya Kazi nyingi ndogondogo na kuzisimamia vizuri (multichannelled) Kuteka wengine (Wanaume) hii ni hatari sana! Wanaume wanapaswa kuwa macho zaidi!

Maisha ya Pauline Jaricot Mwanzilishi wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimisionari (PMS) alijikita katika sala na matendo ya huruma. Tarehe 3 Mei 2022 itakuwa ni siku muhimu katika historia ya Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimisionari (PMS) kwani mwaka 2022 yanatimiza miaka 200 tangu kuanzishwa kwake rasmi kwanza kama Chama cha kitume cha kukuza Imani. Kuanzia Jumatatu tarehe 3 Mei 2021 Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimisionari yameanza maandalizi ya sherehe hizo za 2022, kwa kutazama kwa kina vyanzo vya karama ya mwanzilishi wake ambaye ni mwamini mlei, Pauline Maria Jaricot. Mtumishi wa Mungu Pauline Maria Jaricot alizaliwa huko Lione nchini Ufaransa, tarehe 22 Julai 1799, baada ya kupitia wakati mgumu wa ujana wake kwa sababu ya kuanguka na kumsababisha madhara makubwa ya kimwili, mwanamke huyo alihisi ndani mwake wito wa kimisionari. Tarehe 3 Mei 1822 pamoja na kikundi cha wanawake, walinzisha chama cha kukuza imani, na ambacho baadaye kikaridhiwa na Papa Pio VII mnamo 1823. Pauline alijikita kwa dhati kuhudumia maskini na wagonjwa, akiwatembelea kila siku katika Hospitali na watu wenye magonjwa ya muda mrefu!

Msaada kwa walio na mahitaji msingi ulikuwa umesindikizwa kwa maisha ya sala ya kina. Kila siku alipokea Ekaristi, alikuwa akiwaombea uongofu wa wadhambi na uinjilishaji ulimwenguni. Mauti yalimjia akiwa maskini huko Lione mnamo tarehe 9 Januari 1862. Mnamo tarehe 25 Februari 1963 alitangazwa kuwa Mtumishi wa Mungu na Mtakatifu Yohane XXIII. Tarehe 26 Mei 2020 Papa Francisko ameridhia mchakato wa kutangazwa kuwa Mwenyeheri, kufuatia na muujiza kwa njia ya maombezi yake. Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimisionari (PMS) yameenea katika nchi 130 Ulimwengu ambalo linahesabu wamisionari 354,000, makatekista milioni 3 na majimbo 114 katika maeneo ya kimisionari. Milioni 150 za dola ambazo zinahudumia mipango ya kichungaji na kijamii.  Yote hayo kwa lengo la kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro katika jitihada zake uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu ni msaada mkubwa katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Nawaalika wasikilizaji na wasomaji na kwa upendeleo wanawake wote wakatoliki Tanzania kuona fahari ya kuwa sehemu ya utume hu una uinjilishaji kupitia mfuko wa baba Mtakatifu kwa majitoleo yao ya hali na mali.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2021 yananogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Uhusiano na mafungamano ya Kristo Yesu na wafuasi wake na binadamu katika ujumla wake, yamewawezesha kufunuliwa Injili na Fumbo la Umwilisho linalopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka kielelezo cha ushuhuda wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anagusia uzoefu wa Mitume wa Yesu wanaoshuhudia upendo, huruma na msamaha ulioneshwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Anaelezea matatizo na changamoto zilizojitokeza kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo katika mwanzo wa safari yao ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Leo hii, walimwengu wanakabiliwa na changamoto ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu aliyefufuka na kutukuzwa ndiye chemchemi ya matumaini ya waja wake. Katika mchakato wa uinjilishaji, Wakristo wanahamasishwa pia kulinda na kutunza mazingira. Kanisa lipo kwa ajili ya kuinjilisha, mwaliko kwa Wakristo kuwa ni vyombo vya uinjilishaji.  Utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ni kiini cha Kanisa, kwani Kanisa liko kwa ajili ya kuinjilisha. Kila mwamini anawajibika kuinjilisha kadiri ya uwezo, nafasi na dhamana yake katika maisha na utume wa Kanisa.

Wajibu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa! “Asanteni sana akina mama kwa moyo wenu wa huruma” (Rej. Njia ya Msalaba, kituo cha 8) Ninapenda kukushirikisha kuhusu: Wajibu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa dhamana ambayo inapata chimbuko katika Biblia Takatifu. Tutaangalia mifano ya wanawake waliofanya vizuri na waliofanya vibaya pia katika Agano la Kale na Agano Jipya pia na kujitahidi kupata fundisho kwa ajili ya maisha na utume wetu. Sehemu ya majadiliano haya imetoholewa katika andiko la Padre Samweli Muchunguzi na wengine: Sura ya kwanza Kazi ya Uumbaji wa mwanamke – “Hawa, mama yao wote walio hai” Rej. Mwanzo 1:27-28; 2:18, 20-25. Uumbaji wa Adamu na Hawa ulikuwa ni “mzuri sana” kwa sababu walikuwa na ushirika, upendo, ukamilifu, na utulivu kati yao na Mungu. Hawa aliumbwa kuwa mwenza wa Adamu. Wote wawili walipewa kazi sawa ya kuitunza bustani. Mungu aliwaumba katika sura yake na aliwataka wasaidiane (Mwanzo 1:27). Hawa, mwenza wake Adamu, alikuwa na uwezo sawa wa akili na mshiriki katika jamii na masuala yote ya uzazi. Walipendana, kuheshimiana, na kumheshimu Mungu. Hawa aliishi katika ulimwengu uliokamilika.  Rej. Mwanzo 3:1-20. Hawa alidanganywa na Shetani aliyemfanya awe na mashaka na mambo yale aliyoambiwa na Mungu. Aliamua na kukubali kuzungumza na Shetani, katika kumweleza yale Mungu aliyowaagiza, Shetani, Ibilisi alipata ujasiri wa kumshauri kuwa, Mungu hakuwatakia mema, bali aliwadanganya.

Mwanamke Hawa alisukumwa na mataminio (ya lile tunda) naye akafanya uamuzi (nje ya mapenzi ya Mungu) na kumwingiza mumewe katika dhambi yake. Akampa tunda, naye kwa hiari yake akala tunda walilokatazwa. Licha ya kumtii Mungu kutokana na upendo wake kwa Mungu, Hawa aliamua kuasi na kumshirikisha mumewe pia.Hali ya uasi ilileta madhara makubwa sana katika ulimwengu wao. Dhambi ya kutotii ilileta mabadiliko mabaya na makubwa kwao na kwa ulimwengu alioumba Mungu. Nyoka alilaaniwa, na ardhi ililaaniwa kwa kuzaa miiba na michongoma, chakula chao kitakuwa ni kwa uchungu na kwa jasho lao, mwanamke atazaa kwa uchungu mwingi na hakika watakufa. Mungu akawafukuza kutoka mazingira hayo mazuri ya bustani. Dhambi iliharibu mahusiano mazuri yaliyokuwapo kati yao na Mungu. Tangu hapo binadamu anahangaika na kutafuta namna ya kurudisha tena mahusiano na Mungu. Fundisho: Akina mama wa leo wanaitwa kuwa watiifu kwa Mungu na kufanya kazi ya Eva mpya. Wanaalikwa kuyazingatia yoye anayoagiza Mwenyezi Mungu katika Amri zake kumi. Wanaaswa kuzingatia yote anayoagiza Mungu kwa njia ya maelekezo ya Kanisa lake (Amri za Kanisa). Mwanamke awe mlinzi wa maadili safi na chombo cha kueneza huruma, msamaha na upendo wa Mungu. Kwa njia ya mwanamke, Baraka za Mungu ziwajie watu wake. Huu ndiyo utume wake kwa Kanisa la Mungu.

Sura ya Pili: Sara Ni Kielelezo cha Imani, Utii na Heshima. Rej. Mwanzo 12:1-5; 18:1-15; 21:1-13; Waebrania 11:11; 1 Petro 3:5-6. Imani na utii (Mwanzo 12:1-5). Sara alikuwa mke mzuri wa mwanamume tajiri Ibrahimu aliyeheshimika katika mji mkubwa. Kwa kuwa mumewe alikutana na Mungu aliye Hai na kumwamini, Sara alikubali kuondoka na kumsindikiza mumewe kwenda mahali wasikokujua, jinsi Mungu alivyowaagiza. Kwa kumtii Mungu, waliahidiwa kwamba kupitia uzao wao, taifa kubwa litaundwa, na kupitia kwao mataifa yote watabarikiwa. Sara alifuata uongozi wa kiroho wa mumewe na wa Mungu aliyesema naye, hivyo alitii kila aliloambiwa, aliondoka na mumewe kwenda katika mazingira mapya wasiyoyajua. Kuvumilia hali ngumu kwa heshima na imani (Mwanzo 12:10-20). Ibrahimu alifanya uamuzi mbaya wa kudanganya juu ya hadhi ya Sara kama mkewe na kumweka katika hali ya hatari. Hata hivyo, Mungu akawa msaada wake Sara na kuingilia hali hiyo. Mungu huwaheshimu na kuwabariki wanawake wanaoheshimu na kutii waume wao, bila kujali udhaifu au kushindwa kwao. Mungu hutumia uzoefu huo kuongeza imani na utii wetu kwake. Sara ni kielelezo cha imani. Biblia inasema kuwa, alijipamba kwa kumtumaini Mungu na kukubali mamlaka ya mumewe na kumtii bila hofu yoyote (1Petro 3:5-6).

Kutovumilia huleta shida (Mwanzo 16:1-6). Ahadi ya kupata mtoto ilipochelewa, Sara alifuata busara yake mwenyewe, akamshauri mumewe Ibrahimu kumwingilia mjakazi ili apate uzao kwake na hivyo kutimiza ahadi ya Mungu. Dhambi ya Sara ya kutoamini ahadi ya Mungu na kutovumilia ilileta huzuni, migongano na mashindano katika familia. Sara aliposhindwa kungojea mpango wa Mungu matokeo yake ni lawama, wivu, utengano na kudhalilishana kati ya wanawake hao wawili. Ingawa Ibrahimu aliwapenda Hajiri na kijana wake, lakini alikubali Sara akawafukuza, jambo ambalo lilileta mgogoro wa kudumu kati ya koo mbili za uzao wa Ibrahimu. Licha ya wateule wa Mungu kushindwa Mungu alishika Agano lake. (soma Mwanzo 18, 20 na 21). Mungu alitimiza ahadi zake kwa wakati wake, hata waliposhindwa na kuyumba katika imani yao. Ibrahimu na Sara wote wanatajwa katika Agano Jipya kama ni watu wa imani. Wamewekwa kuwa kielelezo kwa jinsi walivyotembea katika imani na kumtii Mungu (Waebrania 12:8-12; 1Petro 3:6). Fundisho: Tujifunze kutoka kwa Sara heshima, imani na utii. Pia tuone kuwa kukosa uvumilivu katika taabu na matatizo yetu husababisha migogoro na kutoelewana katika jamii na familia. Akina mama wanapotimiza wajibu wao katika Kanisa ni sharti wazingatie hizo fadhira njema kutoka kwa Sara na kuepuka mapungufu tuloyabaini kwa mama huyu.

Sura ya 3. Hana – Mwanamke wa Imani na Sala: Rej. 1 Samweli 1:9-28. Ndoa ya Hana yapata matatizo. Hana alikuwa ni mke wa kwanza wa mwanamume aliyempenda Mungu. Ingawaje Hana alikuwa mgumba, lakini mumewe alimpenda sana. Mke mwenza alikuwa na watoto, mara kwa mara alimsumbua kwa kumkumbusha hali yake ya ugumba. Alitowesha amani katika familia kutokana na vurugu. Mume alifanya mambo kuwa magumu zaidi kwa Hana kwa kuonyesha upendeleo, jambo ambalo liliongeza wivu na kutoelewana. Hana alilia mara kwa mara, hata akakataa kula, akiomba na kumlilia Mungu kuhusu hali yake. Kutokana na historia ya viongozi wakubwa kama Ibrahimu na Isaka, Hana alimjua Mungu kuwa ni wa miujiza. Alimjua kuwa ni msikivu, mwaminifu kwa watu wake, hivyo akaamua kumimina roho yake ya huzuni mbele za Mungu, akimwomba ampe mtoto wa kiume. Hana alizoea kuingia hekaluni kila mwaka kuabudu. Alipojiweka mbele ya Bwana akaanza kulia mbele ya watu kwa sababu ya uchungu wake. Aliamua kuchukua hatua ya ujasiri ya kuweka nadhiri iliyoonyesha ukweli wa imani ya moyo wake. Akamwitia Mungu kwa ujasiri, “Ee Bwana wa Majeshi” na pia kutambua unyonge wake na moyo wa utumishi. Aliahidi kumweka mtoto atakayepewa, wakfu kwa Bwana, siku zote za maisha yake. Baada ya maombi hayo, aliondoka katika hekalu akiwa na amani na kuamini kuwa Mungu amemsikia na atafanya. Ombi la Hana lapatiwa jibu na kwa shukrani kuu, anatimiza ahadi yake kwa Mungu. Alimleta mtoto hekaluni mbele ya Mungu na kumtoa amtumikie kwa muda wote wa uhai wake (1Samweli 1:26-28). Soma sala yake ya shukrani katika 1 Samweli 2:1-10. Fundisho: Akina Mama wanakumbushwa na kuelekezwa kuwa na imani thabiti na kuomba bila kuchoka. Wanawake baadhi siku hizi wanaonekana kutangatanga katika makanisa ya kisasa wakitafuta majibu ya matatizo yao. Wanaletewa sasa mfano mzuri wa Hana. Kumwomba Mungu na kutulia katika imani yao wakiwa na amani na kuamini kuwa Mungu amewasikia na atafanya. Hakika Mungu anatenda kwa muda wake. Atajalia kile wanachikihitaji muda muafaka.

Sura ya Nne: Mke wa Potifa: Mwanamke Mwenye Tabia Mbaya. Rej. Mwanzo 39:1-20. Mke wa Potifa alikuwa na kila kitu. Alikuwa na mume Afisa mkuu katika nchi ya Misri, walikaa katika nyumba kubwa iliyojaa samani nyingi nzuri zenye gharama kubwa na kuvaa nguo nzuri za thamani. Pamoja na hivyo vyote alikuwa na utupu ndani yake, ili kuujaza utupu huo, alijaribu sana na hata kumbembeleza Yusufu, mtumishi wa mume wake, ili alale naye. Alijaribu hata kumbaka ili atosheleze mwili wake. Lakini heshima ya Yusufu kwa Mungu na kwa bwana wake ilimzuia. Mwanamke huyo aliposhindwa kumpata Yusufu, alitafuta njia mbadala ya kumsingizia na kumtuhumu Yusufu mbele ya Potifa, ndipo Yusufu akafungwa. Dhambi ya kwanza ya uchu wa mali ilimpeleka kwa dhambi zingine za uongo, usingiziaji na usaliti. Mafarisayo walimlaumu Yesu jinsi alivyokutana na mwanamke wa tabia mbaya kwa sababu alimkubalia mwanamke huyo kumgusa Luka 7:36-50. Lakini Yesu alitambua hitaji lake la kweli la kukubalika na kusamehewa. Yesu alimkubali, akamsamehe dhambi zote kwa sababu ya upendo wake mkuu. Wakati mwingine Yesu aliletewa mwanamke katika fumanizi la uzinzi Yohane 8:3-11. Yesu aliwajibu washtaki wa mwanamke huyo, maneno yaliyowaonyesha dhambi zao wenyewe, wakaondoka. Yesu hakumhukumu yule mwamamke, alimwagiza kwenda na kutotenda dhambi tena.

Fundisho: Yesu alifundisha kuhusu uzinzi na talaka (Mathayo 5: 27). Alieleza kwamba, hata kumtazama mtu kwa tamaa, ni sawa kama umezini. Sisi kama viungo vya mwili wa Kristo na hekalu la Roho Mtakitifu tusitoe miili yetu katika matendo ya uasherati na hivyo kuchafua mwili wa Kristo na roho zetu. Bali tutoe miili yetu kwa utukufu wa Mungu (1 Wakorintho 6:13b-20). Miili yetu ni hekalu la Mungu aliye Hai, hivyo haipaswi kuchafuliwa na mahusiano yasiyomjua Mungu (2 Wakorintho 6:14). Wanandoa wasipojitoa kikamilifu katika ndoa yao, uchu wa ngono utaleta tamaa mbaya na kuishia kuangamizana (Mithali 6:32). Ngono inapofanyika katika udanganyifu na katika hali isiyo halali husababisha hatia, lawama, chuki, aibu, tena kuongeza upweke na matatizo mengi ya kujirudia katika ndoa (Mithali 5:3-6; 23:27-28; 6:27-29). Wote wanoshiriki katika matendo ya mwili yakiwamo uzinzi na uasherati hawataurithi ufalme wa Mungu (Wagalatia 5:19-21). Sisi Wakristo tunaamriwa kujitakasa na kuepukana na uchafu wowote wa miili na roho zetu, tuwe wacha Mungu na watakatifu (2 Wakorintho 7:1). Basi wanawake kuweni makini katika utume wenu kwa Kanisa la Mungu kuwaombea watumishi wenu Maaskofu, Mapadre na Mashemasi ili wasichafuliwe na kunaswa na mitego ya adui katika utume wao. Nanyi, kila mmoja ajihadhari asije kuhusika katika kuwakwaza kama alivyofanya mke wa Potifa!

Sura ya Tano Abigaili - Mke wa Mpagani na Mpatanishi wa Amani. Rej. 1 Samweli 25:2-31. Abigaili alikuwa mzuri tena mjanja. Nabali, mumewe alikuwa tajiri, lakini mkorofi na mpumbavu. Daudi alikuwa ametawazwa kuwa mfalme wa Israeli, lakini alimkimbilia Sauli na kutangatanga na watu wake nyikani. Walitoa ulinzi kwa watumishi wa Nabali waliokuwa wakikata manyoya ya kondoo. Daudi alitoa maagizo kwa watu wake, kumwendea Nabali kwa amani, kuomba chakula kwa sherehe yao. Nabali aliwajibu vibaya sana tena kwa kejeli na hata kumkashifu Daudi. Daudi alipoambiwa yaliyotokea, alikasirika na kujitayarisha kwenda kumwangamiza Nabali na familia yake. Mmoja wa vijana alitambua mabaya ambayo yangetokea, akaenda kumwarifu Abigaili yote yaliyofanywa na mumewe. Abigaili akatayarisha sadaka ya amani na kuondoka mara moja kumwendea Daudi. Akamkabili Daudi na kukiri hatia na upumbavu wa mumewe alioufanya na kuomba msamaha. Alimshauri pia, kufikiria hasara atakayopata ya kulipiza kisasi kwa kumwaga damu kwa mikono yake, bali baraka za amani atakazopata kwa kutofanya hivyo. Pia alimkumbusha wito na utume wake kwa Bwana. Busara yake ilimsaidia Daudi kutuliza hasira na kuacha kuua.

Tabia ya Abigaili na jinsi alivyonena ilileta mabadiliko ya haraka katika utata uliokuwepo. Inategemea ni kwa namna gani wanawake hutumia ndimi zao kwani huweza kuleta au kuzuia mtikisiko. Zaburi inatoa ushauri wa kuzuia ndimi kwa mabaya ili kuleta amani kuliko ugomvi (Zaburi 34:13-14). Pia, kujua nyakati za kusema na kujizuia (Mhubiri 4:7 na Zaburi 39:1-3). Maneno mazuri ni kama fedha inayokubalika na huleta uponyaji mioyoni (Mithali 10:20), na maneno mabaya ni kama upanga mkali uchomao moyo au mshale wa sumu uuao (Mithali 12:18). Mtume Yakobo anazumgumzia matatizo ya kutozuia na kutotawala ulimi (Yakobo 1:26; 3:5-12; 4:11). Ulimi huo huo hulaani, hubariki, husingizia, hutukana na hutoa maneno maovu kwa ndugu, ulimi pia hukemea kwa ukali (1 Timotheo 5:1). Mambo hayo hayatakiwi katika kanisa la Kristo. Fundisho: Kuishi kwa amani na mwenza asiyeamini ni changamoto katika ndoa. Hata hivyo, Rej. 1 Wakorintho 7:10-16 inashauri kuwa, mwenza aliyeamini anaweza kumsaidia mwenzake na watoto kuokoka kutokana na matendo na imani wanayoona kwake. Katika 1 Petro 3:1 inaelezea kuwa njia ya kumvuta mwenza ni mwenendo kuwa msafi na uchaji wa Mungu, tena haya huzungumza zaidi kuliko maneno. Maandiko Matakatifu yanakataza kutengana au talaka kutokana na imani tofauti. “Maana Mungu ametuita katika amani” (1 Wakorintho 7:12-15). Yesu alifundisha juu ya talaka (Mathayo 5:31-32). Ingawaje talaka ilikubalika katika sheria ya Musa (Kumbukumbu 24:1-4), lakini mtazamo mwema wa Yesu unakumbusha kuwa, talaka siyo suluhisho sahihi, bali pale tu uzinzi unapofanyika (yaani pale ambapo hakuna ndoa bali wawili hao wanaishi katika uzinzi). Yesu anakataa suala la talaka kwa sababu huwapeleka wahusika kutenda dhambi (Marko 10:11-12; Luka 16:18). Ninyi mnaoishi na wanaume wasioamini mna utume wa kuwaongoa kwa matendo yenu na mwenendo mwema. Huo ndiyo utume wa akina Mama katika Kanisa la Mungu. Chukueni mfano wa Abigaili ili mjitahidi kuwa watu wa kupatanisha kwa amani na maneno na matendo yenu yawavute wengi kwa Mungu.

Sura ya  Sita: Ukarimu, Matendo Mema: Kiroho na Kimwili na Uchaji wa Mungu: Mwanamke Mshunami (2 Wafalme 4:8-22, 32-37) alikuwa tajiri na mkarimu kwa Elisha, ila alikuwa hajazaa. Huyo alimtaka ale nao chakula kila mara alipopita. Alimtambua kuwa ni Mtakatifu wa Mungu, hivyo akamshauri mumewe wamtengee chumba cha kupumzikia kila alipopita. Alitafuta njia ya kutumia mali yake kwa hudumu ya Mungu, kwa mali yake alimhudumia mtu wa Mungu. Elisha alipotaka kumbariki kwa ukarimu wake, yeye alimwomba ambariki kwa mtoto. Tunawashukuru sana akinamama mnaotumia mali zenu kulitegemeza kanisa la Mungu. Mali ni pamoja na nguvu zenu, muda wenu, pesa yenu, jasho lenu, sala zenu, ushauri, n.k. Mungu hatakosa kuwabariki sana kwa wakati wake, hasa kuwajalia kile mnachokihitaji katika maisha yenu. Martha wa Bethania (Luka 10:38-42) alikuwa na mazoea ya kumkarimu Yesu na wanafunzi wake, maana ni marafiki wa familia. Ilikuwa ni hesima wapewe mahali pa kupumzika kila walipokuja. Baadaye Martha aliingia katika hali ya mahangaiko kutokana na shughuli nyingi za kukaribisha wageni na hata akakosa muda wa kuzungumza nao. Hivyo Martha, alimlaumu na kumhukumu Mariamu kwa kutojali kumsaidia kazi, bali kukaa na kuzungumza tu. Yesu alimshauri Martha kuhusu umuhimu wa kujenga roho yake na kutowahukumu wengine. Akina mama wapendwa, ninyi ni wakarimu sana.

Tumieni kipawa chenu hicho kujijenga kiroho zaidi na kila mmoja kutimiza wajibu wake pasipo kulaumiana na kuhukumiana. Tumieni fursa zinazopatikana kushauriana na kuelekezana kwa upendo na busara. Dorkasi alikuwa ni mwanafunzi mtenda mema (Matendo 9:36-42) na alijitoa kuwasaidia maskini kwa dhati. Alikuwa na kipaji cha kuwabariki wengine, hasa wajane. Wajane labda walikuwa wengi katika mji wa Yafa, uliokuwa kando ya pwani, kwa sababu ya vifo vya ajali za waume wao waliokuwa wanamaji na wavuvi. Huenda naye alikuwa ni mjane, lakini alitumia uwezo wake kuwatia moyo na kuwasaidia wengine, kimwili na hata kihisia na kiroho. Kutokana na upendo wake mkuu wa kujitoa, alipendwa sana. Fundisho: Mwanamke mchaji wa Mungu lazima apambwe na matendo mema na uzuri wa ndani, roho ya upole na utulivu (1 Timotheo 2:9-10; 1 Petro 3:4-5). Mapambo ya nje tu hayaonyeshi uzuri wa mtu, bali ni ule wa ndani ujengwao katika utu wa kweli. Wanawake watakatifu wa Agano la Kale walijipamba kwa kutii wanaume wao (1 Petro 3:5; 1 Timotheo 2:15). Wanawake wahimizwa kudumu katika imani, upendo, utakatifu na unyoofu. Mwonekano wa mtu alivyo kwa nje huonesha tabia yake alivyo, na huashiria mara nyingi kilichomo ndani yake. Ni muhimu kuvaa mavazi ya heshima kwa mwili wetu na kumheshimu Yesu aliye ndani yetu. Tuwe na sifa za ustahimivu, kiasi, uaminifu, maneno ya neema na heshima (1 Timotheo 3:11, 4:7; Tito 2:3; 1 Petro 3:2).

Sura ya 7: Mjane wa Sarepta - Mateso na Ukarimu. Rej. 1 Wafalme 17:7-24. Mwanamke huyu alipita katika wakati mgumu. Alikuwa amefiwa na mumewe, halafu ukame ulisababisha ukosefu wa chakula na maji, alikuwa na akiba ya chakula ya siku moja tu. Its not wajane wa leo where tunalia wakati funguo a gari iko kiunoni na kadi ya bank kwa bra. Alipoende kutafuta kuni alikutana na mtu asiyemfahamu, lakini alimtambua ni mcha Mungu kwa mavazi aliyovaa. Alikuwa ni Eliya ambaye pia alikuwa na njaa. Aliyetumwa na Mungu kwa huyo mjane ili kujipatia mahitaji yake. Eliya alimwomba amletee maji ya kunywa na kipande cha mkate. Mjane alipoelezea hali yake, Eliya alimwagiza, “Usiogope, nenda ufanye kama ulivyosema, lakini unifanyie mimi kwanza na kuniletea, kisha ujifanyie wewe na mwanao. Kwa kuwa Bwana Mungu wa Israeli, anaahidi pipa la unga halitapunguka wala chupa ya mafuta haitaisha hadi hapo mvua itakaponyesha”. Mwanamke huyu alikuwa ni mpagani, hakuwa Mwisraeli, huenda aliwahi kusikia habari za Mungu wa Israeli. Hali ngumu aliyokuwa nayo na ahadi alizoambiwa na nabii zilimfanya akubali kufanya aliyoombwa. Hatua ya imani ya kwanza ni ile ya kukubali kuamini alilosema nabii. Ndipo alipotii na kumfanyia kwanza nabii chakula, na alipata mfululizo wa miujiza ya ongezeko la unga na mafuta! Biblia inatuambia chakula kiliongezeka na kuwatosheleza watu wote wa kwake na nabii Eliya kwa siku nyingi (1 Wafalme 17:15-16). Hatua yake ya imani kwa Mungu ilikuwa ni msingi wa maisha yake na vile vile kumweka hai mtumishi wa Mungu.

Hata hivyo siku moja alipatwa na maafa tena. Mtoto wake aliugua ghafla na kufa. Alikuwa na maswali ya kujiuliza: Je, ni jaribu la kutomwamini Mungu na upendo wake? Kwa nini Mungu amwokoe kutoka kifo cha njaa na afe kwa ugonjwa? Je, arudie maisha yake ya nyuma ya upagani? Je, amemkasirisha Mungu? Katika uzuni yake alifikia hatua ya kumtuhumu mtumishi wa Mungu kuhusika na kifo cha mwanaye. Eliya alileta hali ile mbele ya Mungu na kumwomba arudishe uhai wa yule mwana. Ombi lilijibiwa, mtoto alifufuliwa akawa hai. Suala la kufufuliwa mtoto wake, lilileta msukumo mpya wa imani na upendo wake kwa Mungu. Aidha, jaribu hili lilimjengea uaminifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Fundisho: Mateso ya mama huyu ni mateso yanayookoa. Wapendwa akina mama, kila jaribu unalopitia ni fursa ya kukupeleka karibu zaidi na Mungu ukilipokea kwa imani na uvumilivu. Yaunganishe mateso yako na ya Yesu Kristo na utapata faraja kuu. Ukianza kutafuta mchawi anayesababisha shida zako, utapotea na kujidhoofisha sana.

Sura ya Nane: Mariamu wa Bethania, Mwanamke Aliyependa Sana. Rej. Luka 10:38-42. Mariamu alichagua kufanya jambo lisilo la kawaida la kukaa miguuni pake Yesu akisikiliza maneno yake, badala ya kushugulika na ukarimu kama alivyofanya dada yake Martha. Na Martha alipomnung’unikia Mariamu kwamba hakutekeleza wajibu wake, Yesu alithibitisha uchaguzi wake Mariamu kwamba amechagua yaliyo bora, na kumwonya Martha kwa jinsi alivyomhukumu dada yake. Katika Yohane 11:17-37, Mariamu anaomboleza kifo cha ndugu yake na kusikitika kwa nini Yesu alikawia kuja, wakati aliarifiwa ugonjwa wake. Alikuwa na imani juu ya uwezo wa Jesu kuponya rafiki yake mpendwa, kwa nini hakuzuia kifo chake? Ingawa hakuelewa kutokana na kuumizwa na tukio hili, upendo na imani yake kwa Yesu haikuyumba. Upendo mkuu wa Yesu kwa familia ya Mariamu ni dhahiri kwa jinsi alivyoomboleza nao. Lakini dhumuni la Mungu (kuimarisha imani yao) lilikamilika vizuri zaidi kupitia kifo cha Lazaro na kufufuliwa kwake kutoka wafu.

Wapendwa kwa macho ya kibinadamu tunapomwita Yesu twaweza kudhani anachelewa, lakini Yesu anatenda kwa wakati wake. Tusubiri tu akifika tumwonyeshe “KABURI” letu, na tusubiri maelekezo yake. Akikwambia ondoa jiwe – fanya hivyo. Hata tukiona Yesu kachelewa siku nne bado Yeye amewahi – huo ndio muda wake wa kufanya muujiza. Upendo mkuu wa Mariamu unaoneshwa zaidi pale Yesu alipowatembelea tena nyumbani kwao (Yohana 12:1-8). Alipata nafasi tena ya kuonyesha upendo wake bila kujali atakavyoeleweka kwa matendo yake. Mariamu alichukua marashi yake ya gharama akampaka Yesu miguuni na kufuta kwa nywele zake. Matendo hayo ya kumwabudu Yesu, yalithibitisha imani yake kwa Yesu kuwa ni Masihi, na kumshukuru Yesu kwa mabadiliko aliyomfanyia katika maisha yake. Alikumbuka jinsi Yesu alivyozungumzia juu ya mateso yake yatakavyokuwa, akajua muda umefika. Kutokana na upendo mkuu aliokuwa nao kwake, aliupaka mwili wake Yesu mafuta kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wake kwa Kristo Yesu. Fundisho:Wapendwa akina mama, mwenyezi Mungu amewajalia mapaji mengi, karama nyingi kama vile zile sifa kumi na tano tulizoona katika utangulizi. Zitumie hizo kumtumikia Mungu. Tumia mali zenu na karama zenu kwa ajili ya maondoleo ya dhambi zenu.

Sura ya 9: Mariamu, Mama wa Yesu, Usafi wa Maisha, Unyenyekevu na Utayari wa Kupokea Mapenzi ya Mungu, uvumilivu na Imani kuu Rej. Luka 1:26-38; 2:6-14, 17-19; Mathayo 1:18-25) Tutakumbuka kuwa Picha ya Harusi ya Kana imechanguliwa kuwakilisha mwanga wa furaha ya upendo ndani ya familia. Mariamu alikuwa ni msichana wa kawaida, bikira, mtulivu, mnyenyekevu na asiyejulikana, aliyeishi Nazareti. Pamoja na hayo, alitokewa na malaika Gabrieli, na kumwambia amejaliwa, na “Bwana yu pamoja nawe.” Mariamu alishangaa na kufadhaika kwa salamu hiyo. Kwa uhakika Mariamu alithamini mahusiano yake na Mungu. Kila mwanamke Myahudi alitamani kumzaa Masihi aliyeahidwa. Mariamu ni binti mcha Mungu aliyejua maandiko matakatifu na aliyetegemea kuona ukombozi wa Israeli. Zaidi ya yote alikuwa na moyo wa utashi wa kutumiwa na Mungu. Alipoambiwa na malaika kwamba alichaguliwa kumzaa Mwokozi wa ulimwengu, aliuliza itakuwaje hali yeye ni bikira. Aliamini neno la Mungu, akajitoa kikamilifu kwa mapenzi yake bila kusita. Je, Mariamu alifikiria yale ambayo yangempata katika kujitoa katika mapenzi ya Mungu? Utaratibu wa Kiyahudi uliruhusu mwanamke akipatwa na mimba kabla hajaolewa kuuawa kwa kupigwa mawe. Lakini ukubali wa Mariamu wa heshima pekee wa kuwa mama wa Masihi umeandikwa katika Luka 1:46-55. Wimbo wake unamtukuza Mungu, umejaa sifa na shukrani za kuchaguliwa kuleta ukombozi kwa watu wa Mungu. Mariamu, Mama wa Yesu angeweza kushangazwa na kuogopa matukio yote yaliyohusu kuzaliwa kwake Yesu. Badala yake alikubali na kukumbuka ahadi zilizotolewa huko nyuma kumhusu na akaamini Mungu kuzitimiza (Luka 2:19).

Alipatwa na changamoto katika malezi, lakini alizikabili na kumlea Yesu. Akakua, akawa mwenye nguvu, hekima na kufunikwa na neema ya Mungu (Luka 2:40). Mariamu alielewa uwezo wa Yesu ulivyo mkuu, na alifanya bidii kuwashawishi na kuwasaidia watu kumwelewa Yesu jinsi alivyo (Yohane 2:1-11). Imani yake na kujitoa katika mapenzi ya Mungu ilimjenga na kumwezesha kuvumilia mambo magumu aliyopitia wakati wa maisha ya Yesu. Yesu alipotamka kwamba jamaa yake wa kidunia hawapewi umuhimu wa kwanza, mama yake hakujali aliendelea kumtia moyo katika huduma yake (Mathayo 12:46). Mwishowe, Mariamu alisimama karibu na msalaba akishuhudia matusi, dhihaka, mateso na kufa kama mhalifu. Hata baada ya kifo, Mariamu ametajwa pamoja na wanafunzi wa Yesu wakisali chumbani (Matendo 1:14). Wakati wa kifo cha mwanaye, Mariamu hakudumu katika maombolezo bali aliendelea kufuatana na wengine katika huduma ya Mungu. Fundisho: Bikira Maria ni kioo cha uinjilishaji mpya na mfano bora wa kuigwa na wanawake wote. Sifa zake ni hazina kwa wote wamwaminio Yesu Kristo. Akina mama igeni kwa kwake fadhira za imani kuu, unyenyekevu, uvumilivu, malezi bora ya watoto, ushirikiano katika familia, kujitoa kwa ajili yaw engine bila kujali sana hasara zinazoweza kutupata kama ulimwengu huu upitao bali uzima na wokovu wa watu mnaowahudumia. Jifunzeni kwa Mama Maria tabia ya kusali pamoja kama jumuiya au familia na hasa kushiriki Misa Takatifu katika jumuiya na siku zilizoamriwa kama Jumapili na sikukuu nyingine.

Sura ya Kumi: Nyumba ya Kikristo Inarithisha Imani (fadhila za kimungu- Imani matumaini na Mapendo. Rej. 2 Timotheo 1:5; Waefeso 5:21-6:4. Kazi muhimu sana waliyo nayo mabibi na mama ni kuweka hali ya mazingira ya nyumbani, iwe mahali watoto wanapojifunza kumpenda Mungu na wenzao. Paulo alitambua kuwa imani ya Timotheo ilianza na kulelewa na wale alioishi nao, bibi yake Loisi na mama yake Eunike (2 Timotheo 2:5). Mazingira ya nyumbani ni mwalimu wake wa kwanza wa kujenga au kuharibu mtoto kitabia. Akina Mama wanao umuhimu mkubwa sana katika miaka ya kwanza ya mtoto, kuzaliwa hadi miaka saba, kwa sababu Mama hukaa na mtoto kwa muda mwingi. Katika umri huu, mtoto hujifunza mambo kwa haraka sana. Huiga kutoka kwa mama na wale walio karibu naye. Mama wanapowafundisha wototo simulizi za mashujaa wa imani, au kuwasomea katika Biblia, hupenda sana kusikia simulizi hizi na hunasa katika ubongo, hawasahau. Watoto wenye asili ya mafunzo hayo, hujenga tabia njema, kutokana na yale wanayoambiwa, kusikia na kushuhudia wazazi na wenzake na watu wengine, na watakuwa na misingi imara katika imani. Mama zangu wapendwa, tuangalia sana vitu tunavyowapa watoto wetu, mazingira ya malezi yao, na zaidi sana tuwape muda wetu, n.k.

Waraka wa Paulo kwa Waefeso 5:21-6:4 unatoa baadhi ya miongozo katika nyumba ya Kikristo. Familia nyumba iwe mfano wa uhusiano wa upendo wa Yesu kwa kanisa, kama bibi harusi wake. Unyenyekevu wa Kristo alivyotii mapenzi ya Mungu ni kielelezo cha mahusiano yetu ya mume na mke. Wanawake watii na kuheshimu wanaume wao kama wafanyavyo kwa Kristo aliye kichwa cha kanisa. Wanaume wawapende wake zao na kuwaheshimu kama miili yao wenyewe, wawajali, wawatunze bila ubinafsi. Mahusiano ya ndoa yawe mfano wa upendo wa Kristo kwa kanisa bila kujali maisha yake, na yawe mfano wa kanisa linavyonyenyekea kwa hiari na kuongozwa na Kristo kutokana na upend huo. Pia, Paulo anafundisha kwamba, uhusiano wa mume na mke ulivyo juu sana ya mahusiano mengine yoyote yale, kwa maana wao wameunganishwa kuwa mwili mmoja na kujitoa kikamilifu kwa mwenza na watoto wao. Watoto waagizwa kuwatii wazazi wao katika Bwana (Waefeso 6:1-4), wakiwaheshimu kama ilivyoagizwa ili wabarikiwe katika maisha marefu ya kuishi (Kutoka 20:12). Hali bora ya maisha ya watoto hutegemea uhusiano wa upendo wa wazazi wao. Kutii kwa upendo ni matokeo ya ushuhuda wa amani na upendo walioonyesha wazazi wao. Inafuata maelekezo ya utulivu na maadili bila kutumia lugha kali, vipigo, na ulazima wa matakwa yao. Mafundisho ya wazazi yawe “kilemba cha neema kichwani” na “mikufu” shingoni mwake (Mithali 1:8-9).

Sura ya 11: Maria Magdalena (anaitwa mtume kwa kuwa alikuwa wa kwanza kutangaza Habari za Kristo mfufuko kwa mitume – ametangazwa na Papa Francisko: Toba, Imani na ushuhuda wa Ufufuko; Pia wanawake walioandamana na Yesu: Maria Magdalena, Yoana mke wa Kuza, Susana na wengine kadhaa (Soma: Lk 7:36-8:3; 23: 27- 31, 49, 55; 24: 1- 12) – walitumia rasilimali fedha na muda kwa ajili ya kumhudumia Kristo Yesu pamoja na Mitume wake! AINA ZA UTUME: Utume wa Toba, ni utume wa machozi. Machozi ni tiba; machozi yana nguvu; machozi huvuta huruma. Akina mama wapendwa, tumieni machozi yenu kuliombea kanisa la Mungu. Tumia machozi yenu kulipia dhambi zenu na za ulimwengu. Machozi yenu yaivute huruma kwa wengine wanaowakosea. Kuna Utume wa Ufuasi – kuandamana na Yesu. Ninyi akina mama mnakumbushwa kuandamana na Yesu na kanisa lake katika kuinjilisha ulimwengu. Andamaneni kuelekea kanisani kusali; andamaneni kuelekea hospilini kuwaona na kuwafariji wagonjwa. Andamaneni kuelekea msibani kuwafariji wafiwa na kuwaombea wafu. Andamaneni kuelekea kwa wahitaji na maskini na kuwahudumia. Andamaneni kuelekea seminarini kuwafadhili waseminaristi na walezi wao. Tuandamane na Yesu kuelekea Kalvari, tukiguswa na mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu wanaotuzunguka. Kuna utume wa ushuhuda kushuhudia ufufuko wa Yesu. Zawadi ya kuushuhudia mwili wa utukufu wa Yesu alipewa Mwanamke kwanza. Tumieni karama yenu ya kusimulia kueneza habari njema ya Neno la Mungu badala ya chuki na masengenyo. Eneza msamaha badala ya kulipiza kisasi kwa sababu hatuna vigezo vya haki. Eneza mwanga wa furaha ya Injili ya uhai, ndoa na familia badala ya kiza la dhambi na mauti!

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Septemba 2016 alimtangaza Mama Theresa wa Calcutta kuwa Mtakatifu, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Huruma ya Mungu kwa wafanyakazi wa huruma na wale wa kujitolea. Katika mahubiri yake, alikazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu. Waamini wawe ni mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Huruma iwe ni kielelezo cha sala na imani tendaji inayomwilishwa katika huduma na unyenyekevu. Waamini wanapaswa kuwa na ujasiri na kuthubutu kumwona na kumtambua Kristo Yesu kati ya watu wadogo, wanyonge na maskini. Wote hawa waoneshwe Injili ya matumaini, huruma na upendo. Mama Theresa wa Calcutta alisimama kidete kutangaza na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Aliinama na kuwaganga maskini kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Akasimama kidete kulinda: utu, heshima na haki zao msingi. Alikuwa ni sauti ya maskini na wanyonge duniani, kielelezo makini cha uwepo endelevu na angavu wa Mungu kati ya maskini. Mama Theresa wa Calcutta awe ni kielelezo cha upendo aminifu wa Mungu usiokuwa na ndoana.

Hitimisho: Utume wa Mtakatifu Veronika, shujaa aliyethubutu kupangusa uso wa Yesu unaonesha ushupavu wa wanawake kama chanzo cha faraja (Rej. Njia ya Msalaba kituo cha Sita) – Matendo ya huruma kiroho na kimwili. Akina mama mnao utume wa kupangusa uso wa Yesu anapoteseka. Uso wa Yesu ni Kanisa lake. Uso wa Yesu ni Watumishi wake. Uso wa Yesu ni maskini, wagonjwa, yatima, wajane, wagane na wanyonge pamoja na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kanisa la Yesu linateswa na wazushi. Wanawarubuni watu kwa mafundisho potofu na ahadi bandia za mafanikio ya mali, utajiri na uponywaji. Akina mama mnaalikwa kufanya kazi ya Veronika ya kulipangusa Kanisa uso kwa kuwa imara ninyi katika imani, matumaini na mapendo na kamwe msikubali kuyumbishwa. Jitahidini kusimamia imani na mwenendo wa watoto wenu, kwa kuliombea Kanisa nasi viongozi wenu, kwa kujiombea ninyi wenyewe ili Shetani, Ibilisi “ashindwe na kulegea.” Mnaweza kuupangusa uso wa Yesu vizuri zaidi mkiungana katika pendo na kweli. Mkawa na sauti moja. Wanawake waliomlilia Yesu walikuwa wengi. Walilia akawasikia, akawaelekeza cha kufanya. Tuienzi WAWATA ili chozi letu liwe na nguvu tunapomlilia Mungu tukimpelekea maombi yetu, toba zetu na shukrani zetu. “Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi. Upendo wangu uwe kwenu katika kuungana na Kristo Yesu!” (1Kor 16: 23 – 24.) Kwa hakika, wanawake ni majembe ya nguvu katika maisha na utume wa Kanisa!

21 October 2021, 15:34