Tafuta

Huruma ya Kristo Yesu kwa wagonjwa ni ishara inayong'aa kwamba, Mwenyezi Mungu amewajia watu wake na kwamba, Ufalme wa Mungu umekaribia! Huruma ya Kristo Yesu kwa wagonjwa ni ishara inayong'aa kwamba, Mwenyezi Mungu amewajia watu wake na kwamba, Ufalme wa Mungu umekaribia! 

Tafakari Jumapili 23 ya Mwaka B: Kristo Mganga: Huruma ya Mungu!

Mwinjili Marko leo anatuonesha kuwa kiziwi na mwenye utasi ni yule ambaye bado hajapata fursa ya kukutana na Kristo Yesu na kuisikia Injili yake, lakini pia kila mmoja anayefunga kwa makusudi masikio yake na hivyo kutoruhusu Injili ya Kristo ipenye na kuingia katika masikio ya moyo wake. Kwa muujiza huu, Yesu leo anatangaza mwanzo mpya kati ya mbingu na dunia.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Isaya wa pili kama wanavyokiita wanazuoni wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu, ni sehemu ya Kitabu kikubwa cha Nabii Isaya ambapo mwandishi anajaribu kuwarejeshea matumaini taifa lile la Israeli wakiwa bado utumwani Babeli. Na ndio tunasoma katika somo la kwanza la Dominika ya leo ujumbe wenye matumaini, ujumbe wa faraja na kuwarudishia watu wale furaha na amani tena. Mwandishi anajaribu kuonesha pande mbili tofauti ambazo kwa hakika zitarejeshewa tena matumaini na faraja na furaha. Mwandishi anatuonesha kuwa furaha na matumaini hayatarudi kwa Wanawaisraeli tu bali hata katika nguvu asili za uumbaji, “maana nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji.” Upande wa pili mwandishi anaonesha pia si tu watarejea katika nchi yao, yaani kupata tena ukombozi kutoka utumwani Babeli bali hata wenye magonjwa pia watapokea uponyaji; “Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema atarukaruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba.”

Ukombozi kadiri ya Isaya wa pili ni karibu sawa na ufufuko, ni uumbaji mpya iwe kwa nchi yao bali hata na watu wake. Ni kujaliwa hali mpya inayokuwa bora zaidi, kwani utumwani ni sawa na kuwa mtu mfu, ni kukosa uzima, kukosa matumaini, kukosa furaha na amani ya kweli. Kutoka utumwani ni sawa na kufufuka kutoka kaburini, kutoka katika hali iliyokuwa duni na mateso makubwa na dhiki. Kukombolewa kunafananishwa na safari ya kurejea tena katika bustani ile ya Paradiso, mahali penye uzima tena sio tu kwa mwanadamu bali hata na mazingira yake yanayomzunguka, ni mahali penye amani na usalama kwani mwanadamu anarejea katika mahusiano ya ndani na muumba wake na viumbe vingine pia. Na ndio tunaona unabii ule wa Isaya wa pili unatimia leo katika somo la Injili. Tunaposoma sehemu ya Injili ya leo juu ya uponywaji wa huyu aliyekuwa kiziwi na mwenye utasi, tunabaki na maswali kadhaa na hasa jinsi au namna ya Yesu anavyomponya; Yesu leo hatumii tu neno lake bali pia kuna ishara nyingine ambatanishi ambazo kwa kweli zinatushangaza na kutuacha na maswali juu ya umaana na uhalali wake.

Yesu hamponyi leo mbele ya watu bali anamtenga na kufanya uponyaji faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua na mwishoni ndipo akamwambia “Efatha”, neno la Kiaramayo lenye maana ya “funguka”. Kwa kweli tunashawishika kuona anatumia namna au njia zile wanazotumia waganga wengi wa kienyeji au watenda miujiza hata katika mila na mazingira yetu ya Kiafrika, kwani wao mara nyingi wanatumia njia ambazo inakuwa karibu ngumu kuelewa maana yake. Marko mwinjili anatuonesha kuwa kitendo hiki Yesu anakifanya akiwa katika mipaka ya Dekapoli, ndio huko pia Yesu anamponya mtu aliyekuwa na mapepo na kuruhusu mapepo yale kuwaingia nguruwe. (Marko 5:1) Ndio kusema Yesu anafanya muujiza huu akiwa katika nchi ya Kipagani, katika nchi ambapo Yesu anatumia ishara zile zile ambazo zilizoeleka na kueleweka na watu wale, lakini kama tutakavyoona leo anazipa maana mpya, maana inayokuwa sio tena kama ile ya waganga wa kienyeji na watenda mazingaombwe bali ile ya Kitaalimungu, ila ya Kimungu.

Mgonjwa anayeponywa leo ni kiziwi na mwenye utasi, ndio kusema alikuwa kiziwi na pili nusu bubu, mtu aliyekuwa na shida sio tu ya kusikia bali hata kutamka vizuri na kwa usahihi maneno, ni mmoja aliyekuwa anaongea kwa shida na tabu kubwa. Na si tu aliongea kwa shida bali pia ilikuwa ni ngumu kumuelewa anapozungumza au anapoongea na ndio neno linalotumika la Kigiriki ni “moghilàlos”. Neno hili linasikika katika somo la Injili ya leo na pia katika sehemu ya Isaya wa pili kama tulivyotangulia kuona katika tafakari yetu ya leo hapo juu. Na ndio tunaona Mwinjili Marko analitumia tena hapa kuonesha kuwa unabii ule wa Isaya unapata utimilifu wake kwa njia ya Yesu Kristo. Kwa Nabii Isaya, bubu na kiziwi lilikuwa ni taifa lile la Israeli, taifa lililo muasi na kuwa mbali na Mungu wao, lakini katika Injili ya leo, bubu na kiziwi si tu mtu yule mpagani anayeletwa mbele ya Yesu ili amponye, bali ni kila mmoja wetu anayekuwa hajakutana bado na Kristo Yesu. Kila mmoja anayeshindwa kulisikia na kulishika Neno lake na kuwa shuhuda kwa maneno na matendo yake, huyu ni sawa na bubu-kiziwi.

Kiziwi ni mmoja mwenye ulemavu wa masikio na hivyo kushindwa kusikia ujumbe unaowasilishwa kwake, na matokeo yake naye kushindwa kuuwakilisha ujumbe kwa wengine. Ni mmoja anayebaki na kuishi kama kisiwa, kwa tabu na mateso na shida kubwa, ni karibu ni mmoja anayeishi katika ulimwengu uliofungwa, ni karibu sawa na kuishi utumwani, kwenye kifungo cha kushindwa kuwasiliana, kwani mwanadamu kwa asili ni mwana mawasiliano na mwana mahusiano. Tumeumba na ndivyo asili yetu ilivyo kuhusiana kwa kuwasiliana, hivyo anayekuwa kiziwi na mwenye utasi anajikuta katika aina ya kifungo na mateso. Anajikutaka katika hali ya kushindwa kuhusiana na wengine vema na vizuri kwa kushindwa kuwasiliana nao vema. Mbaya zaidi nyakati zile za Yesu, kila ugonjwa ulionekana kuwa ni laana kutoka kwa Mungu. Na mbaya zaidi ukiziwi ulionekana karibu sawa na ukoma kwani mmoja alilaaniwa hivi kushindwa hata kulisikia Neno la Mungu na kushindwa kuliwasilisha au kuwashirikisha wengine.

Mwinjili Marko leo anatuonesha kuwa kiziwi na mwenye utasi ni yule ambaye bado hajapata fursa ya kukutana na Kristo Yesu na kuisikia Injili yake, lakini pia kila mmoja anayefunga kwa makusudi masikio yake na hivyo kutoruhusu Injili ya Kristo ipenye na kuingia katika masikio ya moyo wake. Mtume Paulo kwenye Waraka wake kwa Warumi anatuonesha umuhimu wa kulisikia Neno ili tuweze kuamini. (Warumi 10:9-14) “Kama ukikiri kwa kinywa chako kuwa Yesu ni Bwana na ukiamini moyoni mwako kuwa Mungu alimfufua kutoka wafu, utaokoka.” Kwa kumponya mtu yule aliyekuwa kiziwi na mwenye utasi, Yesu leo anatangaza mwanzo mpya kati ya mbingu na dunia. Ni uumbaji mpya kwani kwa kulisikia Neno lake na kuweza kulitangaza kwa watu wote, hapo nasi tunashiriki katika kuujenga ufalme wa Mungu ulimwenguni, kuisikia na kuipeleka ni kujenga mahusiano mapya kama yale ya Bustani ya Paradiso kati ya Mungu na viumbe vyake vyote akiwemo mwanadamu.

Uponyaji wa kiziwi na mwenye utasi ni uponyaji ambao Yesu anataka kumponya kila mmoja wetu. Ni uponyaji wa familia zetu, jamii na taasisi zetu, dini zetu na hata tamaduni na mila zetu. Ndio mwanzo wa majadiliano yenye kusikilizana na kuheshimiana na kuelewa wengine wanaokuwa na mawazo au maono tofauti na yetu. Kushindwa kujadiliana na kuongea baina yetu iwe katika familia zetu au jumuiya zetu au sehemu zetu za kazi au katika jamii zetu za kisiasa na nyingine, ni matokeo ya kubaki kuwa viziwi na wenye utasi. Ni kushindwa kumsikiliza mwingine, na hivyo kushindwa kuingia katika mahusiano na mwingine. Kushindwa kuwasikiliza wengine inatupelekea pia kushindwa kuhusiana nao vema, na hiyo ni hali ya kubaki kuwa kiziwi na mwenye utasi. Yesu Kristo leo anatualika ili atuponye, ili atutoe katika kifungo hicho cha kubaki viziwi na wenye utasi. Neno la Kristo lina nguvu kwani linakuja ili kutuponya sisi sote kwani mara nyingi tumekuwa viziwi na wenye utasi kwa kushindwa kulisikia Neno lake, yaani Injili yake na hivyo kutupelekea pia kushindwa kuliwasilisha kwa wengine sio tu kwa maneno yetu bali hata kwa maisha yetu yanayokinzana na Neno na imani yetu.

Neno la Kristo leo linataka kufungua masikio yetu na kulegeza pia ndimi zetu! Mwinjili Marko pia anatuonesha Yesu Kristo anaponya kwa kutumia ishara karibu kama zile za Kipagani, lakini leo zinapata maana mpya. Ni ishara ambazo ndizo zinatumika katika Ibada ya Sakramenti ya Ubatizo. Kiziwi na bubu tunaona analetwa na haji mwenyewe, hapa tunashangaa kwani huyu mtu sio kipofu kama yule wa Betsaida, ambaye kwa hakika alihitaji watu kumsindikiza na kumfikisha alipo Yesu. (Marko 8:22-23) Mwinjili Marko anataka kutuonesha kuwa ili kukutana na Yesu Kristo, hatuna budi kusindikizwa na wale ambao tayari wamekutana naye na hivi kuona makuu na uweza wake wa Kimungu. Na ndio wajibu wetu nasi kila mmoja wetu wa kuwasindikiza wengine ili nao waweze kukutana na Yesu Kristo, ili nao waweze kupokea uponyaji wa kuwa viziwi na wenye utasi ili waweze kulisikia Neno lake na kuwa watangazaji wa Habari Njema kwa maneno na matendo yao. Na ndio tunaona hata leo wabatizwa na wanaoimarishwa daima wanakuwa na wasimamizi. Ni wajibu wa msimamizi kushiriki kikamilifu katika safari ya imani ya yule tunayemsindikiza aidha siku ya Ubatizo au ya Kipaimara. Ni wajibu pia wa wazazi na ndugu na jamaa yote inayokuwepo kutambua ni wajibu wetu wa kuwa mifano mizuri na mema inayoendana na kweli za Injili ili kuwasadia wanaokuwa wadogo kiimani kukua katika imani yao, kukua katika mahusiano yao na Mungu na wengine.

Mwinjili Marko kila mara baada ya muujiza anatuonesha Yesu akiwakataza wasisambaze au wasiseme juu ya makuu yale, hii ndio ile inayoitwa “siri ya ukuhani wa Yesu”, Yesu hakutaka watu wamtambue kama mtenda miujiza, kama mleta nafuu ile ya kidunia, bali wapate kumtambua kikamilifu baada ya kutimia kwa tendo lile la ukombozi wetu, yaani baada ya mateso, kifo na ufufuko wake.  Na hata mitume wake wanatumwa kutoka na kwenda kuhubiri Injili kwa mataifa yote, sio kabla ya tendo la mateso, kifo na ufufuko bali baada ya ndio wanatumwa na hasa baada ya kumpokea Roho Mtakatifu watoke na kuanza kuhubiri kwa mataifa yote. Mtu yule kiziwi na mwenye utasi anatengwa na makutano, ndio kusema kila mmoja anayekutana na Neno la Kristo Yesu, anayempokea Yesu hana budi kujitenga na namna za kiulimwenguni, sio kwa kukaa mbali na wengine bali kuanza kuongozwa kwa mantiki mpya, sio tena ya dunia hii bali ya Mungu mwenyewe. Ni kukubali kuongozwa na kweli za Injili, kumtegemea Mungu katika yote na hali zote, ni kukubali kuwa kiumbe kipya, kuanza mahusiano mapya na Mungu na wengine pia na viumbe vingine vyote.

Yesu aliinua macho yake juu mbinguni akaugua, ndio kusema anatuonesha muunganiko wake na Mungu, anatuonesha kuwa tunaposali tunaingia katika mahusiano na Mungu, ni kutaka mapenzi ya Mungu yatimie katika maisha yetu, ni kuruhusu Mungu aongoze na atawale maisha yetu, anayetenda muujiza ni Mungu mwenyewe katika maisha ya mwanadamu. Kusali ni kunyanyua mioyo yetu na kumwelekea Mungu, ni kuingia kwenye majadiliano ya upendo na Mungu. Yesu anaweka vidole vyake masikioni mwa yule mtu aliyekuwa kiziwi na mwenye utasi, ni ishara hiyo inatumika siku ya Ubatizo wetu kwa kuwekea vidole masikioni na midomoni, kila mbatizwa anapewa utume na wajibu wa kulisikia Neno la Mungu na kuwa mtangazaji, kila mbatizwa anapokea uponyaji kama mtu yule aliyekuwa kiziwi na mwenye utasi. Mtu yule hakupokea tu uponyaji wa kimwili bali zaidi sana wa kiroho. Mate ni ishara ya nguvu ya Roho wa Mungu kwa mtu yule na ndio pia siku ya Ubatizo wetu tunampokea Roho Mtakatifu, ni nguvu ya Mungu ndani mwetu inayolegeza kila aina ya kifungo ili nasi tukawe mashahidi wa Injili ya Kristo Yesu.

Mate hata katika baadhi ya jamii zetu za Kiafrika ni ishara ya baraka, wazazi au babu na bibi waliwatemea mate kichwani, watoto au wajukuu kabla ya kuanza safari ya kwenda mbali nao, ni ishara ya kuwabariki, ni ishara karibu sawa na ile anayotumia Yesu ya kumjalia na kumshirikisha uzima wa Kimungu huyu aliyekuwa kiziwi na nusu bubu. “Efatha” ni neno la Kiaramayo, ambalo hakika halikuwa kuruhusu kufunguka kwa masikio tu bali kwa mtu mzima, ili mtu yule aweze kufungua milango ya moyo wake na kuruhusu Injili ya Kristo Yesu kuingia na kutawala na kuongoza maisha yake.  Mwinjili Marko anahitimisha sehemu ya Injili ya leo, kwa kutuonesha jinsi watu wale walivyoweza kukiri imani yao. “Wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.” Nawatakia Dominika na tafakari njema.

02 September 2021, 09:09