Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 24 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Kiri ya Imani ya Mtakatifu Petro, Mtume na Kashfa ya Fumbo la Msalaba. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 24 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Kiri ya Imani ya Mtakatifu Petro, Mtume na Kashfa ya Fumbo la Msalaba. 

Tafakari Jumapili 24 Mwaka B: Kiri ya Imani ya Petro: Kashfa ya Msalaba

Kristo Yesu anatangaza kwamba, Yeye ni Masiha, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu, kielelezo makini cha Injili ya huduma ya upendo, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni Masiha wa Bwana anayeleta ukombozi kwa mtu mzima: kiroho na kimwili kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu! Mapya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 24 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Nabii Isaya anatangaza matumaini kwa Waisraeli waliokuwa utumwani Babeli. Anawatangazia ukombozi utakaoletwa na Mtumishi mwaminifu wa Mungu ambaye atapata mateso makali, kifo, lakini atafufuka kwa wafu. Utabiri huu unapata utimilifu wake kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ndiye yule aliyekuja kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na mapendo, inayomwilishwa katika huduma, kielelezo cha imani tendaji. Kiri ya Imani ya Mtakatifu Petro ni tukio muhimu ambalo liliibua taswira halisi ya Masiha wa Mungu Mteseka. Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu na fungamani inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji.

Fumbo hili lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake.  Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Tunajiunga na Baba Mtakatifu Francisko anayefanya hija ya Kitume nchini Hungaria, Jumapili tarehe 12 Septemba 2021 ili kufunga rasmi Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa. “52nd International Eucharistic Congress, (IEC) ambalo lilifunguliwa tarehe 5 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Tunaungana na familia ya Mungu nchini Tanzania katika kufunga Maadhimisho ya Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa, Jimbo kuu la Tabora nchini Tanzania linanogeshwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu chemchemi ya uzima wetu.”

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Kiri ya Imani ya Mtakatifu Petro, Mtume Mk 8: 27-35 “Wewe ndiwe Kristo” ni tukio ambalo limebeba uzito wa pekee sana katika Injili zote nne. Tangu wakati huo, “Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.” Mk 8:31. Kristo Yesu anajitambulisha kuwa ni Masiha mteseka, atakayekataliwa na watu. Kwa Mitume wa Yesu na watu wa nyakati zile, walimtambua Masiha wa Mungu aliyefungamanishwa na masuala ya kisiasa na kijeshi. Lakini, leo Kristo Yesu anatangaza kwamba, Yeye ni Masiha, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu, kielelezo makini cha Injili ya huduma ya upendo, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni Masiha wa Bwana anayeleta ukombozi kwa mtu mzima: kiroho na kimwili. Si kwa mtutu wa bunduki au mapinduzi ya kijeshi, bali kwa njia ya utii kama kielelezo cha utekelezaji wa mapenzi ya Baba yake wa Mbinguni. Anamletea mwanadamu ukombozi wa kweli kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Huu ni ukombozi unaosimikwa katika huduma; kwa kuwaondolea dhambi, kwa kuwalisha na kuwanywesha wakati wa njaa na kiu; kwa kuwaponya na kuwatakasa magonjwa yao na kuwafufua kwa wafu.

Huu ulikuwa ni ufunuo na utambulisho mpya kabisa kiasi cha kushindwa kuingia katika akili na mawazo ya Mtakatifu Petro, ambaye alimchukua na kuanza kumkemea. Lakini Kristo Yesu “Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” Mk 8:33. Kristo Yesu anatumia fursa hii kutoa katekesi ya kina, kuhusu masharti kwa wale wote wanaotaka kumfuasa, wanaotaka kufuata nyayo zake. Mosi lazima wajikane, Pili, wajitwike Msalaba na tatu washike njia ya kumfuasa kikamilifu. Kwa maneno mengine, wafuasi wa Kristo Yesu wanapaswa kutangaza na kushuhudia Injili kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo, kama kielelezo cha imani tendaji. Huu ni mwaliko kwa waamini kupambana na udhaifu wa mwili, dhambi na utepetevu wa moyo, tayari kutangaza na kushuhudia Msalaba kama kielelezo cha hekima na ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Kristo Yesu, ni Masiha wa Mungu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hii ndiyo Kashfa ya Fumbo la Umwilisho linalopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka. Mitume na wafuasi wa Kristo Yesu walizamisha imani yao katika ustawi, maendeleo na mafao ya kisiasa kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau. Kifo, Ufufuko na Maisha ni kati ya mambo ambayo wafuasi wa Emau walikuwa wakijadiliana njiani baada ya mateso na kifo cha Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu wao.

Ni watu waliokuwa wamechanganyikiwa kutokana na Kashfa na upuuzi wa Msalaba, uliozika matumaini yao yote. Wanafunzi hawa walijenga matumaini yao kwa Yesu ambaye amekufa na kushindwa vibaya, kiasi kwamba amezikwa pamoja na matumaini yao yote! Yesu, Mwalimu na Mkombozi aliyewafufua wafu na kuponya wagonjwa akashindwa kujiokoa mwenyewe hadi kuishia kwenye Kashfa ya Msalaba. Walishindwa kuamini ilikuaje Mwenyezi Mungu akashindwa kumwokoa Yesu kutoka kwenye ukatili mkubwa wa kifo. Msalaba wa Kristo ulikuwa ni Msalaba wa mawazo yao kuhusu Mungu; Kifo cha Kristo kilikuwa ni kifo cha yule waliyedhani pengine ni Mungu. Wanafunzi hawa ndio waliokufa na kuzikwa kaburini kutokana na kushindwa kwao kufahamu Fumbo la Msalaba. Liturujia ya Neno la Mungu , Jumapili ya 24 ya Mwaka B wa Kanisa itusaidie kuenenda katika upya wa maisha ulioletwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Tujitahidi kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huruma na Upendo wa Mungu kwa waja wake, kwa kuwa ni Ekaristi kwa jirani!

Liturujia J24
11 September 2021, 15:11