Tafuta

Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa Nchini Tanzania 9-12 Septemba 2021 Kauli mbiu "Ekaristi Takatifu Chemchemi ya Uzima Wetu". Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa Nchini Tanzania 9-12 Septemba 2021 Kauli mbiu "Ekaristi Takatifu Chemchemi ya Uzima Wetu". 

Kongamano IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa, Jimbo kuu la Tabora, Tanzania

Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa, Jimbo kuu la Tabora nchini Tanzania linanogeshwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu chemchemi ya uzima wetu”. Sherehe zote hizi zinaadhimishiwa kwenye Kituo cha Hija ya Huruma ya Mungu Kitulizo cha Moyo, a.k.a “Pahija Ifuchang’holo” kuanzia tarehe 9 hadi 12 Septemba 2021. Ni Kipindi cha Katekesi Kuhusu Ekaristi Takatifu na Utume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa ilianzishwa rasmi na Papa Leo XIII kunako mwaka 1876 ili kusaidia mchakato wa kumwezesha Kristo Yesu: kufahamika, kupendwa na kutumikiwa kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu na fungamani inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu kitaifa iwe ni chachu ya upatanisho, haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Ekaristi Takatifu iwe ni shule ya huduma ya unyenyekevu, tayari kujisadaka kwa ajili ya wengine; kiini cha umisionari na ufuasi wa Kristo. Waamini wawe mstari wa mbele kuonesha mshikamano, upendo na wema; wapanie daima kujenga maisha yao ya kiroho na kimwili, kielelezo cha nguvu ya Ekaristi Takatifu inayopyaisha maisha na kubadili mioyo ya waamini, tayari kuwahudumia na kuwalinda maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ni mwaliko kwa waamini kujitahidi kuwa wakamiliifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu kwa kupinga ukosefu wa haki, rushwa na ufisadi; mambo yanayovuruga umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Kanisa linapania kuwa kweli ni chombo cha haki, amani, umoja na mshikamano na mafungamano ya kijamii. Maadhimisho haya yawe ni chachu ya kupyaisha maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuifia dhambi na kuanza kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha. Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu iwasaidie waamini kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Hapa ni mahali pa katekesi endelevu katika maisha ya kiroho, kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau, waliobahatika kufafanuliwa Maandiko Matakatifu na hatimaye, wakamtambua Kristo Yesu kwa kuumega Mkate. Mama Kanisa anawakumbusha waja wake kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Sadaka; Shukrani na masifu kwa Mungu Baba; Ni kumbu kumbu ya sadaka ya Kristo na ya Mwili wake; Kanisa ni kielelezo cha uwepo wa Kristo kwa nguvu ya Neno na Roho wake Mtakatifu.

Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Tanzania yalipaswa kuzinduliwa rasmi tarehe 30 Juni 2020 huko Jimbo kuu la Tabora kama alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu baada ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara kunako tarehe 7 Oktoba 2018. Jubilei hii ilinogeshwa na kauli mbiu: "Miaka 150 ya Uinjilishaji, Furaha ya Injili". Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora anawakaribisha watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania kushiriki katika Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Tanzania; sanjari na Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Tanzania linanogeshwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu chemchemi ya uzima wetu”. Sherehe zote hizi zinaadhimishiwa kwenye Kituo cha Hija ya Huruma ya Mungu Kitulizo cha Moyo, a.k.a “Pahija Ifuchang’holo” kuanzia tarehe 9 hadi 12 Septemba 2021.

Katika ujumbe wake kwa watu wa Mungu amegusia kwa ufupi historia ya uinjilishaji Ukanda wa Magharibi mwa Tanzania, utume uliofanywa kwa namna ya pekee na Shirika la Wamisionari wa Afrika waliofika rasmi Tabora, Unyanyembe kunako tarehe 12 Septemba 1878 na kesho yake yaani tarehe 13 Septemba 1878 wakaadhimisha kwa mara ya kwanza katika eneo hili, Fumbo la Ekaristi Takatifu chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa. Wamisionari wa Afrika ndio waasisi wa Seminari kuu ya Kipalapala ambayo imekuwa ni kitalu cha miito ya Kipadre. Leo hii kuna “Mapadre wengi wa nchi kavu” wanaochangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Tanzania. Jimbo kuu la Tabora lilianzishwa rasmi kunako tarehe 25 Machi 1953. Askofu mkuu Cornelius Bronsveld, M. Afr., akapewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo kuu la Tabora. Kwa mara ya kwanza, Maandamano la Ekaristi Takatifu yalifanyika tarehe 14 Juni 1925 na tangu wakati huo, waamini wamekuwa wakiandamana na Ekaristi Takatifu kielelezo cha ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu.

Ratiba elekezi iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania inaonesha kwamba, Alhamisi tarehe 9 Septemba 2021 asubuhi, kuna maadhimisho ya Kutabaruku Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu. Ibada hii inaongozwa na Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora. Jioni kutakuwa na Masifu ya Jioni, Kuabudu Ekaristi Takatifu na Mkesha, Ibada inayotarajiwa kuongozwa na Askofu Joseph Roman Mlola, ALCP/OSS, wa Jimbo Katoliki la Kigoma. Ijumaa tarehe 10 Septemba 2021, Askofu Flaviani Matindi Kassala, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi wa Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Tanzania. Ibada hii inatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan ambaye atapata nafasi pia ya kuwahutubia watanzania. Kati ya mada zitakazojadiliwa katika maadhimisho ya Kongamano hili ni pamoja na: Historia ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu. Ekaristi Takatifu na Mtakatifu Yosefu na Bikira Maria. Ekaristi Takatifu na Maandiko Matakatifu. Zab 87:7. Mada nyingine ni Katekesi Kuhusu Ekaristi Takatifu, Ibada ya Upatanisho na Maungamano. Ekaristi Takatifu na Liturujia ya Kanisa. Historia ya Ukristo/Ukatoliki na Changamoto zake katika mchakato wa uinjilishaji Kanda ya Magharibi. Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Tanzania linanogeshwa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Sala za Kanisa, Sakramenti ya Upatanisho pamoja na Katekesi.

Jumamosi tarehe 11 Septemba 2021 Ibada ya Misa Takatifu kwa Heshima ya Bikira Maria itaongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Na jioni Askofu Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki la Bunda ataongoza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Rozari na Kutoa Tafakari. Jumapili, tarehe 12 Septemba 2021ni kilele cha Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa. Ibada ya Maandamano ya Ekaristi Takatifu itaongozwa na Askofu Beatus Christian Urassa, ALCP/OSS, wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga pamoja na Askofu Msaidizi Prosper Lyimo wa Jimbo kuu la Arusha. Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora ataongoza Ibada ya Misa Takatifu ya Kufunga maadhimisho haya. Kuanzia tarehe 13 hadi 15 Septemba 2021 kutafanyika Kikao cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Kikao cha Bodi ya Seminari Kuu. Alhamisi tarehe 16 Septemba 2021 Maaskofu wataanza kuondoka kuelekea Jimboni Morogoro kwa ajili ya kumweka wakfu na kumsimika Monsinyo Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Morogoro na baadaye Jimbo kuu la Dar es Salaam! Yaani hadi raha!

Ekaristi Tanzania
08 September 2021, 15:25