Tafuta

Manyanyaso ya wasichana na mimba za mapema Manyanyaso ya wasichana na mimba za mapema 

Afrika Kusini:Taasisi katoliki inaomba hatua zichukuliwe dhidi ya unyanyasaji

Taasisi ya Katoliki ya Elimu nchini Afrika Kusini inataka serikali nchini humo kuchukua hatua za haraka dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na ujauzito wa mapema.Takwimu za Idara ya Afya ya Jimbo la Gauteng inaonesha kuwa kati ya mwezi Aprili 2020 na Machi 2021 ilirekodi ujauzito wa wasichana 23,000,ambapo miongoni mwa wasichana elfu moja ni kati ya miaka 10 na 14!

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Ukatili wa kijinsia na mimba za mapema zinaongezeka nchini Afrika Kusini. Kulingana na data iliyotolewa siku za hivi karibuni na Waziri wa Ulinzi na usalama ubakaji wa wasichana 10,006 uliripotiwa kati ya mwezi Aprili na Juni mwaka huu, na ongezeko la zaidi ya 70% ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha 2020. Takwimu ambazo zilisukuma Taasisi Katoliki ya Elimu (Cie) kwenda kuomba mamlaka ya Afrika Kusini ili kuingila kati na kuchukua hatua za haraka za kupambana na unyanyasaji wa kijinsia nchini humo. Kwa mujibu wa taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la Aciafrica, linasama kuwa ongezeko la unyanyasaji wa kijinsia pia linaonekana kuhusishwa na ongezeko la wasiwasi kwa ujauzito wa mapema. Katika suala hili, Taasisi Katoliki ya Elimu CIE inataja, hasa, data ya Idara ya Afya ya Jimbo la Gauteng ambayo kati ya mwezi Aprili 2020 na Machi 2021 ilirekodi ujauzito wa wasichana 23,000 ambapo wasichana karibu elfu moja ni kati ya miaka 10 na 14! Takwimu ambazo kulingana na Taasisi inapaswa kuibua maswali kadhaa ya kujiuliza  kwa sababu uhusiano kati ya mambo haya mawili ni dhahiri.

Taasisi Katoliki ya Elimu CIE tayari imewataarifu wakuu na wale wanaohusika na ulinzi wa watoto shuleni juu ya shida hiyo. Walakini, kuna ukosefu wa wafanyakazi wa kijamii na miundo ya msaada kwa familia na wasichana wenyewe ambao wanahitaji kujua wapi waende kupata msaada ikiwa watabakwa. Kwa upande wake, Taasisi inasisitiza kujitolea kwake kufanya kazi kwa ajili ya ulinzi wa watoto na hadi sasa imezindua mpango mkubwa wa uhamasishaji na habari katika shule zote za Katoliki nchini humo. Hata hivyo hofu kubwa juu ya unyanyasaji wa kijinsia nchini Afrika Kusini tayari ilitolewa mwaka jana na Baraza la Maaskofu wa Afrika Kusini (Sacbc), ambao kwa dhati alilaani kuongezeka kwa mauaji kwa wanawake na unyanyasaji wa nyumbani dhidi ya wanawake na watoto wakati wa karantini. Maaskofu walikuwa wametaka kukomeshwa kwa utamaduni wa kukaa kimya na mbinu kamili kujihusisha katika shida hii inayohusisha na sekta zote za jamii, hasa kama ilivyofanywa wakati wa wimbi kuu la UVIKO-19. Baraza la Maaskofu Afrika Kusini (Sacbc) pia iligeukia makanisa yote ili kuzingatia suala hili, ikiongeza ufahamu na kuwaelimisha waamini wote.

Hata hivyo hivi karibuni mwezi Mei imeanzishwa Taasisi mpya katika mapambano dhidi ya manyanyaso ya watoto na watu wazima. Rais wa Kituo cha Ulinzi wa Watoto cha Chuo Kikuu Cha Kipapa Gregoriana, Roma, Padre Hans Zollner alielezea sababu zilizopelekea uundwaji wa Taasisi Mpya ya Athropolojia na kwamba ni katika kazi na jitihada za miaka hii kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kiakili na kupambana dhidi ya kila aina ya vurugu na unyanyasaji wa kila aina. Taasisi Mpya ya Anthropolojia ambayo itakuwa na mafunzo ya kisayansi kuhusu hadhi ya mwanadamu na juu ya utunzaji wa watu walioathirika, (IADC), ni suala ambalo wamependelea wakuu wa taaluma na kuridhiwa na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, ambapo si katika kutazama jina tu, bali ni ule unyeti wake kama alivyothibitisha Padre huyo na mjumbe wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Ulinzi wa Watoto.

Kwa mujibu wa maelezo yake amesema, kuna sababu mbili ya mabadiliko hayo: Awali ya yote, ni kwamba Kituo cha Ulinzi wa Watoto (CCP) hapo awali kisingeweza kuwa na wafanyakazi wake wa kufundisha na kutoa digrii zake za kitaaluma. Kwa sasa, kutokana na mabadiliko kuwa Taasisi ya Anthropolojia, itawezekana kufanya hivyo, kwa njia ambayo walimu na maprofesa wataweza pia kukua zaidi na zaidi. Sababu ya pili ni kwamba wakati walipoanza, karibia miaka tisa iliyopita, nia ya kituo hicho (CCP), ilikua inajikita zaidi juu ya masuala ya manyanyaso ya watoto, na katika harakati za miaka minne iliyopita wameona maendeleo na mabadiliko makubwa, maoni ya umma na katika Kanisa ambazo zimejumuishwa hata watu wazima walioathirika. Kwa maana hiyo walitakiwa wao kubadilika na kufanya jambo ambalo ni muhimu zaidi la kitaaluma.

Kutokana na hilo, kama Taasisi lazima wakue na kuhamasisha watu wenye uwezo wa kuwa profesa, watu ambao wamekwisha kufanya utaalam kupitia katika kituo hicho (CCP). Lakini si hao tu, pia hata wale ambao walikuwa wanaendeleza elimu katika vituo vingine vya elimu katika mantiki hiyo. Kwa sasa wanaendelea kufanya kazi katika nyanja mbali mbali zilizo jitokeza hivi karibuni kama vile: unyanyasaji wa kiroho na kwa maana hiyo  katika muktadha wa kutoa ushauri au mwelekeo wa kiroho, unyanyasaji kwa upande wa watawa katika sehemu nyingine za ulimwengu, shida kubwa ambayo ilishutumiwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa miaka mitatu iliyopita na  suala lote la uwajibikaji kwa wakuu wa mashirika ya kitwa  katika suala zima la manyanyaso ya kijinsia. Malengo yaliyowekwa bayana, Padre Padre Hans Zollner  amethibitisha kuwa wataendelea na hatua zao za masomo na kwa hatua zote wanazofanya kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama vile Mabaraza ya Maaskofu au Wakuu Mashirika ya kitawa. Lakini juu ya yote, kama Taasisi ya Chuo Kikuu, wanataka kuendeleza utafiti zaidi juu ya mada maalum: kwa mfano, jinsi gani dini na taaluma mbali mbali za kielimu zinaweza kushirikiana ili kuongeza jitihada za kuzuia unyanyasaji.

Taasisi Mpya ya Antropologia itakuwa  katika Chuo Kikuu Cha Gregoriana, Roma, ambayo itapanua juhudi zake katika kazi ya ulinzi wa watoto na watu wazima walio katika mazingira magumu na kuhamasisha mazingira salama ambayo yanazingatia heshima ya hadhi ya mwanadamu. Wakati huo huo itapanua kwa kina ukuu wa somo hili na utafiti na kwa wote wanafahamu jinsi gani ilivyo msingi kwa ajili ya kukabiliana na manyanyaso ndani na nje ya Kanisa au jamii. kwa maelezo zaidi:

 https://childprotection.unigre.it/

MANYANYASO
01 September 2021, 15:42