WAWATA Jimbo Kuu DSM Yawasha Moto wa Jubilei ya Miaka 50! Yaani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Jubilei ni kipindi cha kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa: upendo, wema na ukarimu wake kwa WAWATA katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita. Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, ili kuomba: huruma, msamaha, neema na baraka ya kusonga mbele tena kwa ari na moyo mkuu katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Katika kipindi hiki kuelekea kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, hapo mwezi Septemba 2022, wanaongozwa na kauli mbiu “Nuru Yetu Iangaze! Tuyatakatifuze Malimwengu. Miaka 50 ya WAWATA: Upendo, mshikamano na uadilifu wa uumbaji. Kauli mbiu hii inachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu Lk. 1:39: Mapendo kwa jirani: “Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda…” Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 28 Agosti 2021, Kumbukumbu ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya uzinduzi wa maadhimisho kuelekea kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA.
Hii pia ilikuwa ni Siku ya WAWATA Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi ameadhimisha siku hii maalum kwa heshima ya Bikira Maria Malkia wa Mbingu, ili kutoa fursa kwa WAWATA kusali na watoto wao, kuwaombea Waseminari na kuwaunga mkono katika mchakato wa malezi na makuzi yao kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Monika kwa Mtoto wake Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Ruwa’ichi amepembua kwa ufupi historia ya maisha na utume wa Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa pamoja na changamoto za maisha alizokutana nazo wakati wa ujana wake. Mtakatifu Monika, Mama yake Mtakatifu Augustino anayeadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 27 Agosti ya kila mwaka alimlilia, akamwombea na kumsindikiza kwa ushauri, usikivu mwanana, machozi na mahangaiko makubwa. Na kwa sala za Mtakatifu Monika, Augustino akatubu na akamwongokea Mungu. Hatimaye, akabatizwa na kuanza maisha adili na matakatifu na mwishoni akabahtika kutukuka katika maisha na utume wake kama Askofu wa mji wa Hippo, ulioko Kaskazini mwa Afrika.
Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anasema, “Ubi Maior Minor Cessat” yaani kwa Kiswahili cha mtaani ingekuwa hivi “Alipo mkuu, mdogo anaachia ngazi”. Kutokana na heshima, ukuu na utukufu wa Bikira Maria, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kwa kuungana na WAWATA Jimbo, liliamua kuadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Malkia wa Mbingu. Tarehe 22 Agosti, kila Mwaka, Mama Kanisa anafanya kumbukumbu ya Bikira Maria Malkia wa mbingu, Sikukuu iliyoanzishwa na Papa Pio wa XII kunako mwaka 1954 kama alama ya matumaini kwa watu wa Mungu. Ni Sikukuu inayomwonesha Bikira Maria aliyepewa upendeleo wa pekee, ili kushiriki ukuu wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu: Kuhani, Mfalme na Nabii. Hii ni dhamana ambayo Wakristo wabatizwa wanaishiriki kikamilifu mintarafu Sakramenti ya Ubatizo. Papa Pio XII katika Waraka wake wa kitume “Ad Caeli Reginam” anabainisha kwamba, ingawa Sikukuu inaonekana kana kwamba, ni mpya, lakini inachota utajiri wake katika Maandiko Matakatifu, Liturujia ya Kanisa, Sanaa ya mambo matakatifu pamoja na Ibada ya watu wa Mungu kwa Bikira Maria.
Kwa mara ya kwanza Sikukuu hii iliadhimishwa tarehe 31 Mei, lakini baada ya mageuzi ya Liturujia yaliyofanywa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Sikukuu hii ikapangwa iadhimishwe tarehe 22 Agosti ya kila mwaka. Hii ni kumbukumbu inayoadhimishwa na Mama Kanisa kwa heshima ya Bikira Maria, siku chache tu baada ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, hapo tarehe 15 Agosti. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anasema lengo kuu katika maadhimisho haya ni kuungana na WAWATA Jimbo kuu la Dar es Salaam kumsifu, kumtukuza na kumheshimu Bikira Maria aliyependelewa, akakingiwa dhambi ya asili, akapalizwa mbinguni na hatimaye, akapewa hadhi ya kuwa ni Malkia wa Mbingu. Bikira Maria ni mwombezi, mtetezi, kimbilio la mfabo bora wa kuigwa kwa jinsi ya kumfuata na kumshuhudia Kristo Yesu. Utenzi wa Bikira Maria, “Magnificat” unapata chimbuko lake kutoka katika Agano la Kale. Bikira Maria ni kielelezo cha Eva mpya, Mtumishi wa Mungu aliyeuletea ulimwengu Mkombozi, Kristo Yesu, Hakumu na Mpatanishi kati ya Mwenyezi Mungu na mwanadamu.
Kristo Yesu ndiye anayewapatia Mataifa hadhi ya kumjua na kumtumikia Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto kwa waamini kufuata nyayo za Bikira Maria, ili wawe tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Wajitahidi kuwa wamisionari wanaotangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani sanjari na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Bikira Maria alibahatika kuwa ni Mama wa Mungu na mfuasi wa kwanza wa Kristo Yesu, mfano na kielelezo cha utimilifu wa Kanisa. Bikira Maria ni mwombezi, mtetezi na msaidizi wa waamini katika shida na mahangaiko yao. Ni mtangulizi wa waamini wa kwenda na kuishi na Kristo Yesu katika utukufu wake wa mbinguni. Kanisa linamheshimu na kumtukuza Bikira Maria kama Malkia wa Mbingu. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi ameendelea kufafanua kwamba, WAWATA wanapokwenda Visiga kusali pamoja na watoto wao. Ni fursa ya kuwaombea Waseminari ambao wako hapo kwa ajili ya malezi na makuzi yao, ili kupambanua miito yao. Wanasali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaongoza katika maisha yao.
Jimbo kuu la Dar es Salaam linawashukuru na kuwapongeza WAWATA kwa ukaribu na ujirani wao mwema; utayari wa kuwa karibu na watoto wao kwa kuwalea, kuwatunza na kuwasaidia ili wamjue, wampende, wamtumikie na kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Kristo katika ulimwengu mamboleo. Mwishoni waweze kufika mbinguni.Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anasema, anaendelea kuenzi utamaduni wa Jimbo kuu la Dar es Salaam wa kuwahusisha WAWATA katika maisha na utume wa Kanisa na kwa namna ya pekee katika malezi na makuzi ya Seminari ya Bikira Maria, Visiga. Anawashukuru WAWATA kwa moyo wa ukarimu na upendo; majitoleo na sadaka; mshikamano na umoja wa udugu wa kibinadamu katika maisha na utume wao. Waamini watambue daima kwamba, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Kamwe Kanisa haliwezi kutosheka na miito, kumbe, malezi na makuzi ya miito ni dhamana endelevu na fungamani kwa watu wote wa Mungu.
Katika risala yao, Mama Stellah Rwegasira, Mwenyekiti wa WAWATA Jimbo kuu la Dar es Salaam amezungumzia kuhusu wajibu na dhamana ya WAWATA ndani ya Kanisa; umuhimu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA na yale mambo msingi ambayo wanapaswa kuyatekeleza kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Jubilei ya WAWATA. Mpango mkakati wa WAWATA kwa mwaka 2021-2022 ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi! Huu ni mwaka wa kufunga, kusali, kutafakari na kufanya hija kwenye vituo mbalimbali vya hija, kijimbo, kitaifa na Kimataifa kadiri ya hali itakavyoruhusu. Pili ni kuendelea kutekeza sera, mipango na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa kuzingatia vipaumbele vya Kanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu.
Nyaraka zifuatazo ni dira na mwongozo katika Maadhimisho kuelekea Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA: Amoris laetitia yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia. Pia kuna Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” kuanzia tarehe 19 Machi 2021 hadi tarehe 26 Juni, 2022 yanayoongozwa na kauli mbiu “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu.” Malengo makuu ni: kujitahidi kunafsisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka ili kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani; zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Pili, hii ni fursa ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa familia kama shule ya upendo, huruma, haki, amani na ukarimu. Itakumbukwa kwamba, Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, uhai na upendo kielelezo cha ukomavu wa imani. Tatu, waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ndoa inapyaisha upendo wa kibinadamu. Kumbe, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa familia na vijana.
Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ulizinduliwa tarehe 8 Desemba 2020 na utahitimishwa tarehe 8 Desemba 2021. Waraka wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu”: Papa Francisko anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu kuwa ni “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika unyenyekevu Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa. WAWATA inataka kuchota fadhila na tunu msingi za maisha ya Mtakatifu Yosefu ambaye pia ni Msimamizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Wanataka kumwangalia kama Baba wa familia, ili kuendelea kutambua na kuthamini dhamana na wajibu wa baba katika familia. Kuna nia ya kutaka kushirikiana kwa karibu zaidi na UWAKA ili kufanikisha malengo haya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia katika ujumla wake.
Laudato si: Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi na wongofu wa kiikolojia, kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” uliozinduliwa hapo tarehe 18 Juni 2015 mjini Vatican. Baba Mtakatifu anapenda kukazia umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa. Huu ni waraka unaokazia pia umuhimu wa kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kumbe, wanandoa wanao wajibu wa kulinda na kutetea uhai. WAWATA inaangalia jinsi ambavyo itawasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi kwa kuwajengea uwezo wa kiuchumi ili waweze kujitegemea, kutegemeza familia na Kanisa katika ujumla wake! WAWATA, Kumekucha asiye na mwana...! Yaani ukicheza na WAWATA utasutwa mapemaaaa!