Tafuta

Uchaguzi mkuu Zambia: Siasa Safi ni chombo cha haki, amani, upatanisho na umoja wa Kitaifa. Uchaguzi mkuu Zambia: Siasa Safi ni chombo cha haki, amani, upatanisho na umoja wa Kitaifa. 

Uchaguzi Mkuu Zambia 2021: Siasa Safi Ni Chombo Cha Haki na Amani

Zambia, Alhamisi tarehe 12 Agosti 2021 inafanya uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge. Chaguzi nyingi Barani Afrika zimekuwa ni chanzo cha vurugu, uhasama na mipasuko ya kijamii. Wananchi wa Zambia wanahimizwa kulinda na kudumisha amani na utulivu, wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi mkuu nchini humo, yaani wakati wa kampeni, uchaguzi na kutangaza matokeo! Amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2019 anasema, siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani. Ni kielelezo cha demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi yanayowashirikisha wadau mbalimbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani. Siasa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu na kwamba, siasa safi hutekelezwa kwa kufuata katiba, sheria na kanuni maadili; mambo msingi katika kukuza na kudumisha misingi ya amani, haki, ustawi na mafao ya wengi. Siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo katika jamii; ni matunda ya ukomavu yanayojikita katika uongozi bora, maridhiano, utawala wa sheria, uvumilivu, uaminifu na bidii. Kamwe tofauti za kiitikadi kisiwe ni chanzo cha vita, kinzani, vurugu na mipasuko ya kijamii inayowatumbukiza watu kwenye majanga na maafa makubwa!

Baba Mtakatifu anasema, siasa safi ni huduma kwa ajili ya wananchi; inayofumbatwa katika sanaa ya kusikiliza na kushirikisha karama na mapaji kwa ajili ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na usawa; maskini na akina “yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wakipewa kipaumbele cha kwanza. Lakini, ikumbukwe kwamba, amani ni tete sana inapaswa kulindwa na kuhifadhiwa kama mboni ya jicho! Huduma ya amani inajengwa katika mahusiano na mafungamano ya kijamii; kwa njia ya ushirikiano na mshikamano wa jamii na jumuiya ya Kimataifa. Ni katika muktadha huu, familia ya Mungu nchini Zambia, Alhamisi tarehe 12 Agosti 2021 inafanya uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge. Chaguzi nyingi Barani Afrika zimekuwa ni chanzo cha vurugu, uhasama na mipasuko ya kijamii. Wananchi wa Zambia wanahimizwa kulinda na kudumisha amani na utulivu, wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi mkuu nchini humo. Yaani wakati wa kupiga, kuhesabu na kutangaza matokeo. Wadau wote wa zoezi hili wanapaswa kuhakikisha kwamba, uchaguzi unakuwa huru, wa haki na amani, ili uweze kuakisi maamuzi ya wananchi wa Zambia wakati wa kupiga kura!

Askofu mkuu Alick Banda wa Jimbo kuu la Lusaka, Jumapili tarehe 8 Agosti 2021 amewaongoza watu wa Mungu Jimbo kuu la Lusaka kusali kwa ajili ya kuombea amani, usalama na utulivu wakati na baada ya uchaguzi mkuu nchini Zambia. Kinyang’anyiro cha Urais nchini Zambia, kinawashirikisha wagombea 16 ambao kila mmoja anadhani kwamba, akipewa nafasi ataweza kuwahudumia wananchi wa Zambia kama Rais. Wagombea wote wanapaswa kujiandaa kisaiokolojia kwamba, Zambia inamhitaji Rais mmoja tu. Katika ushindani huu mkubwa, kwa wale watakaoshindwa kihalali wakubaliane na matokeo na hivyo kuanza kujipanga tena upya! Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala huu si wakati wa kujikita katika uchoyo na ubinafsi. Wananchi wenye haki ya kupiga kura wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanasukumwa na dhamiri nyofu kuwapigia kura wale wanaodhani kwamba, wataweza kuwaongoza vyema. Zambia inafanya uchaguzi ili kuchagua: Rais, Wabunge 156 na Viongozi wa Wilaya 117.

Uchaguzi Mkuu Zambia
11 August 2021, 14:20