Tafuta

2021.08.31 Misa ya Uzinduzi wa Jubilei ya miaka 100° ya Parokia ya Rutabo, Bukoba,Tanzania ambapo katika fursa hiyo Askofu Rwoma ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa watoto 530 2021.08.31 Misa ya Uzinduzi wa Jubilei ya miaka 100° ya Parokia ya Rutabo, Bukoba,Tanzania ambapo katika fursa hiyo Askofu Rwoma ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa watoto 530 

Tanzania:uzinduzi wa miaka 100 ya Parokia ya Rutabo&kipaimara kwa watoto 530

Imeadhimishwa Misa Takatifu ya Uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 100 ya Parokia ya Rutabo,jimbo katoliki la Bukoba,Tanzania.Katika tukio hilo Askofu Desiderusi Rwoma ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa watoto 530.Hawa ni watoto kutoka vigango vyote vinavyojumuisha Parokia pamoja na watoto wa Shule ya Mtakatifu Yosefu iliyopo Parokia ya Rutabo.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican na Patrick P. Tibanga - Radio Mbiu,Kagera.

Tangu kuingia kwa uinjilishaji barani Afrika, matunda ya kazi ya uinjilishaji yameonekana sana kwa dhati, kila pande ya kona ya Afrika na kama ilivyo katika Parokia ya Rutabo jimbo katoliki la Bukoba Tanzania ambalo limezindua Jubilei ya miaka 100 ya Parokia, tarehe 30 Agosti 2021. Ilikuwa ni sherehe kubwa sana ambayo ilipambwa hasa na vijana 530 kwa kupewa sakramenti ya kipaimara, ambapo wote hao walitokea katika vigango mbali mbali vinavyounda Parokia hiyo ambayo inaongozwa na Padri Godwin Rugambwa, pamoja na idadi kadhaa ya wanafunzi wa Shule ya Mtakatifu Yosefu ambao wanaongozwa na Mwalimu Mkuu wa Shule  Padri Avitus Tibaigana.  Katika maadhimisho ya siku hiyo, wanafunzi wa shule hiyo waliimba wimbo wa “Uje Roho Mtakatifu” kwa kuomba mapaji yote saba ya Mungu ili iwashukie hao waimarishwa.

JUBILEI YA MIAKA 100 YA PAROKIA YA RUTABO,BUKOBA TANZANIA
JUBILEI YA MIAKA 100 YA PAROKIA YA RUTABO,BUKOBA TANZANIA

Misa  Takatifu iliongozwa na Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo katoliki Bukoba, Tanzania, ambaye wakati wa mahubiri aliwaomba  wazazi na walezi kuwalea watoto katika maadili mema yanayompendeza Mungu na kuwafundisha kuipenda na kudumu katika imani na mafundisho ya Kanisa  Katoliki ili wawe mfano bora katika jamii. Katika mahubiri yake Askofu Rwoma amesema kuwa ni vema waimarishwa wakayaishi mapaji saba ya Roho Mtakatifu ili yapate kuwasaidia katika maisha yao na zaidi kumshirikisha Mungu kwa kila jambo wanalolitenda katika maisha yao ya kila siku. Aidha Askofu Rwoma amewataka waimarishwa wote kuzingatia imani yao ikiwemo kuhudhuria maadhimisho ya misa mbalimbali na siku kuu zilizoamriwa  pamoja na kuzingatia sakramenti za Kanisa ikiwemo Sakramenti ya Kitubio na kuwasihi waimarishwa kutovutwa na mali za ulimwengu na kukataa vishawishi vyote vya ulimwengu huku wakimpokea Roho Mtakatifu ili awaimarishe katika Imani yao.

WATOTO 530 WAPEWA KIPAIMARA KATIKA PAROKIA YA RUTABO, BUKOBA.
WATOTO 530 WAPEWA KIPAIMARA KATIKA PAROKIA YA RUTABO, BUKOBA.

Ukristo barani Afrika una historia ndefu inayokaribia miaka elfu mbili ambapo ukristo huo kwa upande wa bara hili umepambwa na wingi wa madhehebu ambayo yamepatikana katika mchakato wa safari kutokana na historia ya Kanisa, baadhi katika bara hilo, na baadhi kutoka katika mabara mengine. Kwa hakika ukristo ndiyo dini kubwa zaidi barani, hasa Kusini mwa janga la Sahara, pamoja na Uislamu ambao unaongoza Kaskazini kwa jangwa hilo. Leo  hii karibu nusu ya Waafrika wote ni Wakristo. Lakini asilimia ya Wakristo inaweza kuwa ndogo katika nchi kadhaa na kubwa katika nchi nyingine. Katika Afrika Kaskazini Wakristo ni wachache.  Na kumbe ni wengi kwa theluthi mbili za bara kusini kwa Sahara. Kwa ujumla Wakristo wanaishi katikati  ya wafuasi wa dini nyingine, hasa uislamu na dini za jadi ambazo pamoja na uinjilishwaji, bado zinaendelea kuwapo, hata kuleta changamoto kubwa katika uinjilishaji, na madhehebu mengine yasiyo ya kikristo ambayo yametokea kwenye mabara mengine.

PADRI GODWINI, RUGAMBWA PAROKO WA RUTABO,ASK. RWOMA NA PADRI AVITUS TIBAIGANA.
PADRI GODWINI, RUGAMBWA PAROKO WA RUTABO,ASK. RWOMA NA PADRI AVITUS TIBAIGANA.

Hata hivyo idadi ya wakristo inazadi kuongezeka kwa haraka sana kila kukicha. Shukrani kwa watumishi wa Mungu kama Mapadri na watawa wazawa na wamisionaria katika kazi ngumu ya kuijilisha Neno la Mungu. Kila baada ya nukta nne Mwafrika mmoja anaingia Ukristo. Wengine huzaliwa katika familia ikiwa na  mzazi mmoja au wote wawili Wakristo tayari. Katika madhehebu mengi kuna desturi ya kuwabatiza watoto wadogo kwa mfano Wakatoliki. Ubatizo huo unawafanya kuwa wanakanisa walio hai kwa kupakwa mafuta matakatifu. Wanapoendelea kukua watafundishwa na pengine hata  kukaribishwa kwenye Kipaimara kadiri ya miongpzo yote ya Kanisa. Katika ibada hiyo kijana anarudia ahadi ya ubatizo wake na kuwekewa mikono na askofu au mchungaji mwingine ambaye anakuwa ameteuliwa na Akofu wa Jimbo na kuombewa ili Roho Mtakatifu amsaidie katika maisha yake ya Kikristo, kutenda na kunena ukweli, kuamini kile ambacho anatenda na kuishi. Madhehebu mengine lakini hayabatizi watoto wadogo. Yanaweza kuwapokea katika Kanisa kwa ibada maalum lakini yanasubiri mpaka mtoto atakapokuwa mtu mzima, halafu apokee ubatizo na kuwa Mkristo rasmi. Njia nyingine ya kukua kwa Kanisa ni ile wanayoiita kuongoka. Maana yake mtu asiye Mkristo anasikia habari njema za imani na kuvutiwa moyoni, kama anayosisitiza mara kwa mara Baba Mtakatifu ya kwamba wakristo wote wawe mashuhuda , kwani ushuhuda ndiyo unapitisha mvuto kwa wale wasio wakristo.

KANISA LA RUTABO LIKIWA LIMEPAMBWA NA WATOTO WA KIPAIMARA 530
KANISA LA RUTABO LIKIWA LIMEPAMBWA NA WATOTO WA KIPAIMARA 530

Kwa maana hiyo mtu huyo baada ya kuvutia  anamwona  kiongozi wa Kanisa na ambaye anamwongoza ili kupata mafundisho juu ya imani na maisha ya Kikristo na ndiyo njia ya ukatekumeni. Baada ya mafunzo hayo ya ukatekumeni  anaweza kubatizwa. Hatua hii mara nyingi kwa watu wazima huwa wanabatizwa katika usiku wa Pasaka kwa upande wa Wakatoliki. Atakuwa mwanakanisa katika dhehebu fulani lakini vilevile kama mkristo katika Kanisa moja takatifu la Bwana Yesu Kristo lililopo popote ulimwenguni; na katika Kanisa Katoliki, linaongozwa na kiongozi mkuu Baba Mtakatifu, Kharifa wa mtume Petro na ambaye kwa sasa ni Papa Francisko. Kwa maana hiyo tunaweza kusema kwamba wafrika walio wengi kidogo, hasa kwa wazee ni watu waliopata uongofu, maana waliwahi kuwa wafuasi wa dini nyingine (hasa dini za jadi, lakini wengine kutoka katika uislamu), wakasikia sauti ya Habari Njema ya Wokovu na wakaamua kumfuata Yesu Kristo mteswa, msulibiwa na kufa na siku ya tatu afufuka katika wafu. 

KUOMBEA MAASKOFU NA JUBILEI PAROKIA RUTABO
31 August 2021, 11:33