Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 22 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Amri za Mungu, Haki, Ukarimu na Upendo kwa Mungu na Jirani. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 22 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Amri za Mungu, Haki, Ukarimu na Upendo kwa Mungu na Jirani. 

Tafakari Jumapili 22 ya Mwaka B: Haki, Ukarimu na Moyo wa Upendo

Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 22 ya Mwaka B wa Kanisa inatukumbusha kuwa wakarimu wenye haki kwa maskini na wahitaji kwa kuondoa mifumo inayowakandamiza wengine na kuwafanya wanyonge na maskini zaidi. Hii itawezekana kama mioyoni mwetu tumejaza wema na ukarimu kwani ulichokijaza moyoni ndicho kinachoakisi matendo katika maisha. Moyo Safi!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 22 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatukumbushwa kuwa wakarimu wenye haki kwa maskini na wahitaji kwa kuondoa mifumo inayowakandamiza wengine na kuwafanya wanyonge na maskini zaidi. Hii itawezekana kama mioyoni mwetu tumejaza wema na ukarimu kwani ulichokijaza moyoni ndicho kinachoakisi matendo katika maisha. Somo la kwanza la kitabu cha Kumbukumbu la Torati (4:1-2, 6-8); linawakumbusha Waisraeli wajibu na sababu za kuzishika Amri alizowapa Mungu. Israeli anaambiwa ili aweze kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zao na ili apate kuishi, lazima kuzikiliza amri na hukumu anazofundishwa, kuzishika kwa moyo na kuzitenda au kuziishi. Katika kufanya hivyo kuna masharti ya kuzingatia; kutokuongeza wala kupunguza neno lolote, katika Amri za Mungu bali wazishikeni na kuzitenda zilivyo, maana hiyo ndiyo hekima yao na akili zao. Kuzishika na kuzitenda amri za Mungu ni kitambulisho chao machoni pa mataifa kuwa wao ni taifa kubwa, ni watu wenye hekima na akili kwa maana Mungu yuko karibu nao kila wamwitapo. Na tena hakuna taifa lenye amri na hukumu zenye haki kama Torati ambayo Mungu amewapa na kuiweka mbele yao. Kwa ubatizo sisi kwa njia ya Yesu Kristo sisi nasi tumefanywa taifa teule la Mungu, Taifa kubwa, hivyo ili tuweze kuishi vyema sharti kuzishika na kuziishi amri za Mungu na maagizo ya kanisa kama yalivyo maana ndiyo hekima na akili atupayo Mungu Baba yetu.

Somo la pili la Waraka wa Yakobo kwa watu wote (1:17-18, 2, 27); linatueleza kuwa zawadi njema tuliyopata toka kwa Mungu Baba ni ufunuo wake katika Injili ya Yesu Kristo. “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.” Ufunuo huu ndilo neno la ukweli tunalopaswa kulishika kwa kuwasaidia wenye shida na kujihadhari na yote yanayotutenga na Mungu. Yakobo anatuasa akisema; “Wekeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.” Kumbe namna njema ya kuiishi injili ni kwa maneno na matendo yetu mema kama anavyosisitiza Yakobo; “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Haina maana kukiri kanuni ya imani na kusema nasadiki huku tunatoa na kupokea rushwa, tunawanyang’anya yatima mali zao, tuna kiburi, tunaua watu, tunazini, tuko mafisadi, tunatukana, tuna wivu na kusema mambo ya kipumbavu. “Dini iliyo safi, na isiyo na taka, isiyo na unajisi, mbele za Mungu Baba, Yakobo anatuambia ni hii: “kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao”. Basi tukifanya hivyo tutakuwa na hazina mbinguni.

Injili ilivyoandikwa na Marko (7:1-8, 14-15, 21-23; inatufundisha kwamba si matendo ya nje yanayomfanya mtu najisi, bali yanayotoka moyoni. Kwa hiyo dhambi za mawazo ni asili ya uovu wa matendo ya nje. Fundisho hili la Yesu ni kuwakosoa mafarisayo kwa kuwaona wanafunzi wake kuwa wadhambi sana kwasababu walikula chakula “kwa mikono najisi”, yaani bila kunawa. Kwa maana; “Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao; tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali”. Mafarisayo na waandishi walimuuliza Yesu swali ambalo kimsingi ni swali la kumshutumu Yesu mwenyewe wakisema; “Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi?” Yesu anawajibu kwa kunukuu utabiri wa Nabii Isaya kuwa wao ni wanafiki maana humheshimu Mungu kwa midomo ila mioyo yao iko mbali naye; wanamuabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu” (Mk.7:7). Yesu anaendelea kuwaaambia kuwa; wanaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu.

Kisha akawageukia makutano na kuwafundisha ukweli akiwaambia; “Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu (Mk. 7:15-23). Maana moyoni hutoka matashi mabaya au mawazo mabaya. Moyoni hutoka uchoyo. Moyoni hutoka mawazo ya wizi. Moyoni hutoka upumbavu. Moyoni hutoka mawazo ya uzinzi. Moyoni hutoka mauaji. Moyoni hutoka wivu, rushwa, ukaidi, ulaghai, masegn’enyo. Ndiyo maana waswahili husema; Lililo moyoni ulimi huiba. Ukiongea neno zuri ulimi utakuwa umeliiba toka moyoni. Ukiongea neno baya ulimi unaliiba toka moyoni. Hii ndiyo kusema moyo ni makao ya mawazo mazuri na mawazo mabaya. Ni makao ya hisia, hamu, huba na chuki. Kumbe ni vyema kuulisha na kuujaza moyo yaliyo mema ili ndani mwake yatoke yaliyo mema. Basi tuzingatie haya; Amri za Mungu ni hekima na akili kwani zinatuonyesha ni lipi la kutenda. Amri za Mungu zinatuonyesha mapenzi ya Mungu kwetu. Zinatusaidia kuwa wakamilifu, kutenda haki na kusema ukweli kama wimbo wa katikati unavyoimba; “Bwana, ni nani atakayekaa katika kilima chako kitakatifu? Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, atendaye haki na kusema ukweli” (Zab.15:1-5).

Kwa hiyo tusipozishika amri za Mungu, matendo yetu yataongozwa na mawazo yetu binafsi au mawazo ya watu wengine. Na hayo yasioongozwa na Mungu yanatutia unajisi mawazo mabaya ya “uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, na upumbavu.” Amri za Mungu zi juu ya mila zetu na sheria nyingine maana zatuongoza katika kutenda mema. Jambo jema ni lile linaloendana na asili au maumbile ya kibinadamu. Amri za Mungu ndizo zatuonyesha lipi ni jema kwa sababu Mungu aliyetuumba ndiye anajua asili yetu. Kwa hiyo, sheria zozote lazima ziendane na Amri za Mungu, siasa ziongozwe na Amri za Mungu, biashara ziongozwe na Amri za Mungu, utaratibu wa nyumbani uongozwe na Amri za Mungu, sheria za nchi ziongozwe Amri za Mungu. Mzaburi alipouliza; “Bwana, ni nani atakayekaa katika kilima chako kitakatifu? Alijibiwa; “Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, atendaye haki na kusema ukweli, ambaye hakumtendea mwenziwe mabaya, hakumsengenya jirani zake atimizaye viapo vyake”. Basi tukumbuke daima kuwa kibali cha kuingia mbinguni ni swali hili; nilipokuwa uchi ulinivika, nilipokuwa gerezani ulikuja kunitazama, nilipokuwa na njaa ulinipa chakula, nilipokuwa na kiu ulininywesha, nilipokuwa mgonjwa ulikaja kunifariji”. Nasi tufanye hayo ili kibali chetu kikamilike.

J 22 Mwaka B
25 August 2021, 15:31