Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Yesu anaimarisha utashi, anazima njaa na kiu ya maisha ya kiroho na kupyaisha matumaini. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Yesu anaimarisha utashi, anazima njaa na kiu ya maisha ya kiroho na kupyaisha matumaini. 

Tafakari Jumapili 19 ya Mwaka B: Yesu Kiini Cha Matumaini Mapya!

Mungu anayetujalia mahitaji yetu mbalimbali ndiye aliye pia nguvu yetu wakati wa udhaifu na mapungufu yetu ya kibinadamu. Tunapopitia magumu, changamoto au migogoro ya maisha ya kiroho na kimwili, Yeye anatuimarisha na kutujalia nguvu ya kuweza kusonga mbele katika safari yetu. Anaimarisha utashi wetu, anazima njaa yetu na anaamsha upya matumaini ndani yetu.

Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya 19 ya mwaka B wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inaamsha tumaini ndani yetu na kutoa mwaliko wa kujiaminisha kwa Mungu aliye nguvu na uzima wetu. Tunatafakarishwa ya kwamba Mungu anayetujalia mahitaji yetu mbalimbali ndiye aliye pia nguvu yetu wakati wa udhaifu na mapungufu yetu ya kibinadamu. Tunapopitia magumu, changamoto au migogoro ya maisha ya kiroho na kimwili, Yeye anatuimarisha na kutujalia nguvu ya kuweza kusonga mbele katika safari yetu. Anaimarisha utashi wetu, anazima njaa yetu na anaamsha upya matumaini ndani yetu.

TAFAKARI: Katika somo la kwanza Nabii Eliya anajikuta katika hali ya uchovu na kukata tamaa. Haoni msaada tena hata anatamani kufa. Yuko katika mgogoro wa kiroho. Huyu ni nabii ambaye alitenda mambo makubwa na kudhihirisha uweza wa Mungu. Alipambana na wafalme na akawashinda manabii wa uongo wa Baal. Lakini imekuaje sasa anakata tamaa? Inakuaje sasa haoni chema chochote ndani yake? Yuko katika mahangaiko na giza. Katika hali yake hii Mungu anampelekea msaada kwa njia ya malaika. Malaika anampa chakula na maji naye Eliya anapata nguvu ya kusonga mbele kuelekea katika mlima wa Mungu. Mungu ni kimbilio na nguvu ya watu wake. Hawaachi kamwe waelemewe. Katika udhaifu wao yeye uwapa nguvu tena na kuamsha ndani yao matumaini mapya.

Katika somo la pili Mtume Paulo anawapa Waefeso tumaini kwa kuwakumbusha kuwa wanao muhuri wa Roho Mtakatifu, yaani, wamefanywa kuwa wana wa Mungu. Hivyo basi, Mungu hawezi kuwaacha kamwe kwa sababu ni watoto wake. Anawaongoza daima kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Kwa sababu hiyo yawapasa kuenenda kama wana wapendwa wa Mungu, watu wenye tumaini na wenye kuona na kutenda mema na si kama watu waliokata tamaa, wenye kulaani na kutenda maovu. Wasimhuzunishe Roho wa Mungu akaaye ndani yao. Katika Injili Yesu anananung’unikiwa sababu ya kile alichosema na kufundisha ya kuwa yeye ni chakula kutoka Mbinguni. Yesu anatumia nafasi hii kuweka tumaini kwa watu hawa. Anaona wazi mahangaiko yaliyomo ndani ya mioyo ya watu wanaomfuata. Anajua wazi kuwa njaa na kiu ya watu hawa haviwezi kuzimwa kwa chakula cha kawaida kama walivyotaka. Njaa na kiu ya watu hawa vinazimwa kwa uwepo wa Mungu na kwa muunganiko wa kweli naye. Watashiba na kupoza kiu yao kwa chakula kitokacho Mbinguni, yaani mkate wa uzima ambaye ni Yesu mwenyewe. Yeye ndiye anayewavuta watu kwa Mungu.

KATIKA MAISHA: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, masomo ya Dominika hii yanatukumbusha ukweli ya kwamba sisi wanadamu ni viumbe dhaifu. Hata wale ambao tunawaona kuwa ni bora sana kuna wakati wanaelemewa na kukata tamaa. Kuna wakati tunanung’unika na kulaani. Upo wakati ambapo maisha yetu yanagubikwa na giza na hatuoni tena tumaini. Upo wakati ambapo tunapata mgogoro wa kiroho na tunakuwa dhaifu. Lakini ni katika udhaifu ndipo tunaijua nguvu ya Mungu. Tusingaliweza kuijua vema nguvu na uweza wa Mungu ikiwa hatujaonja udhaifu. Sisi sote tutapitia nyakati za ukame na tutakutana na magumu katika safari yetu. Kuna wakati tutaona shaka na kudhani ya kuwa hatuna msaada wowote. Katika hali hiyo tunachopaswa si kujitazama sisi wenyewe bali kumuelekea Mungu aliye nguvu yetu katika udhaifu. Tunaweza kupata nguvu na kuwa na tumaini jipya la kuendelea mbele katika maisha yetu ikiwa tunaegemea kwake Mungu. Mungu hatuachi kamwe bali anatupa msaada katika safari yetu. Lakini lazima tufungue jicho, tuuone msaada na kuupokea.

Kama ilivyokuwa kwa Eliya ndivyo ilivyo kwetu sote.  Mungu anatutegemeza katika safari yetu kwa kutuletea msaada. Kuna malaika wa Mungu ambaye atatuletea msaada wakati wa shida. Msaada wa Mungu unakuja kwetu kwa namna mbalimbali, yaani, kupitia watu na matukio. Je, unaposongwa na migogoro ni wapi unakimbilia kupata faraja na msaada wako? Aidha, masomo ya Dominika hii yanatukumbusha kuwa sisi ni wana wa Mungu na tunabeba muhuri wa Roho Mtakatifu. Kwa sababu hiyo tunapasika kuishi kweli kama wana wa Mungu na kuenenda katika njia njema, njia ya upendo. Mtume Paulo anatuhasa ya kuwa mambo mabaya na mienendo mibovu haipaswi kuwa sifa ya wana wa Mungu wenye chapa ya Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwetu kutoa maisha bora na ya mfano kwa wengine. Kama wakristo lazima tuwe watu wa tumaini na si watu wa uchungu, ghadhabu na hasira. Maisha yetu lazima yawe kielelezo cha uwepo wa Mungu kwa watu wake. Sisi lazima tuwe sababu ya kuamsha matumaini katika maisha ya wengine.

Jambo jingine muhimu ambalo tunaalikwa kufanya katika Dominika hii ni kujiweka karibu na Mungu. Katika zaburi tunaalikwa kuonja na kuona ya kuwa Bwana yu mwema. Mwaliko huu wa kuuonja wema wa Mungu unawekewa mkazo katika Injili na Yesu mwenyewe anayewaalika watu wampokee yeye kama chakula cha uzima maana kwa kufanya hivyo anawafungulia njia ya kumwendea Mungu, aliye Baba wa wote. Sisi wanadamu ni watafutaji. Yapo mambo mengi sana tunayotafuta katika maisha na safari yetu hapa duniani. Basi katika kuhangaika na mambo mengi tumtafute Mungu kama kipaumbele cha kwanza. Yesu ametufungulia njia hiyo katika Ekaristi takatifu ambamo iko siri ya upendo wa Mungu. Ninakutakia Dominika Njema.

07 August 2021, 15:15