Tafuta

Lazima kuelimisha zaidi juu ya wimbi la tatu la UVIKO-19 kwa kufuata itifaki zote zinazotolewa Lazima kuelimisha zaidi juu ya wimbi la tatu la UVIKO-19 kwa kufuata itifaki zote zinazotolewa 

Nigeria:wanawake katoliki wahamasisha kuzuia wimbi la tatu la UVIKO-19

Wanawake katoliki nchini Nigeria wako mstari wa mbele katika kuhamasisha kuzuia maambukizi ya wimbi la tatu la UVIKO-19 na kuhamasisha watu wapate chanjo.Ni Bi Mary Ashibi Gonsum, Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Katoliki nchini Nigeria (CWON)ambaye amemua kuhamasisha wahusika wakuu wa chama hiki ili kusaidia mamlaka ya nchi katika kuzuia wimbi hilo nchini humo.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Katika kuhamasisha hali halisi ya virusi vya korona katika wimbi baya la  tatu linalosambaa kwa haraka sana, Bi Mary Ashibi Gonsum, Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Katoliki nchini Nigeria  (CWON), amemua kuhamasisha wahusika wakuu wa chama hiki katoliki  ili kusaidia mamlaka  ya nchi katika kuzuia wimbi la tatu la UVIKO -19 katika nchi hiyo. Kwa mujibu wake amesema: “Hofu kubwa ya wimbi la tatu la UVIKO-19 ndiyo mwanzo wa busara, kwani kuna ongezeko jipya. Lazima kufanya kila liwezekanalo ili kuzuia kuambukizwa. Mara kwa mara ni lazima kuwa na mawasiliano na viongozi kwa ngazi za kijimbo, kidekania na kiparokia ili kuhakikisha kuwa wanahamasisha juu ya wimbi la tatu la virusi na ulazima wa kujikinga kukaa salama”.

“Huu ni msaada mkubwa ambapo Umoja wa Wanawake Katoliki Nigeria (CWON) upo katika mikoa mitano ma majimbo katoliki 55 nchini Nigeria. Miongozo ni rahisi, tunasubiri kwamba wajumbe wetu waendelee kuvaa barakoa, kunawa mikono, kutumia sanitaiza, kutunza umbali wa kijamii, na si tu wakati wa kufanya mikutano tu bali mahali popote wanapokuwa. Lazima kuhakikisha kwamba familia zao zinaendelea kufanya hivyo pia” amesisitiza Bi Gonsum.  “Wenyeviti wa kitaifa, mkoa na majimbo wanapaswa kuhamasisha, ili kuongeza uhamasishaji na kuwashawishi watu, hasa katika parokia, kudumisha itifaki za UVIKO-19 na hatua nyingine za afya ya umma kama vile elimu ya hatari ya kuambukizwa, wakijitokeza kwaajili ya vipimo inapobidi na kukubali chanjo, amesisitiza Bi Gonsum.

Akizungumzia juu ya hofu ya wale ambao hawataki kupata chanjo na maswali halali kuhusu ufanisi na usalama wa chanjo, mwenyekiti wa CWON amewashauri wanawake wote wajihadhari na habari potofu zenye lengo baya na badala yake wakimbilie kupokea chanjo hiyo. Hatimaye kiongozi huyo wa wanawake katoliki amewaombea uponywaji wale wote walioathiriwa na virusi, na pia kwa wafanyakazi wa afya na wataalamu wengine walio mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya virusi vya korona. Akikumbusha wanawake kwamba Mungu hawaachi watoto wake, Bi Gonsum almesema, “Tunaamini kwamba Mungu ndiye mwokozi wetu na kwamba hashindwi kamwe.  Nina hakika kwamba tutaishi na kuona wema wa Bwana mwishoni mwa janga hili”.

Ikumbukwe kuwa kufikia sasa, nchini Nigeria imeorodhesha kesi 174,315 za UVIKO-19, kulingana na takwimu rasmi; 165,005 waliruhusiwa, na 2,149 wamekufa. Kulingana na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Nigeria (NCDC), kesi 407 zilirekodiwa katika Jumapili ya Jumapili Agosti 1 na wakati madaktari wanaanza tena mgomo wa kitaifa kwa muda usiojulikana. Wakati huo huo, dozi milioni 4.8 za chanjo ya Moderna iliyotolewa na serikali ya Amerika imewasili nchini humo.

03 August 2021, 15:09