Tafuta

2021.08.26 Picha ya Mapadri mara baada ya misa ya washiriki wa Mkutano wa kwanza wa HAWAKA kanda ya Mwanza 2021.08.26 Picha ya Mapadri mara baada ya misa ya washiriki wa Mkutano wa kwanza wa HAWAKA kanda ya Mwanza 

Tanzania:Askofu Rwoma ahimiza Vijana katoliki kufunga ndoa kwa wakati!

Askofu Desderius Rwoma wa Jimbo Katoliki la Bukoba Tanzania,amehimiza Vijana katoliki kufunga ndoa kwa wakati kwa kuzingatia maadili ya imani ya Kanisa Katoliki na kuacha tamaa za ujana.Amesema hayo katika mkutano Mkuu wa Kwanza wa Halmashauri ya Walei,Kanda ya Mwanza uliofanyika Chuo cha Kumbukumbu ya Kardinali Rugambwa,Bukoba.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican na Patrick P. Tibanga, Radio Mbiu–Kagera.

Jumatano tarehe 25 Agosti 2021, umefanyika Mkutano wa Kwanza wa Halmashauri ya Walei wa Katoliki (HAWAKA) Kanda ya  Mwanza unaoleta pamoja majimbo 8 katoliki ambayo ni Jimbo katoliki la Kayanga, Rulenge-Ngara, Geita, Bunda, Shinyanga, Musoma , Bukoba na Jimbo Kuu katoliki Mwanza, uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Kardinali Rugambwa (CARUMCO) Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania, kwa kuongozwa na mada: “Jukumu la viongozi wa Almashauri ya Walei katika kukuza dhamira ya familia”, katika mwanga wa barua ya Mtakatifu Paulo: “Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. (2,Kor 8,7).

Askofu Rwoma akiwa katika ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza wa HAWAKA Kanda ya Mwanza
Askofu Rwoma akiwa katika ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza wa HAWAKA Kanda ya Mwanza

Katika hotuba ya Ufunguzi wa mkutano huo, Askofu Desderius Rwoma wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania, ametoa wito kwa vijana wote katoliki kufunga ndoa kwa wakati lakini kwa kuzingatia maadili ya inamni ya Kanisa katoliki na kuachana na tamaa mbaya za ujana. Hata hivyo amesema si vijana peke yake, lakini hata watu wazima ambao wana umri na wanapaswa pia kufunga ndoa, badala ya kuchukuana hivi hivi na kukaa bila kufunga ndoa.  Kwa kusisitiza zaidi Askofu Romwa amesema kwamba ndoa ni Muungano wa kisakramenti kwa hiari ya kifungo cha upendo wa kudumu kati ya mume na mke, kwa maana hiyo kijana anatakiwa kujitafakari kabla ya kuingia wito huo na pia kuwatakia vijana kuzingatia maadili bora ya Kanisa kwa kuacha kuishi uchumba sugu, kuacha ushirikina, umbea pamoja na tamaa za ujana na kuipokea vyema zawadi ya watoto watakojaliwa na Mungu. Ndoa inayozungumzwa  Askofu amebainisha kwamba ni ndoa ya mwanamme na mwamke ( Mw 2, 24), huku akitoa mfano kwamba dunia hii ina mengi kwani unakuta  nchi nyingine za kigeni zimfikia hatua ya kuhalisha ushoga.

Washiriki wa Mkutano wa Kwanza wa HAWAKA kanda ya Mwanza
Washiriki wa Mkutano wa Kwanza wa HAWAKA kanda ya Mwanza

Kwa Upande wake Mratibu wa shughuli za Walei katoliki Kanda ya Mwanza, Padre Faustine Kamugisha ambaye pia Paroko wa Parokia Parokia ya Minziro Jimbo Katoliki la Bukoba amewataka Viongozi wa Halmashauri za Walei kutumia vyema Ulimi wao na kuzingatia Kanuni maalum za kushawishi waamini ikiwemo  kuwa mfano mzuri kwa waamini, kuwaheshimu waamini na kuwatia motisha waamini kwa kila wanachofanya kwa ngazi ya Parokia. Naye Padri Adeodatus Rwehumbiza katibu wa Idara ya Walei Jimbo katoliki la Bukoba na Paroko wa Parokia ya Kanisa Kuu la Bukoba, katika kuwasilisha mada ya vijana na ndoa takatifu katika mkutano huo, amesema ikiwa wajibu wa viongozi wa halmashauri ya walei  ni katika kustawisha  utume wa familia , je  viongozi tunashirikije?  Hii ni kwa sababu amesema “Utakuta familia ya kiongozi wa Halmashauri ya Walei anauhasama na moja ya familia anayoingoza, anashindwa hata kwenda kuongoza sala kwenye nyumba ambayo hawapatani, na weee ukiwa kiongozi unamalizaje tatizo hilo?

Washiriki wa Mkutano wa kwanza wa HAWAKA
Washiriki wa Mkutano wa kwanza wa HAWAKA

Katika mkutano huo wa Kwanza wa Almashauri ya Walei Katoliki (HAWAKA) umekuwa na maazimio ambayo ni:  Kutoa elimu ya dini na semina juu ya Sakramenti ya ndoa na umuhimu wake kwa wakati sahihi kwa wanaoingia katika ndoa na waliokaa muda mrefu kwenye ndoa, pamoja na kuwaandaa vyema makatekista ili kutoa elimu ya ndoa na sharti la Katekista huyo awe katika wito wa ndoa; Kutoa elimu juu ya WAWATA(Umoja wa Wanawake Katoliki Tanzania) kwa chipukizi kuanzia ngazi ya Jumuiya, Kigango na Parokia ili kuwapata warithi na viongozi wazuri wa WAWATA, na mengineyo ambayo yameweza kuazimiwa katika mkutano huo muhimu kwa Kanda ya Mwanza.

Hata hivyo tukumbuke kuwa Mkutano huo wa Kwanza wa Halmashauri ya Walei Katoliki wa Kanda ya Mwanza umewaleta pamoja viongozi hao wa Halmashauri ya Walei kutoka majimbo yanaounda Kanda ya Mwanza ambayo ni: Jimbo Katoliki la Bukoba, Musoma, Bunda, Shinyanga, Rulenge-Ngara, Geita, Kayanga na Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza. 

HOTUBA YA ASK RWOMA BUKOBA
26 August 2021, 16:34