Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia: Uchaguzi Mkuu 2021: Demokrasia Imetamalaki Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia: Uchaguzi Mkuu 2021: Demokrasia Imetamalaki 

Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia: Demokrasia Imetamalaki!

Maaskofu Katoliki Zambia wanasema, huu ni ushindi wa wananchi wote wa Zambia kwa sababu demokrasia imetamalaki. Kwa wale wote walioshinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 12 Agosti 2021, waendelee kukuza na kudumisha amani na utulivu; umoja na mshikamano wa udugu miongoni mwa watu wa Mungu nchini Zambia. Walioshindwa wajipange upya kwa matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anafafanua changamoto za siasa safi katika Ujumbe wa Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 kwa kusema, amani ni sawa na matumaini yanayosongwa na changamoto pamoja na magumu yanayowaandama walimwengu. Zote hizi ni kutokana na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka na matokeo yake ni matumizi mabaya ya madaraka na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbalimbali za maisha ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu inapaswa kudumishwa.  Ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi na kwamba, mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii. Ni kiongozi anayeaminika na kuthaminiwa na jamii na kwamba anajitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri! Baba Mtakatifu anasema, hivi ni vigezo muhimu sana wakati wa kufanya chaguzi mbalimbali, ili kuhakikisha kwamba, haki, dhamana na wajibu vinatekelezwa kikamilifu. 

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia (ZCCB) linampongeza Rais mteule wa Zambia, Bwana Hakainde Hichilema wa Chama Cha United Party for National Development (UPND) na Bwana Edgar Lungu, Rais anayemaliza muda wake kutoka katika Chama cha Patriotic Front (PF). Maaskofu Katoliki Zambia wanasema, huu ni ushindi wa wananchi wote wa Zambia kwa sababu demokrasia imetamalaki. Kwa wale wote walioshinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 12 Agosti 2021, waendelee kukuza na kudumisha amani na utulivu; umoja na mshikamano wa udugu miongoni mwa watu wa Mungu nchini Zambia. Wale walioshindwa katika kinyang’anyiro hiki, waanze kujipanga kwa kesho iliyo bora zaidi. Bwana Edgar Lungu, Rais anayemaliza muda wake ameridhia matokeo na kuwashukuru wananchi wa Zambia kwa kumpania nafasi ya kuwaongoza kama Rais. Alitamani tena kuendelea kuwatumikia wananchi wa Zambia kwa: akili, nguvu na uweza wake, lakini mambo yamekwenda kinyume chake. Kwa sasa anasema, anajiandaa kukabidhi madaraka kwa Rais mteule Bwana Hakainde Hichilema wa Chama Cha United Party for National Development (UPND). Haki, amani, upendo, msamaha na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni kati ya mambo muhimu yaliyopewa uzito mkuu!

Rais mteule Bwana Hakainde Hichilema amenukuliwa na vyombo vya mawasiliano ya jamii akiwataka wananachi wote wa Zambia kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kuendeleza uhuru wa kujieleza kadiri ya sheria, taratibu na kanuni za Zambia. Huu ni wakati wa kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano pamoja na msamaha, kwa kujielekeza katika utawala bora unaozingatia na kuheshimu sheria, taratibu na kanuni msingi za Zambia.Vita ya kiuchumi inahitaji umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kunogesha kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wa kizazi kipya.

Zambia Demokrasia
19 August 2021, 16:32