Tafuta

Sakramenti ya Kipaimara inawaimarisha waamini ili kuwa ni mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wajitahidi kuyafahamu Maandiko Matakatifu na Mafundisho ya Kanisa Sakramenti ya Kipaimara inawaimarisha waamini ili kuwa ni mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wajitahidi kuyafahamu Maandiko Matakatifu na Mafundisho ya Kanisa 

Umuhimu wa Kipaimara, Biblia Takatifu na Ushuhuda wa Imani!

Sakramenti ya Kipaimara inathibitisha na kuimarisha neema ya Ubatizo. Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara wanakirimiwa mapaji ya Roho Mtakatifu. Mama Kanisa anawaombea watoto wake kutoka kwa Mungu ili awakirimie Roho Mtakatifu Mfariji. Awape Roho wa hekima na akili; Roho wa ushauri na nguvu; Roho wa elimu, ibada na uchaji wa Mungu! Ushuhuda makini!

Na Ndahani Lugunya, - Dodoma, Tanzania.

Mababa wa Kanisa wanasema, kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara muungano wa wabatizwa na Kanisa hufanywa kuwa mkamilifu zaidi, kwani wanatajirishwa kwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuieneza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu Mfufuka. Sakramenti ya Kipaimara inathibitisha na kuimarisha neema ya Ubatizo. Waamini waliozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu, wakaokolewa kutoka katika dhambi ya mauti, kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara wanakirimiwa mapaji ya Roho Mtakatifu. Mama Kanisa anawaombea watoto wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili awakirimie Roho Mtakatifu Mfariji. Awape Roho wa hekima na akili; Roho wa ushauri na nguvu; Roho wa elimu na ibada. Mama Kanisa anawaombea kwa Mwenyezi Mungu ili awajaze Roho wa uchaji kwa njia ya Kristo Yesu! Matunda ya Sakramenti ya Kipaimara ni kuzamishwa zaidi katika kufanywa waana wapendwa wa Mungu na hivyo kuunganishwa kwa nguvu zaidi na Kristo Yesu.

Ni Sakramenti inayoongeza ndani ya waamini vipaji na karama za Roho Mtakatifu na hivyo waamini kukamilishwa zaidi kiungo cha waamini na Kanisa la Kristo Yesu. Waamini wanapata nguvu na ari ya kueneza na kutetea kwa maneno na matendo kama mashuhuda aminifu na wa kweli wa Kristo Yesu, tayari hata kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wakristo walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara daima wanakumbushwa na Mama Kanisa kwamba, wamepokea mhuri wa kiroho. Yaani, Roho wa hekima na akili, shauri na nguvu; elimu, ibada na uchaji mtakatifu. Ni dhamana na jukumu la waamini kulinda amana na utajiri huu. Mwenyezi anawatia alama na amewajaza amana yake, Roho Mtakatifu nyoyoni mwao. Rej. KKK 1285-1321.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma nchini Tanzania, hivi karibuni ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 190 kutoka katika Parokia ya Mtakatifu Gemma Galgani, Nkuhungu, Jimbo kuu la Dodoma. Katika mahubiri yake, amewataka vijana waliokomaa, kiimani, kimaadili na kiutu, kuhakikisha kwamba, wanamshirikisha Mungu Roho Mtakatifu vipaumbele na changamoto na fursa katika maisha. Wajenge na kudumisha utamaduni wa kusali, kutafakari na kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa zinazowakirimia neema na baraka za kuweza kusonga mbele. Vijana wasivutwe na mambo ya nje tu katika maisha yao ya baadaye! Kwa wale wanaotaka kufunga ndoa, wasikimbilie kuona mavazi mazuri na “mkorogo wa wasichana”. Kwa wasichana wasiwakimbilie “vijana waliopiga pamba nyepesi, wanaotembea kwa kudunda na wenye pochi nene” wakadhani kwamba, hapo ndipo walipofika na roho yao imetulia!

Bali katika maamuzi mazito ya maisha wasali na kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwapatia wachumba, wema, watakatifu, wachamungu na waadilifu watakaosaidiana kujenga, kudumisha na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia. Watambue kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Kwa kuwa makini katika maamuzi yao, kwa hakika wanaweza kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Bila nguvu na utamaduni wa sala, yote ni ubatili mtupu! Pale vijana wanapoteleza na kuanguka kwa kushindwa kufanya maamuzi makini na yenye busara, wawe wepesi kumkimbilia Mwenyezi Mungu ili kuomba msamaha, tayari kutubu, kuongoka na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika imani, matumaini na mapendo!

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya amewataka waamini kujenga utamaduni wa kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha. Maandiko Matakatifu yanasema kwamba, Imani inapata chimbuko lake kwa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, kiasi kwamba, Biblia inapaswa kuwa ni Maktaba ya kwanza kabisa kuwamo ndani ya Familia ya Kikristo, ili familia hii iweze kuonja uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu katika maisha na vipaumbele vyake. Kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya kifamilia ni sehemu ya mchakato wa kurithisha imani inayofumbatwa katika ukimya wa Mwenyezi Mungu aliyefunuliwa na Kristo Yesu kama huruma na upendo wa Baba wa milele. Kati ya “majanga” yanayoziandama Familia nyingi za Kikristo ni kudhani kwamba, Maandiko Matakatifu yanasomwa tu wakati wa Ibada ya Misa, Jumapili na Siku kuu zilizoamriwa.

Watu wenye hekima na busara zao waliwahi kusema kwamba, dunia inasimikwa katika nguzo kuu tatu: Biblia, Liturujia na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, imekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kutafakari Neno la Mungu, kuimarisha imani na hatimaye, kumwilisha Neno hili katika uhalisia wa maisha. Hii ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza waamini kujitaabisha: kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, wakianzia kwenye Familia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo na kwenye Vyama vya Kitume Maparokiani. Hizi ni juhudi pia za uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Familia zijenge utamaduni wa kusali, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu katika maisha yao ya kila siku. Wazazi na walezi wawajengee watoto wao uwezo wa kutamani na kusoma Biblia Takatifu. Biblia iheshimiwe na kutunzwa vyema. Askofu mkuu Beatus Kinyaiya anakaza kusema, kwa kufanya hivi waamini watakuwa wanatekeleza kikamilifu: Unabii, Ukuhani na Ufalme wao, unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Takatifu ya Ubatizo. Wazazi wafuatilie vyema malezi na makuzi ya watoto wao ili kujenga taifa la watu wema, waadilifu na watakatifu!

Wakati huo huo, Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida, hivi karibuni naye ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo 42 kutoka katika Parokia ya Mtakatifu Padre Pio, Mwenge, Jimbo Katoliki la Singida. Aliwataka waamini kusimama imara katika imani na kamwe wasiyumbe yumbe; watafute na kuambata utakatifu wa maisha kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Kamwe wasitafute njia ya mkato kwa changamoto za maisha kama vile ukata wa fedha na magonjwa kwa kutaka kufanyiwa miujiza ya uponyaji! Waamini wajitahidi kuyafahamu vyema Mafundisho ya Kanisa ambayo yanachota utajiri wake kutoka katika Biblia Takatifu, Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hizi ni nyenzo msingi zinazoweza kuwasaidia waamini kutambua na kuishi kikamilifu Mafundisho ya Kanisa bila kusahau mwanga angavu wa Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium” yanayotolewa na viongozi wa Kanisa. Roho Mtakatifu amewakirimia waamini Mapaji yake Saba na kati ya Mapaji hayo kuna paji la akili. Imani ipewe umuhimu wake katika maisha ya waamini kwani akili ya binadamu ina ikomo wake! Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida alitumia maadhimisho ya Ibada hii ya Misa Takatifu kufafanua kwa kina na mapana Mapaji Saba ya Roho Mtakatifu katika maisha ya waamini!

Kipaimara
20 July 2021, 15:41