Tafuta

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani 25 Julai 2021: Mshikamano wa upendo kati ya wazee, vijana na watoto. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani 25 Julai 2021: Mshikamano wa upendo kati ya wazee, vijana na watoto. 

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya: Siku ya Wazee Duniani 25 Julai 2021

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB, linawataka vijana wa kizazi kipya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na wazee kwa kutambua kwamba, wazee ni zawadi muhimu sana kwa binadamu na wala hawana mbadala! Uzoefu na busara za wazee ni kiungo na hamasa kwa maisha ya wanajamii licha ya changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, Jumapili tarehe 25 Julai 2021, Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani inayokaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya unanogeshwa na kauli mbiu “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Hii ni ahadi ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya na wazee, kushirikishana na hatimaye, kuwa ni wadau pia katika mchakato wa uinjilishaji mpya, unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Siku ya Wazee Duniani ni mwendelezo wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kuhusu: uhai, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Vijana wanahamasishwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kujikita katika maisha ya sala, tayari kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Wazee wanaweza kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kutekeleza dhamana hii kwa ari na moyo mkuu. Ni katika hali na mazingira kama haya, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB, linawataka vijana wa kizazi kipya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na wazee kwa kutambua kwamba, wazee ni zawadi muhimu sana kwa binadamu na wala hawana mbadala! Uzoefu na busara za wazee ni kiungo na hamasa kwa maisha ya wanajamii. Pamoja na changamoto mbalimbali za maisha ya uzeeni bado wazee wana nafasi na mchango mkubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wazee ni alama ya utimilifu wa maisha ya mtu na jamii katika ujumla wake. Wazee ni walezi kwa watoto na vijana. Wazee ni: urithi, amana na utajiri kwa jamii kwani uzoefu na busara zao ni ushuhuda wa kinabii kwa sasa na kwa siku za baadaye. Wazee wanayo dhamana kubwa ya kufundisha na kuwarithisha vijana amana na utajiri unaobubujika kutoka katika imani. Kama Kanisa linalojali, watu wa Mungu nchini Kenya wana wajibika kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya wazee, vijana na watoto.

Hii ni siku muhimu sana kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda na kwamba, Kanisa linawapenda na kujali ustawi, maendeleo, utu, heshima na haki zao msingi. Vijana watambue kwamba, wazee ni baraka ya jamii kwani wazee “wamekula chumvi nyingi” wana busara na hekima; wana sera na mikakati ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wazee wanajisikia kuwajibika zaidi katika jamii! Katika ulimwengu mamboleo, wazee wanakabiliwa na changamoto nyingi sana na kati ya hizi ni: shutuma za uchawi kutokana na watu kujizamisha katika imani za kishirikina. Ni watu wanaoelemewa na upweke hasi, kiasi cha kujikatia tamaa ya maisha. Ni watu wanaokumbana na umaskini wa hali na kipato. Kwa sasa kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, wazee wengi wako katika hatari ya kuambukizwa na ugonjwa huu. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, linayataka majimbo, parokia, vigango na familia ya watu wa Mungu nchini Kenya, kuhakikisha kwamba, wanaadhimisha tukio hili, kwa kuwakutanisha wazee, vijana na watoto, ili kwa pamoja waweze kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya zawadi ya maisha!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wazazi na walezi wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya imani kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani, matumaini na mapendo miongoni mwa watoto wao. Wazazi na walezi warithishe imani hii kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kutambua na kuenzi kweli msingi za maisha kadiri ya upendo na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Watoto wasaidiwe kupata mwanga na ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yao. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, wazazi wawasaidie watoto wao kutambua na kuthamini zawadi ya maisha inayopaswa kulindwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, linawaalika waamini wote katika Makanisa mahalia kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho haya, ili kukoleza moyo wa uinjilishaji kwa kutambua kwamba, wazee wana ndoto na vijana wana unabii kama ambavyo anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Katika kipindi hiki ambacho mahusiano na mafungamano ya kifamilia yanalegalega, Siku ya Wazee Duniani iwe ni fursa ya kuboresha mahusiano haya ya kifamilia, kwa kujenga na kudumisha upendo kati ya vijana wa kizazi kipya pamoja na wazee, ambao wanayo mengi ya kuwafundisha na kuwarithisha vijana wa kizazi kipya. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii.

Maaskofu Kenya
17 July 2021, 15:13