Tafuta

Uhuru wa kidini unatishiwa na vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kidini na kiimani, chuki na uhasama! Uhuru wa kidini unatishiwa na vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kidini na kiimani, chuki na uhasama! 

Uhuru wa Kidini Ni Msingi wa Haki, Heshima na Utu wa Binadamu

Katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi, hadharani au peke yake. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Rej. DH 2.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulizingatia hasa: mema ya kiroho kwa kila mtu; ukweli na haki; Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kanisa linawajibu wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, linahimiza umuhimu wa kulinda dhamiri nyofu pamoja na wajibu wa kimaadili. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba: wanaendeleza Mafundisho ya Kanisa kuhusu haki msingi za binadamu zisizoondosheka na katika sheria za muundo wa jamii. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufunda dhamiri za watu, ili kutambua utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. DH.1.

Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani. “The U.S. Conference of Catholic Bishops” USCCB, kuanzia tarehe Jumanne tarehe 13 hadi Alhamisi tarehe 15 Julai 2021 linaendesha mkutano wa Kimataifa kuhusu Uhuru wa Kidini, huko Jijini Washington, DC. Ni mkutano ambao umeandaliwa na Dini, Madhehebu pamoja na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa yapatayo 40.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB limefurahishwa sana na hatua hii, inayopania kutoa sera na mikakati itakayosaidia kuragibisha uhuru wa kidini sehemu mbalimbali za dunia. Takwimu zilizotolewa na “Pew Forum on Religion and Public Life” zinaonesha kwamba, asilimia 83% ya watu wanaokadiliwa kuwa ni bilioni 7 ya idadi ya watu wote duniani, wanaishi katika nchi ambazo kuna kinzani na mipasuko ya kidini inayofanywa na Serikali husika au makundi ya kijamii. Jumuiya ya Kimataifa, tamaduni, dini na siasa hazina budi kujielekeza ziaidi katika mchakato wa kulinda na kudumisha uhuru wa kidini, sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu. Pamoja na mambo mengine mkutano huu wa Kimataifa unapania kuragibisha umuhimu wa uhuru wa kidini ndani na nje ya Marekani. Pili ni kuwamasisha watu wa Mungu kuchukua hatua madhubiti zitakazolinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

USA: Uhuru wa Kidini
13 July 2021, 15:10