Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 17 ya Mwaka B wa Kanisa: Moyo wa upendo na ukarimu dhidi ya uchoyo na ubinafsi unaoendelea kutawala katika ulimwengu mamboleo. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 17 ya Mwaka B wa Kanisa: Moyo wa upendo na ukarimu dhidi ya uchoyo na ubinafsi unaoendelea kutawala katika ulimwengu mamboleo.  

Tafakari Jumapili 17 ya Mwaka B: Moyo Wa Ukarimu Dhidi Ubinafsi

Mwinjili anajaribu kuoanisha na kuhusianisha tukio la ishara ya mikate pamoja na tukio la kihistoria la kutoka utumwani Misri. Yesu leo anavuka kama vile Musa alivyowavusha Wanawaisraeli katika Bahari ile ya Shamu, na ndio tunaona leo hakuna chombo kinachotajwa kumvusha Yesu. Ukarimu wa kijana mdogo unasaidia Kristo Yesu kutenda ishara kubwa, kielelezo cha Unabii wake!

Na Padre Gaston George Mkude, Roma.

Amani na Salama! Dominika tano mfululizo tumekuwa tukisoma Injili ya Marko, leo Liturjia inatualika kugeukia Injili ya Yohane na hasa sura ile maarufu ya sita, juu ya Yesu kama chakula cha uzima. Mwaka B wa Kanisa kwa kawaida tunasoma Injili ya Marko, lakini Liturujia na Mama Kanisa katika busara yake ameingiza pia Injili ya Yohane sura ile ya sita kwa Dominika tano mfululizo. Injili ya Marko inatupa masimulizi mawili juu ya muujiza wa Yesu kulisha makutano mikate. Na ndio tunaona kwa jinsi anavyotoa mkazo na msisitizo huo, hapo Mama Kanisa ameona ili kupata mafundisho ya kina hatuna budi kugeukia sura ya sita ya Injili ya Yohane. Leo tunasikia juu ya muujiza ule wa kugawa mikate kwa watu wengi na baadaye zaidi katika dominika zijazo tutasikia juu ya mafundisho ya Yesu mkate wa uzima, aliyoyatoa akiwa katika sinagogi la Kapernaumu. Ni vema ili kupata ujumbe kusudiwa na Mwinjili Yohane, badala ya kuwahi kuhitimisha juu ya fundisho la Yesu la Ekaristi Takatifu, ambalo kwa kweli linagusiwa sio mwanzoni mwa sura ile ya sita bali mwishoni kabisa, hivyo niwaalike kusoma na kubaki na kile ambacho kipo mbele yetu ili kukwepa kupotoka au kupata maana inayokuwa sio ile inayokusudiwa na Mwinjili.

Kati ya miujiza iliyofanywa na Bwana wetu Yesu Kristo, ni muujiza huu wa kugawa mikate unayosimuliwa mara nyingi zaidi na wainjili wote wanne. Wainjili wote haidhuru mara moja wanatupa masimulizi ya muujiza huu, na wainjili Mathayo na Marko wanasimulia mara mbili juu ya muujiza huu, hivyo kufanya masimulizi juu ya kugawa mikate kuwa sita. Na ndio hapo tunaweza kujiuliza, kwa nini Kanisa lile la awali linatoa msisitizo mkubwa kabisa juu ya muujiza huu? Yesu alitenda miujiza mingine mingi tena mikubwa zaidi, lakini kwa nini Wainjili wote wanne wanatoa mkazo na msisitizo mkubwa kwa muujiza huu? Na kama ndivyo, kwa nini basi miujiza mingine inasimuliwa mara moja peke yake tofauti na muujiza huu wa leo? Muujiza wa mikate kama unavyosimuliwa na Mwinjili Yohane ni tofauti na jinsi inavyosimuliwa na wainjili wengine. Na ndio mwaliko wangu leo kujaribu kuingia ndani ya Injili hii ili tuweze kwa pamoja kuchota ujumbe unaokusudiwa kwetu. Na ndio tunaona pia Mama Kanisa ameingiza sura ile ya sita ya Injili ya Yohane kwa Dominika tano mfululizo, ili tuweze kuchota mafundisho ya kina kabisa juu ya utambulisho wa Yesu kama mkate wa uzima.

Kwanza yafaa kutambua kuwa Mwinjili Yohane hauiti kama muujiza bali kama ishara, na pia hatusikii moja kwa moja kuwa Yesu aliifanya mikate na samaki kuwa mingi na wengi ili kuwatosha watu wote, na badala yake ni mikate ile ile na samaki wale wale kidogo waliwekwa kwa ajili ya wote mpaka kila mmoja akapata kadiri ya haja na mahitaji yake na kusaza. Na bado wakaweza kukusanya mabaki vikapu kumi na viwili vya mikate, ndio kusema waliweza kupata kila mmoja na bado hawakuweza kumaliza chote kilichowekwa mbele yao. Hivyo tunaona mara moja msisitizo wa somo la Injili ya leo haupo katika ongezeko la mikate wala samaki na badala yake moyo na roho ile ya kushirikiana kidogo kinachokuwepo kwa wote kadiri ya uhitaji wa kila mmoja wetu. Falsafa ya ulimwengu mamboleo ni kuwa na kila kitu kwa wingi katika maisha, iwe ni pesa, afya, elimu, miaka ya kuishi, marafiki, mafanikio, na kadhalika na kadhalika. Na huu ndio ugonjwa wa wengi wetu, wa kujikusanyia, wa kujilimbikizia, wa kujijali na wenye kutaka na kusaka zaidi na zaidi. Ugonjwa huu wa kujilimbikia unaakisi hasa utamaduni wa kifo, unaotokana na maisha yenye kujaa hofu ya kifo, na ndio dalili ya wazi ya kukosa imani.

Kwani tunakuwa watumwa wa vitu na mali na badala ya kuwekeza katika upendo na ukarimu kwa Mungu na kwa jirani. Na kwa kweli somo la Injili ya leo, Yesu anatufundisha juu ya ugonjwa huu wa kujilimbikizia na kujikusanyia kila kitu, ugonjwa wa kutaka zaidi na zaidi katika maisha, ni njaa ya vitu na mali.Yesu leo anatupa dawa ya ugonjwa wetu huu, dawa ambayo ni kinyume kabisa na mantiki, utamaduni na falsafa ya ulimwengu wetu, Yesu leo anatuonesha njia salama na sahihi ya ugonjwa wa ubinafsi na umimi ni ile ya kushirikiana sote kwa pamoja bila ubaguzi kidogo kinachokuwepo mbele yetu. Pasaka, ndio sikukuu ya Wayahudi ilikuwa karibu. Mwinjili Yohane anatuonesha ni wakati gani Yesu alitenda ishara ile. Ndio kusema mazingira yalikuwa ni pale walipokumbuka kukombolewa kwao kutoka utumwani Misri. Ndio kusema Mwinjili anajaribu kuoanisha na kuhusianisha tukio la ishara ya mikate pamoja na tukio la kihistoria la kutoka utumwani Misri. Yesu leo anavuka kama vile Musa alivyowavusha Wanawaisraeli katika Bahari ile ya Shamu, na ndio tunaona leo hakuna chombo kinachotajwa kumvusha Yesu.

Kama vile Musa alivyowaongoza watu wengi ndivyo na Yesu leo wanamkusanyikia watu wengi na hapo anatenda ishara kama vile Musa nyakati za kuwakomboa Wanawaisraeli. Mara mbili Yesu anapanda juu mlimani ni kama Musa alivyokuwa akipanda juu mlimani na huko kupokea maagizo ya jinsi ya kuliongoza taifa lile teule. Wakiwa jangwani Musa aliwalisha Wanawaisraeli mana, na leo Yesu anawalisha pia makutano. Na hata mwishoni watu wale wakamtambua Yesu kama Nabii anayepaswa kuja ulimwenguni na ndivyo ilivyokuwa pia kwa Musa. (Kumbukumbu la Torati 18:18) “Nitawasimamishia kati ya ndugu zao nabii afananaye nawe, nitamtia kinywani mwake maneno yangu naye atawaambia kila nitakachomwamuru.” Ndio kusema somo la Injili ya leo, linatualika kumwangalia Yesu kama Musa mpya, aliyekuja ili kututoa kutoka utumwani na kutufanya huru, kutoka hali duni na mbaya na kutufanya kuwa na uzima wa kweli. Ni kwa ujio wake anatupa namna mpya ya kuishi maisha yetu, sio tena ya kuwa watumwa wa mali na vitu bali watu huru, wenye upendo wa kweli na usio na masharti kwa Mungu na kwa jirani.

Nia na shabaha kubwa ya Musa ilikuwa ni kuwaongoza na kuwafikisha Wanawaisraeli katika nchi ile ya Kaanani, nchi ya maziwa na asali, lakini Yesu Kristo amekuja ili kutuongoza na kutufikisha katika nchi ile ya ahadi, ndio ufalme wa Mungu, ufalme ambao kila mmoja wetu atakula na kushiba na kusaza. (Isaya 25:6). Niwasihi kila mara tunapozungumzia juu ya ufalme wa Mungu, kwa kweli tusifikiri juu ya maisha baada ya maisha ya hapa duniani, bali ni kuwa na kichwa kipya, mwono mpya na namna mpya ya kuishi maisha yetu hapa duniani, maisha yanayoakisi mpango na mapenzi ya Mungu kwetu duniani. Ni uumbaji mpya, ni ulimwengu unaofuata sio mantiki yake bali ile ya Mungu mwenyewe. Ndio ulimwengu ambao upendo ndio amri kuu na inayotawala na kutuongoza katika kila nyanja ya maisha ya mwanadamu. Ni ulimwengu ambao hakuna hata mmoja wetu atakayetindikiwa na mahitaji yake ya lazima na ya muhimu, kwani hakuna hata mmoja anayejiangalia na kujali mambo yake mwenyewe bali kwa kumwangalia mwingine kwa upendo na kushirikiana naye. Leo kwa bahati mbaya tunaishi katika ulimwengu unaokuwa kipofu na bubu kwa shida za wengine, ni ulimwengu wa kila mmoja ajali mambo na maisha yake mwenyewe, kila mmoja aishi maisha yake bila kumwangalia wala kumjali mwingine.

Dominika ya leo pia imetengwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni wazee na wajukuu. Ndio kusema anatukumbusha sisi sote umuhimu wa kuwajali wazee wetu wanaokuwepo iwe katika familia zetu, mitaa na jumuiya zetu, parokia zetu na popote pale. Na pia wajibu wa wazee wa kuwarithisha vijana na hasa wajukuu imani thabiti na ya kweli. Ni Dominika ya kuweza kupata pia rehema kamili kadiri ya maelekezo ya Mama Kanisa. Niwaalike leo kuwaombea wazee na wajukuu wote ulimwenguni, hasa wadumu katika mahusiano ya upendo na kuvumiliana. Wazee na wajukuu wasiwe chanzo cha mitafaruku na kutoelewana bali kuungana kwani sote tunaunganishwa na Kristo Yesu katika upendo wa kweli. Labda swali linaweza kuwa, Je, kuna uwezekano wa kuwa na ulimwengu wa namna hiyo? Je, maliasili zetu za ulimwengu zinaweza kutosheleza mahitaji ya kila mmoja wetu na kubaki na ziada? Ni maswali haya wengi leo tunajiuliza, iwe katika familia zetu, sehemu zetu za kazi, hata katika jumuiya za mapadre na watawa, kote tunaweza kuwa mashahidi kuwa kumejaa ubinafsi na umimi wa hali ya juu kabisa. Kila mmoja anajiona ni yeye ndiye mwenye nafasi ya kwanza na haki ya kumiliki au kutumia kile kidogo kinachokuwepo.

Katika masimulizi ya “Mishnah” ya Kiyahudi waliamini ili mhitaji apate mahitaji yake ya msingi basi ilibidi japo kwa siku apate 1/12 ya dinari. Na ndio tunaona Filipo katika somo la Injili ya leo anafanya mahesabu ya haraka haraka; kwa dinari 200 wanawezaje kulisha na kutosha watu wapatao takribani 4800? Katika Injili ya Luka, simulizi hili tunaona Mitume wakimwambia Yesu awaage makutano kwa kuwaruhusu waende zao wakajitafutie mahitaji yao. (Luka 9:12) Kwa maneno mengine, hili sio swali linalohusiana na imani, hivyo wanakuja kwetu ili tusali pamoja nao, kutafakari Neno la Mungu pamoja nao, kusikiliza mahubiri; wanapokuwa na njaa, kila mmoja aende akajipange mwenyewe. Na ndio tunaweza kuona hata katika mazingira yetu ya leo, ufalme wa Mungu upande mmoja na upande mwingine ni mahitaji ya kimwili ya watu. Leo Yesu anatuonesha kuwa hatupaswi kuyatenganisha, na ndio tunaona Kanisa linaalikwa kila mara kijitafakari na kujiangalia na hasa utume wake kwa maskini na wahitaji. Na ndio tunaona iwe katika maparokia yetu, jumuiya zetu ndogo ndogo za Kikristo umuhimu wa kuwajali maskini na wahitaji bila kuwabagua iwe kwa imani zao au itikadi zao. Na leo tujihoji nafasi ya wazee wanaokuwa katika uhitaji mkubwa katika familia zetu, jumuiya zetu na hata parokia zetu.

Andrea nduguye na Simon Petro anaingilia kati katika kwa kuonesha kuwa kati yao kulikuwa na kijana mdogo aliyekuwa na mikate mitano na samaki wawili. Lakini hata hapo bado anaonesha wasiwasi wake na mashaka makubwa kuwa kilichopo hakiwezi kuwatosha watu wote wale. Chakula ni kidogo kulinganisha na umati mkubwa wa watu wale. Ni katika muktadha huo wa mashaka na wasiwasi, Yesu anawaambia waalike watu kuketi. Mwinjili anatuonesha kuwa mahali pale palikuwa na nyasi, na ndio kusema sio tu anataka kutuonesha mazingira yale bali zaidi ndio kusema inaakisi Zaburi ile ya 23:1-2 Zaburi ya Bwana ndiye mchungaji wetu…kwenye malisho ya majani mabichi. Ndio kusema ni Yesu Kristo mwenyewe aliye mchungaji wetu wa kweli. Ni Yesu Kristo anayetulisha kwenye majani mabichi. Na ndio Yesu anatualika kufuata mantiki yake, ya kuwaketisha watu, ya kuwalisha wengine, ya kuwahakikishia wengine usalama wao hata kabla ya wa kwetu wenyewe. Ni mwaliko wa kumpenda mwingine kama Yesu mwenyewe anavyotupenda.

Ni kwa njia ya mikate na samaki wa yule kijana mdogo ambaye kwa kweli hatujui kwa hakika sana habari zake, ya kuwa alikuwa akiiuza mikate ile au aliitunza kwa ajili yake na labda familia yake. Hayumkini juu ya habari zake, lakini ni kwa msaada wa kijana mdogo umati ule ukapata kula na kubakisha. Na ndio mantiki ya Yesu Kristo kwa kila mmoja wetu ni kuwa na moyo na roho kama ya kijana yule mdogo katika maisha yetu, ya kutoa na kuweka mbele ya wengine hata kile kidogo tunachokuwa nacho, kuwashikirisha wengine na hasa wahitaji upendo wa dhati na wa kweli. Upendo hautudai kutoa kingi au kufanya mambo makubwa bali hata katika udogo na unyonge na uduni wetu, kila mmoja kwa nafasi yake anaalikwa leo kuwa mjumbe wa upendo, kuwajali na kuwashikirisha wengine wanaokuwa wahitaji kwa kile kidogo tulichojaliwa. Kila mmoja wetu leo anaalikwa kuwa kijana yule mdogo ambaye anatoa mikate ile ya shayiri na samaki wale na kuweza kulisha umati mkubwa wa watu.

Kijana mdogo anakuwa ni kielelezo na mfano wa mfuasi wa kweli wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hakika ulimwenguni kunaweza kutokea muujiza mkubwa ikiwa kila mmoja wetu ataongozwa na mantiki ya kijana huyu mdogo aliyekuwa na mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili. Ni mantiki sio ya kujilimbikizia na kuficha kwa ajili yetu wenyewe tu bali ya kuweza kuwashirikisha wengine tone la upendo. Ni mwaliko wa kuwa watu wa kuwashirikisha wengine tone la upendo katika maisha ya siku kwa siku ya ufuasi wetu. Rafiki wa kweli wa Yesu Kristo ni wale wanaokuwa tayari kufuata mantiki yake, na mantiki yake ni hii ya kuwaketisha na kuwashikirisha wengine kidogo tunachojaliwa katika maisha yetu. Niwatakie Dominika na tafakuri njema. Leo ni Dominika ya wazee na wajukuu tunapokaribia kumbukumbu ya Watakatifu Yoakimu na Anna, Jumatatu tarehe 26 Julai 2021.

24 July 2021, 11:04