Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 14 ya Mwaka B wa Kanisa: Nguvu na neema ya Mungu inavyojidhihirisha katika udhaifu wa mwanadamu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 14 ya Mwaka B wa Kanisa: Nguvu na neema ya Mungu inavyojidhihirisha katika udhaifu wa mwanadamu. 

Tafakari Jumapili 14 ya Mwaka B: Nguvu ya Mungu Inayookoa!

Masomo ya dominika hii yanatueleza kuwa katika kutimiza mpango wake, Mungu anawachagua watu wa kawaida kabisa tunaowafahamu na kuyafahamu, mazuri yao, madhaifu yao, familia zao, wazazi wao hata kazi na kipato chao. Hawa Mungu anawatuma kwetu watuletee ujumbe, baraka na nguvu zake za kuokoa. Nguvu na neema ya Mungu inajifunua katika udhaifu wa binadamu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 14 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatueleza kuwa katika kutimiza mpango wake, Mungu anawachagua watu wa kawaida kabisa tunaowafahamu na kuyafahamu, mazuri yao, madhaifu yao, familia zao, wazazi wao hata kazi na kipato chao. Hawa Mungu anawatuma kwetu watuletee ujumbe wake, neema zake, baraka zake na nguvu zake za kuokoa. Lakini kwa kuwa tunawafahamu na tumewazoea wakati mwingine tunawakataa na kuwadharua lakini tujue kuwa tunakataa na kudharau ujumbe wa Mungu ambao mwisho wake ni hukumu ya milele. Somo la kwanza la Kitabu cha Nabii Ezekieli (2:2-5); ni ujumbe wa Mungu kwa Ezekieli anapomtuma kuwa Nabii kwa wana wa Israeli wakiwa uhamishoni Babeli. Katika ujumbe huu Mungu anamweleza Ezekieli hali halisi ya watu anaenda kuwapa ujumbe wake kuwa wana ugumu wa mioyo, ukaidi na uasi. Mungu anamwambia Ezekieli; “Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli wanaoasi, walioniasi mimi, wao na baba zao wamekosa juu yangu. Na wana wao hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni mingumu.”

Mungu anamwambia Ezekieli kuwa anapaswa kujua kuwa hawa watu wanaweza kumsikiliza au wasimsikilize akisema; “Na kwamba watasikia au kwamba hawa kusikia, maana ndio nyumba ya kuasi”. Mungu alitambua kabisa kuwa wana wa Israeli ni watu wenye shingo ngumu. Lakini ni katika hao waliopotea anamtuma mjumbe wake ili awaokoe hao. Alifanya hivyo ili kwamba hata kama hawatabadilika, walau wajue wanalopaswa kufanya na kwa jinsi hiyo wanaweza kulaumiwa kwa sababu wameambiwa wanalopaswa kutenda. Mungu hachoki kututumia ujumbe wake kwa njia ya watumishi wake hata kama tukiwa na mioyo migumu, waasi na tusiosikia bado anaendelea kuturudisha kwake. Ni juu yetu kuupokea au kuikataa neema hiyo. Lakini tutambue siku yaja, siku ya kiama ambapo kila mmoja atasimama mbele ya kiti cha hukumu ya haki ambapo tutaitamani hii neema tusiione. Kumbe wakati ndio sasa wa kuisikia sauti ya Mungu tusifanye migumu mioyo yetu.

Somo la pili la Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (12:7-10); ni ujumbe wa Paulo akiwaeleza wakorintho kuwa licha ya hali yake ya kibinadamu aliweza kuifanya kazi ya Mungu kwa neema ya Mungu tu. Kutokana na udhaifu wa mwili wake, Paulo alijifunza kwamba kufaulu kwake katika kazi ya kuhubiri Injili si mapato ya nguvu yake mwenyewe, ila ni neema ya Mungu. Tukiwa na neema hiyo taabu za mwili si kitu. Paulo anatufundisha kuwa tukifanikiwa katika maisha yetu tusijivune maana ni kwa neema ya Mungu tu tunafanikiwa. Wakati mwingine tukifanikiwa tunanyanyua mabega juu kana kwamba ni kwa nguvu na uweza wetu tumefanikiwa katika maisha. Tukifanya hivyo shetani anapata mwanya wa kutupiga kisawasawa maana tunakuwa tumeikimbia neema ya Mungu inayotulinda dhidi ya mwovu. Basi na tujinyenyekeza mbele za Mungu ili neema yake ijidhihirishe katika maisha yetu nasi tutafanikiwa zaidi.

Injili kama ilivyoandikwa na Marko (6:1-16); inatueleza kuwa watu wa Nazareti walishindwa kusadiki kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu sababu alizaliwa kwao, akaishi nao kama mtu wa kawaida. Kama Ezekieli aliyetumwa kwa hao ndugu zake mwenyewe nao wakamkataa (Eze.3:6), ndivyo ilivyokuwa kwa Yesu kudharauliwa na watu wa nyumbani kwake. Na sababu ya kudharauliwa kwa Yesu si nyingine bali ni kufahamika kwake na familia yake na jamaa yake yote ndiyo maana wanasema kuwa ni mwana wa seremala na wanawataja waziwazi ndugu zake na wazazi wake. Tukitaka kusadiki na kuelewa ufunuo wa Mungu lazima tuwe wanyenyekevu kupokea neema ya Mungu inayoletwa katika mambo madogo madogo ya kimwili.

Mungu anaendelea kututumia wajumbe wake; Maaskofu, Mapadre, watawa, Makatekista, Viongozi wa jumuiya na vyama vya kitume, wengine ni wanafamilia ili watuambie tunayopaswa kutenda kwa wokovu wetu. Sio ajabu kwa kuwa tunawafahamu walikotoka, familia zao, wazazi wao na hata hali zao tumewazoea kama waswahili wanavyosema; “Mazoea huleta dharau na mazoea yana taabu” kwa hali hiyo tukawadharau na kushindwa kuupokea ujumbe wa Mungu. Mtume Paulo anatukumbusha kuwa Mungu anavichagua vilivyodhaifu ili aviaibishe vyenye nguvu. Hii ni faraja kwa wanaoitwa na kutumwa na Mungu msiogope maana Yesu anatuambia; “Heri yenu ninyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila neno baya kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni.” Basi na tujinyenyekeshe mbele za Mungu, tusifanye migumu mioyo yetu, tusiwe watu wa shingo ngumu wasioelezeke, wakaidi na waasi bali tuweni wanyenyekevu tuisikie sauti ya Mungu inayotujia kwa njia ya wale anaowachagua ili tupate wokovu wa milele.

J14 ya Mwaka B
01 July 2021, 17:57