Tafuta

Wafuasi wa Kristo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani sanjari na huduma ya upendo! Wafuasi wa Kristo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani sanjari na huduma ya upendo! 

Tafakari Jumapili 15: Toba, Wongofu na Huduma ya Upendo!

Mwenyezi Mungu anaita na kutuma watu kuhubiri Habari Njema ya wokovu. Zaweza kuwepo changamoto mbalimbali katika kutekeleza kazi hiyo lakini hizo haziwezi kuizuia kazi ya Mungu kusonga mbele. Aidha, tunaweza kujitazama na kuona kuwa hatustahili kwa kazi ya Mungu, lakini tunakumbushwa kwamba ni Mungu ndiye anayetustahilisha na kututegemeza kwa neema yake.

Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.

UTANGULIZI Ndugu msikilizaji wa Radio Vatikani karibu katika tafakari ya Liturjuia ya Neno la Mungu katika Dominika ya 15 ya mwaka B wa Kanisa. Masomo ya Dominika hii yanafanya mwendelezo wa dhamira ambayo tuliisikia Dominika iliyopita ya kwamba Mungu anaita na kutuma watu kuhubiri Habari Njema ya wokovu. Zaweza kuwepo changamoto mbalimbali katika kutekeleza kazi hiyo lakini hizo haziwezi kuizuia kazi ya Mungu kusonga mbele. Aidha, tunaweza kujitazama na kuona kuwa hatustahili kwa kazi ya Mungu, lakini tunakumbushwa kwamba ni Mungu ndiye anayetustahilisha na kututegemeza kwa neema yake. Tu watendakazi pamoja na Mungu katika kujenga ufalme wake.

TAFAKARI: Katika somo la kwanza tunasikia kidogo kuhusu wito wa nabii ya Amosi, mtu kutoka kusini, aliyefanya kazi ya kuchunga mifugo na kulima mikuyu. Amosi hakujua habari yoyote ya kuwa nabii maana halikuwa jambo ambalo alijifunza bali ulikuwa ni wito aliopokea kutoka kwa Mungu. Hakuwa na mafunzo yoyote yale kwa kazi hii bali neema ya Mungu iliyomstahilisha na kumuwezesha kufanya kazi hii. Na pamoja na kwamba Amosi hapokelewi vizuri upande wa kaskazini ambapo alikuwa akifanya kazi yake ya unabii bado anadumu katika kazi yake akijua kwamba hakujiita mwenyewe bali ni wito kutoka kwa Mungu. Mungu ndiye anayeita na kutuma watu kufanya kazi yake na wote wanaohubiri wanahubiri kwa jina la Mungu. Katika somo la pili Mtume Paulo anatoa shukrani na baraka akimsifu Mungu kwa yale yote aliyolijalia Kanisa lake.

Mtume Paulo anakazia ukweli kwamba sisi ni chaguo la Mungu mwenyewe kwa njia ya Kristo Yesu ambaye ametukomboa kwa kumwaga damu yake. Sisi ni wana wa Mungu na ni mali yake. Mungu ametuita kwake kwa sababu anatupenda. Na hata kama tutapitia magumu na changamoto nyingi hatuna sababu ya kuogopa kitu maana sisi ni mali yake na ametuchagua kabla hata ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu ili tupate kuwa watakatifu na bila doa mbele yake katika upendo. Katika Injili tunasikia mitume walioitwa na Yesu sasa wanatumwa kwa mamlaka ya Mungu kwenda kuhubiri na kupunga pepo wachafu. Kama ilivyokuwa kwa Amosi na Paulo ndivyo ilivyo kwa mitume hawa. Hawakujituma wenyewe bali wanapokea utume na mamlaka kutoka kwa Yesu. Ujumbe ni ule ule ya kwamba anayeita na kutuma ni Mungu mwenyewe. Zaidi ya hayo Yesu anawaelekeza kuwa wasitegemee sana vitu katika utume wao bali waongoze na utayari, moyo wa shukrani na bidii katika kazi waliyotumwa kuifanya.

KATIKA MAISHA: Katika Dominika hii sisi sote tunatiwa moyo ya kwamba sisi ni chaguo la Mungu na tumeitwa kuwa watenda kazi pamoja nao; tumeitwa kutangaza habari njema ya ufalme wa Mungu, si kadiri tunavyopenda sisi bali kadiri anavyotutaka Mungu kufanya. Kila Mkristo ana wajibu wa kuhubiri Injili pale alipo na kwa namna yake ya maisha. Kila mmoja ni mtenda kazi pamoja na Mungu. Lazima tuwe na vipaumbele katika utume wetu. Kama vile ilivyokuwa kwa mitume ndivyo inavyopaswa kuwa kwetu. Yesu anawasisitiza wajielekeze zaidi katika mambo ya utume na si katika kujikusanyia vitu. Anawataka pia wawe na moyo wa shukrani. Sisi nasi tunapaswa kukumbuka kuwa tumeitwa kuwa watakatifu. Yanaweza kuwepo mengi ambayo tunatamani kuyapata lakini tukumbuke kwanza utakatifu. Huo ndio unaotuunganisha na Mungu aliyetuita kwa kusudi lake. Utakatifu ndio wapaswa kuwa dira yetu katika yote tunayofanya.

Zaidi ya hayo, tuwe faraja kwa wengine tunapoifanya kazi ya Mungu. Mitume walitumwa wakahubiri Injili, wakatoa pepo wengi na kuponya wagonjwa. Yote haya waliyoyafanya yalikuwa ni sehemu ya faraja kwa watu na sababu ya kuleta tumaini kwa wengine. Tuombe neema ya Mungu ili kuishi kwetu kikristo kuwe chachu ya amani na matumaini kwa wale wote tunaokutana nao. Nakutakia Dominika Njema na Mungu akubariki.

Liturujia J15
09 July 2021, 16:07