Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani 2021: Maaskofu Katoliki Malawi!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani Jumapili tarehe 25 Julai 2021, unanogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria ambayo inaadhimishwa Jumatatu tarehe 26 Julai 2021. Baba Mtakatifu anawataka mababu, mabibi na wazee kujikita katika nguzo kuu tatu za maisha: Ndoto, Kumbukumbu na Sala kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kwa waja wake. “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono” Yoe 2: 28-32. Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani ni matunda yanayobubujika kutoka katika Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” uliozinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na utahitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”.
Ndoto, Kumbukumbu na Sala ni kielelezo cha uwepo endelevu na fungamani wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake. Wazee wawe ni wadau katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika maisha na utume wa Kanisa. Wasaidiwe kukuza na kudumisha tasaufi ya maisha ya kiroho, wahusishwe kikamilifu na uwepo wao uthaminiwe na Kanisa liwe tayari kuchota hekima na busara kutoka kwa wazee hawa. Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi katika maadhimisho haya linasema, wazee wana mang’amuzi, ujuzi, maarifa na uzoefu wa miaka mingi, walisaidie Kanisa kupambana na changamoto mamboleo katika maisha na utume wake! Kwa hakika wazee ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Wazee ni watu muhimu sana katika historia ya binadamu changamoto na mwaliko wa, kushirikishana, kushikamana na kufungamana na wazee kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama Kristo Yesu anavyofungamana na waja wake katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Sadaka na matoleo yote yaliyopatikana, Jumapili tarehe 25 Julai 2021 yatatumika kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na wazee nchini Malawi. Waamini wanahimizwa kujenga utamaduni wa kuwalinda, kuwasaidia na kuwatunza wazee na wagonjwa katika familia na jumuiya zao na kwa njia hii, wanajipatia neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu anayejitambulisha kuwa ni sehemu ya watu hawa. Maadhimisho yote haya yanalenga kumwilisha imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Familia ya Mungu nchini Malawi, licha ya shida, magumu, changamoto na fursa mbalimbali za maisha, wanapaswa kuwa ni watu wa shukrani, kwa kuwasaidia wahitaji zaidi katika familia na jamii katika ujumla wake. Wazee, wagonjwa na maskini, wasaidiwe kwa hali na mali, ili waweze kufurahia mwisho mwema wa uzee wao, kwa kuwa na maisha yanayosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Vijana wa kizazi kipya wanahamasishwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na wazee kwani wazee wana ndoto na vijana wana unabii. Vijana wanapaswa kutekeleza ndoto ya wazee. Hii ni ndoto inayosimikwa katika misingi ya: haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mwelekeo huu unawawezesha vijana wa kizazi kipya kuwa na dira ili kwa pamoja kuweza kujenga ulimwengu ujao, kwa kuunganisha uzoefu, mang’amuzi na magumu ya maisha. Wadau mbalimbali wanapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya kijamii kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, ili dunia iweze kusimama katika misingi ya haki, amani; utu, heshima na mshikamano wa udugu wa kibinadamu!