Tafuta

Shirika la Wazee na Wastaafu Wakatoliki Tanzania: Risala ya Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Wazee na Wajukuu: Changamoto za wazee Barani Afrika. Shirika la Wazee na Wastaafu Wakatoliki Tanzania: Risala ya Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Wazee na Wajukuu: Changamoto za wazee Barani Afrika. 

Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani 2021: Wazee na Wastaafu Tanzania

Shirika la Wazee na Wastaafu Wakatoliki Tanzania katika risala yao linataja baadhi ya changamoto zinazowakabili wazee nchini Tanzania: Wazee wengi wanakabiliwa na umaskini wa hali na kipato vijijini na mijini. Wengi wao wanakumbana na changamoto ya magonjwa ya wazee. Hata baada ya kuanzishwa kwa Bima ya Afya kisheria, bado wazee wanakabiliwa na huduma hafifu ya afya.

Na Padre Gregory Mashtaki, Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania.

Shirika la Wazee na Wastaafu Wakatoliki Tanzania katika risala yao kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Wazee na Wajukuu Duniani wanasema, kwa hakika wazee ni hazina ya Kanisa, ni chemchemi ya furaha ya Injili na wadau katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 31 Januari 2021 alitangaza kwamba, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa siku ya Wazee na wajukuu itakuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila dominika ya nne ya mwezi Julai na kwa mwaka huu ni jumapili tarehe 25 Julai 202. Majimbo, Parokia na Vigango vyote nchini Tanzania, wazee na vijana wa kizazi kipya wanaunganishwa pamoja.  Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho haya unanogeshwa na kauli mbiu “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote hata ukamilifu wa dahari” Mt 28:20! Hii ni ahadi ya Yesu Kristo kwa waja wake. Mwaliko kwa Vijana wa kizazi kipya na Wazee ni kushirikishana na kushikamana kwa pamoja ili hatimaye, kuwa ni wadau wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Uzee ni zawadi na kiungo kati ya vizazi na yenye kurithisha kwa vijana uzoefu wa maisha na imani. Waamini wajiandae kikamilifu. “Roho Mtakatifu angalia na amsha leo mawazo na maneno ya hekima ya Wazee kwani sauti yao ni ya thamani kwa sababu inaimba sifa za Mungu na kulinda maadili ya vizazi vya binadamu”. Vijana wanahamasishwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kujikita katika maisha ya sala, tayari kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wazee wanaweza kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kutekeleza dhamana hii kwa ari na moyo mkuu. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, linawaalika waamini wote kwa adhimisho hili ili kukoleza moyo wa uinjilishaji kwa kutambua kwamba, Wazee wana ndoto na vijana wana unabii (Yoeli 2:28) kama ambavyo anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Katika kipindi hiki ambacho mahusiano na mafungamano ya kifamilia yanalegalega, Siku ya Wazee Duniani inakuwa ni fursa ya kuboresha mahusiano kati ya kizazi kipya kwa kujenga na kudumisha upendo kati ya vijana wa kizazi kipya pamoja na Wazee. 

Wazee ni: “amana na utajiri wa jamii”; wao ni: “watunzaji wa mapokeo hai na wanayo misingi ya jamii”; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana uzoefu na mang’amuzi ya maisha. Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi Wazee wanasahauliwa sana kushirikishwa katika maendeleo ya jamii. Shirika la Wazee na Wastaafu Wakatoliki Tanzania katika risala yao linataja baadhi ya changamoto zinazowakabili wazee nchini Tanzania: Wazee wengi wanakabiliwa na umaskini wa hali na kipato vijijini na mijini. Wazee katika umri wao, wengi wao wanakumbana na changamoto ya magonjwa ya wazee. Hata baada ya kuanzishwa kwa Bima ya Afya kisheria kupitia Kanisa, Serikali za Vijiji na Mitaa, bado wazee wanakabiliwa na huduma hafifu ya afya. Kuna haja kwa wanawake vikongwe kupatiwa ulinzi stahiki kisheria ili kuwalinda dhidi ya nyanyaso za kijinsia, ubakaji, mauaji ya kikatili kwa kisingizio cha imani za kishirikina. Wasiokuwa na msaada, Serikali na wadau mbalimbali waangalie jinsi ya kuwasaidia wale wasiokuwa na makazi, tiba na msaada wa mahitaji msingi.

Kuna wazee ambao wana uzoefu, taaluma na weledi, rasilimali watu ambayo inapotea bure bila hata ya kutumiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Jamii na Kanisa katika ujumla wake. Kumbe, wazee wanapaswa kushirikishwa ili kutoa maoni yao katika mchakato mzima wa maendeleo fungamani ya binadamu kiroho na kimwili. Kuna haja kwa wazee kupata Bima ya afya, ili kuweza kuwapatia nafuu katika mapambano ya maisha yao ya uzeeni. Baba Mtakatifu Francisko, anawaalika wazazi na walezi watambue kwamba, wao ni wadau wa kwanza wanaoshirikiana na Mwenyezi Mungu katika kazi ya uumbaji, malezi na makuzi ya watoto na vijana wao. Tuone familia kama “shule ya upendo, imani na utakatifu wa maisha”. Siku hii ni muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya jamii ili kuwashukuru, kuwaenzi na kuwabariki wazee kutokana na mchango wao katika ustawi, mafao na maendeleo ya watu wa Mungu katika medani mbalimbali za maisha. Hii pia ni fursa ya kukuza na kudumisha ndani ya nyoyo za watu: “faraja, upendo, huruma, imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu”.

Wazazi na walezi kwa kushirikiana na wazee, warithishe imani hii kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kutambua na kuenzi kweli msingi za maisha kadiri ya upendo na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.  Watoto wasaidiwe kupata mwanga na ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yao. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, wazazi wawasaidie vijana na watoto wao kutambua na kuthamini zawadi ya maisha inayopaswa kulindwa na kutunzwa tangu pale mtoto anapotungwa mimi tumboni mwa mama yake hadi uzee stahiki. Wazee ni sehemu muhimu sana kwa jamii yoyote ile. Uzoefu na busara za wazee ni kiungo na hamasa kwa maisha ya wanajamii. Pamoja na changamoto mbalimbali za maisha ya uzeeni bado Wazee wana nafasi na mchango mkubwa kwa ustawi wa jamii. Wazee ni alama ya utimilifu wa maisha ya mtu na jamii katika ujumla wake. Wazee ni walezi kwa watoto na vijana. Wazee ni: urithi, amana na utajiri kwa jamii kwani uzoefu na busara zao ni ushuhuda wa kinabii kwa siku hizi.

Kanisa linasifu heshima inayotolewa na familia ya Mungu Barani Afrika kwa wazee wao, kwani wao ni utajiri, hawatengwi wala kudharauliwa bali, wanabaki kama miamba na walezi wakuu wa mila, desturi na tamaduni njema katika jamii. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujifunza namna ya kuheshimu na kuwathamini Wazee kutoka Afrika. Uzee, umaskini na magonjwa visiwe ni sababu ya kuwatenga na kuwakosea heshima Wazee katika jamii. Jamii kwa ujumla itambue kuwa Wazee ni msingi wa uhai na maendeleo fungamani ya binadamu ili kufikiri na kutenda kiutu, kwa huruma na upendo, mambo yote yanahusiana na kukamilishana. Tujifunze kuenzi, kuheshimu na kuthamini tamaduni zetu. Hii ni changamoto muhimu sana kwa vijana wa kizazi kipya kupyaisha misingi ya tamaduni zao, kama sehemu muhimu sana ya utambulisho wao. Vijana wa kizazi kipya wajenge na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi na Wazee. Wazazi wajenge utamaduni wa kuzungumza na watoto pamoja na wajukuu wao. Ni vema utaratibu stahiki ukawekwa sasa kwa mikutano hiyo ya Wazee na Vijana.

Ni wakati pia kwa Wazee ambao hawajajiunga na Shirika la Wazee na Wastaafu Wakatoliki Tanzania wakaungana kwa sala na washirika mahalia. Paroko mahalia ataratibu hili kwa ushirikiano na Wazee. Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Wazee wana maono ya kinabii wakati vijana wana ndoto za maisha”. Ushuhuda ni mahali ambapo waamini wanaweza kugundua mpango wa Mungu katika maisha yao na haya ndiyo mazingira ya kibinadamu! Vijana na Wazee wanategemeana na kukamilishana katika hija ya maisha yao ya kila siku. Siku ya Wazee duniani ni mwendelezo wa sera na mikakati ya kichungaji iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu: uhai, utu, heshima na haki msingi za binadamu.  Ni fursa ya Wazee na Vijana kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja, mshikamano na undugu unaovunja kuta za utengano kati ya watoto wa Mungu. Tumwombe Mungu adumishe umoja huu wa ki-ekumene akitufunulia akili zetu tuelewe umuhimu wa kuwaenzi Wazee na kudumisha malezi mema kwa Vijana na watoto wetu. Risala hii imeandaliwa na Padre Gregory Mashtaki, Mwanzilishi na Mlezi wa Shirika la Wazee na Wastaafu Wakatoliki Tanzania.

Wazee wa Tanzania

 

24 July 2021, 15:24