Tafuta

Mkutano wa 77 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote Mkutano wa 77 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote 

Maaskofu Katoliki Tanzania: Mkutano Mkuu Wa 77: Mazingira

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Mkutano wake wa 77 uliofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 25 Juni 2021 pamoja na mambo mengine, umejadili Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Walitembelewa na kuzungumza na Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika ujumbe wake kwa njia ya video kama sehemu ya kumbukizi la Miaka Mitano tangu alipochapisha Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” sanjari na uzinduzi wa Jukwaa la Kazi “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, alipenda kukazia yafuatayo: Kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha Maskini, Utunzaji bora wa mazingira na Jukwaa la kazi ili kutekeleza sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote katika kipindi cha miaka saba kuanzia sasa! Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2015 aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujizatiti katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema rasilimali na utajiri wa dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Leo hii kuna uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote.

Janga kubwa la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni changamoto ya kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini. Kuna mwingiliano mkubwa kati ya afya bora na mazingira anamoishi binadamu. Hapa kuna haja ya kujikita katika wongofu wa kiikolojia kwa kubadili mtindo wa maisha kwa ajili ya ikolojia ya binadamu, tayari kujikita katika ujenzi wa jamii mpya! Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa inao wajibu mkubwa kwa vizazi vijavyo, kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko wa kuondokana na ubinafsi unaopelekea matumizi mabaya ya rasilimali na mali ya dunia. Ni wakati wa kujenga utamaduni wa kuheshimu zawadi ya kazi ya uumbaji, kwa kuwa na mtindo mpya wa maisha, unaothamini wongofu wa kiikolojia ili kuwaandalia vijana leo na kesho bora zaidi, na hatimaye, kuwaachia bustani inayostawi na wala si jangwa linalotisha na kukatisha tamaa!

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Mkutano wake wa 77 uliofanyika Jimbo kuu la Dar Es Salaam kuanzia tarehe 21 hadi 25 Juni 2021 pamoja na mambo mengine, umejadili na kupembua Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Walipata nafasi ya kutembelewa na kuzungumza na Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais alipata kusikia kwa ufupi historia na mchango wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hasa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilibainisha: matatizo, changamoto na fursa katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu; mambo yaliyobainishwa katika hotuba iliyosomwa na Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Maaskofu pia wamekamilisha uteuzi wa viongozi wakuu wa tendaji wa Baraza katika kipindi cha miaka mitatu yaani Mwaka 2021 hadi mwaka 2024 kama ifuatavyo: Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga ataendelea kuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita amechaguliwa kuwa ni Makamu wa Rais. Padre Charles Kitima ataendelea kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kipindi kingine cha miaka mitatu. Maaskofu Katoliki Tanzania wamemteuwa Padre Chesco Peter Msaga, C.PP.S., kuwa Naibu Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Padre Chesco Peter Msaga alikuwa ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania litakuwa ni Mwenyeji wa Mkutano wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, utakaoadhimishwa mwezi Julai, Mwaka 2022. Mkutano huu utajikita zaidi katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, linatekelezwa katika kipindi cha miaka saba. Mwaka wa kwanza ni mchakato wa ujenzi wa jumuiya, ushirikishanaji wa rasilimali na utengenezaji wa sera na mikakati ya utekelezaji kadiri ya mwono wa ikolojia fungamani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kujielekeza katika uchumi unaosimikwa katika ikolojia; kwa kujikita katika mtindo wa maisha ya kawaida sanjari na kuendelea kukazia elimu na tasaufi ya ikolojia pamoja na ushirikishwaji wa jumuiya! Mwaka wa Saba, utatumika kumsifu na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Kazi ya Uumbaji.

Kanisa Katoliki nchini Tanzania lingependa kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na utunzaji bora wa mazingira, kwa kuachana na tabia ya kukata miti ovyo na kuanza kujielekeza katika utamaduni wa kupanda na kutunza miti sanjari na hifadhi bora ya taka ambazo mara nyingi zimekuwa ni chanzo cha magonjwa ya milipuko. Wajumbe wamewataka watanzania kuthamini utakatifu wa kazi ya uumbaji, ili kuweza kutumia amana, utajiri na rasilimali za dunia kwa uwajibikaji mkubwa na shirikishi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Elimu ya ikolojia haina budi kutolewa kwa vijana wa kizazi kipya, ili tangu mwanzo, waweze kuanza kujifunza kutunza mazingira kwa mafao ya wengi. Wamekazia umuhimu wa kujikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Ni wakati wa kukazia kanuni maadili na utu wema kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Wongofu wa kiikolojia uwasaidie watanzania kukuza na kudumisha utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira katika ujumla wake; kwa kuachana pia na ukatili dhidi ya wanyama. Vyombo vya mawasiliano ya jamii viendelee kujikita katika wongofu wa kiikolojia, uwajibikaji wa kimaadili na utu wema; ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kuwajali na kuwathamini maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa ni amana na utajiri wa Kanisa. Maskini ndio waathirika wakubwa wa uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote, kiasi kwamba, kila kukicha wanaendelea kudidimizwa kwenye umaskini wa hali na kipato! Mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni dhamana inayowahusu watanzania wote katika ujumla wao. Kumbe, kuna haja ya kuwa na sera bora za mazingira zinazotekelezeka. Familia ya Mungu nchini Tanzania ijitahidi kujenga na kudumisha mifumo na taasisi zitakazosimama kidete katika kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira kwa mafao ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania

 

 

 

04 July 2021, 15:58