Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB limechangia kiasi cha dola za kimarekani milioni 1.36 kwa ajili ya kugharimia miradi Barani Afrika Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB limechangia kiasi cha dola za kimarekani milioni 1.36 kwa ajili ya kugharimia miradi Barani Afrika 

Maaskofu Katoliki Marekani Wachangia Milioni 1.36 Kwa Afrika

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani limepitisha kiasi cha dola za Kimarekani milioni 1.36 ili kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo fungamani ya binadamu Barani Afrika. Hiki ni kielekezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kati ya Bara la Afrika na Marekani katika ujumla wake. Huu ni ushuhuda wa upendo na mshikamano wa dhati kati ya Marekani na Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, hivi karibuni limepitisha kiasi cha dola za Kimarekani milioni 1.36 ili kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo fungamani ya binadamu Barani Afrika. Hiki ni kielekezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kati ya Bara la Afrika na Marekani katika ujumla wake. Bara la Afrika licha umaskini, magonjwa, njaa na vita, bado linaendelea kuwa ni nguzo ya matumaini ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Mabaraza 27 ya Maaskofu Katoliki Afrika, Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yatapokea kiasi hiki cha fedha kwa ajili ya kugharimia shughuli za kichungaji, maendeleo fungamani ya binadamu na mafunzo ya uongozi bora. Kimsingi fedha hii inapania kusaidia kugharimia mchakato wa uinjilishaji wa kina Barani Afrika unaozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Fedha hizi ni kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya Kanisa Barani Afrika. Huu ni mchango unaotolewa na waamini wa Kanisa Katoliki nchini Marekani.

Katika hotuba yake, Kardinali Joseph W. Tobin, Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani inayoshughulikia Bara la Afrika, anasema, hiki ni kiasi kidogo sana cha fedha kilichotolewa ikilinganishwa na mahitaji msingi Barani Afrika. Hata hivyo, fedha hii inaweza kutenda maajabu na kusaidia kunogesha mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hiki ni kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kutoka kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini Marekani. Anasema, haba na haba hujaza kibaba na hivyo kuchochea mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Miradi 56 iliyobainishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, inapania kuwajengea watu wa Mungu Barani Afrika uwezo katika mikakati na shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa Barani Afrika. Miradi inayotekelezwa ni pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote nchini Zambia. Fedha itawasaidia waathirika wa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 nchini Zimbabwe sanjari na uinjilishaji nchini Togo.

Huduma makini kwa ajili ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, itatolewa kwa watu hawa nchini Uganda. Fedha hi inchini Malawi itasaidia kunogesha Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu uliozinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na unatarajiwa kufungwa kwa kishindo hapo tarehe 8 Desemba 2021. Kwa upande wa Burundi msaada huu ni kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa nyanyaso za kijinsi wakati ambapo nchini Cameroon, lengo ni kwa ajili ya kuboresha huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum nchini humo. Bara la Afrika linaendelea kuonesha ari na mwamko katika maisha na utume wake, hususan katika ongezeko la waamini wanaohitaji sasa kusogezewa na hatimaye kupatiwa huduma bora zaidi: kiroho na kimwili. Jambo la msingi kwa waamini Barani Afrika ni kuanza kujifunga kibwebwe ili kulitegemeza Kanisa kwa hali na mali na kwamba, misaada kutoka nje ya Bara la Afrika, isaidie kuongezea juhudi za kulitegemeza Kanisa kwa rasilimali watu, viti na fedha kama kielelezo makini cha ukomavu wa Kanisa mahalia!

Miradi Afrika

 

01 July 2021, 16:09