Tafuta

Afrika ya Kusini imekumbwa na machafuko ya kisiasa na watu zaidi 72 wamefariki dunia na wengine 1, 200 wametiwa mbarano. Maaskofu Katoliki washutumu vurugu hizi. Afrika ya Kusini imekumbwa na machafuko ya kisiasa na watu zaidi 72 wamefariki dunia na wengine 1, 200 wametiwa mbarano. Maaskofu Katoliki washutumu vurugu hizi. 

Afrika ya Kusini Yakumbwa na Machafuko ya Kisiasa! Hali Ni Tete!

Afrika ya Kusini imekumbwa na machafuko makubwa ya kisiasa na watu zaidi ya 72 wamekwisha kupoteza maisha na wengine 1, 200 wamepigwa pingu kwa makosa ya: mauaji, vurugu na kupora mali za watu. Maandamano makubwa yalianza siku kadhaa zilizopita baada ya Rais wa zamani Jacob Zuma kuanza kutumikia kifungo chake cha miezi 15 jela. Kanisa linashutumu vitendo hivi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ujasiri unaleta amani ya kweli, unatafuta na kudumisha ustawi na maendeleo ya wengi. Vita imeharibu sana makazi ya watu, imewatumbukiza wananchi katika baa la njaa, ujinga na maradhi. Vita imewakosesha watu nyumba za sala na ibada; imepelekea watu kukosa fursa za ajira na kwamba, kuna umati mkubwa wa wananchi waliolazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Mchakato wa kutafuta amani ya kudumu ni endelevu na unajikita katika ukweli na uwazi; ujasiri na unyenyekevu pasi na baadhi ya watu kutaka kujikweza na kujimwambafai zaidi. Ni mchakato unaofumbatwa katika ushupavu ili kukuza na kudumisha amani, upatanisho na umoja wa Kitaifa, kwani vita inaleta maafa kwa watu na mali zao. Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowawajibisha hasa wale ambao wamepewa dhamana ya uongozi ili kuhakikisha kwamba wanalinda: utu na heshima ya ndugu zao ili hata wao pia wajisikie kuwa ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa maendeleo fungamani kwa mustakabali wa nchi yao. Ili kudumisha amani ya kweli, kuna haja ya kujenga mazingira ya haki na usawa ili kuondokana na vurugu na migongano inayoweza kupelekea jamii kulipuka kwa vita na misigano ya kijamii.

Kukosekana kwa usawa kutawafanya wale waliotengwa kujibu “mapigo” kwa ghasia. Ikumbukwe kwamba, utamaduni wa amani ni mchakato endelevu unaopaswa kuwashirikisha hata vijana wa kizazi kipya; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja. Kumbe, utulivu ni hitaji muhimu, ili kuweza kufikia malengo yaliyobainishwa, nguvu msingi za maisha na mawazo yanayofyekelea mbali ile tabia ya kudhaniana vibaya. Utajiri mkubwa uliopo unapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kuhakikisha kwamba, wanapata elimu makini, makazi bora zaidi pamoja na fursa za ajira. Sanjari na haya, wakulima wawe na mashamba kwa ajili ya shughuli za kilimo. Huu ni msingi wa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi na silaha madhubuti ya amani ya kudumu! Wananchi wote wanapaswa kuwa ni wasanii katika ujenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Septemba 2019 kwa viongozi wa Serikali, wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia nchini Msumbiji.

Afrika ya Kusini imekumbwa na machafuzo makubwa ya kisiasa na watu zaidi ya 72 wamekwisha kupoteza maisha na wengine 1, 200 wamepigwa pingu kwa makosa ya: mauaji, vurugu na kupora mali za watu wengine. Maandamano makubwa yalianza siku kadhaa zilizopita baada ya Rais wa zamani Jacob Zuma kuanza kutumikia kifungo chake cha miezi 15 jela. Zuma alihukumiwa kwa kukaidi agizo la Mahakama, la kumtaka afike mahakamani hapo kujibu shutuma za kesi ya rushwa dhidi yake. Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, “Southern African Bishops’ Conference, SABC” katika tamko lake mintarafu machafuko ya kisiasa nchini Afrika ya Kusini lina laani vitendo vyote vya vurugu na uvunjifu wa amani ambao umepelekea watu kadhaa kupoteza maisha yao. Huu ni wakati wa kuanza kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi ili kujenga na kuimarisha umoja wa Kitaifa.

Machafuko ya kisiasa yanayoendelea ni hatari sana kwa maisha ya wananchi wengi wa Afrika ya Kusini. Bado janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 linaendelea kupukutisha maisha ya wananchi wengi, hali ambayo inatishia maisha, fursa za ajira na ukuaji wa uchumi. Ili kujenga na kuimarisha demokrasia, kuna haja kwa wananchi wa Afrika ya Kusini kujikita katika utawala wa sheria, majadiliano katika ukweli na uwazi. Ukosefu wa haki na usawa, kiwango kikubwa cha umaskini na madhara ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni kati ya mambo yanayoendelea kuchochea vurughu Afrika ya Kusini. Wananchi wanahitaji huduma na wananchi wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa uchumi nchini Afrika ya Kusini.

Afrika ya Kusini Vurugu
15 July 2021, 16:20