Tafuta

Askofu Simo Chibuga Masondole kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi tarehe 4 Julai 2021. Askofu Simo Chibuga Masondole kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi tarehe 4 Julai 2021. 

Askofu Simon C. Masondole Jimbo Katoliki la Bunda! Kumenoga!

Tarehe 4 Julai 2021 Askofu mteule Simon Chibuga Masondole atawekwa wakfu na kukabidhiwa Jimbo Katoliki la Bunda, ili kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu. Tukio hili muhimu linatanguliwa na Mapokezi mazito kwa Askofu mteule pamoja na ugeni kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Bunda. Jumamosi tarehe 3 Julai 2021 kwenye Parokia ya Chamgasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Jimbo Katoliki la Bunda nchini Tanzania lilianzishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI kunako tarehe 27 Novemba 2010 ili kusogeza zaidi huduma za kichungaji kwa watu wa Mungu jimboni humo. Jimbo hili lilimegwa kutoka Jimbo kuu la Mwanza na Jimbo Katoliki la Musoma. Jimbo Katoliki la Bunda ni kati ya majimbo 34 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Jimbo Katoliki la Bunda lina Parokia 22 kwa sasa zinazohudumiwa na Mapadre 48. Kati yao kuna Mapadre wa Jimbo 31, Mapadre wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni 10 na Mapadre wa “Fidei Donum” ni 7. Jimbo la Bunda lina jeshi kubwa la Makatekista wapatao 256 Baba Mtakatifu Francisko tarehe 6 Aprili 2021 alimteuwa Mheshimiwa sana Padre Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki la Bunda, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bunda, Tanzania, kuchukua nafasi iliyoachwa na Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Nkwande ndiye muasisi wa Jimbo Katoliki la Bunda, ambaye alibahatika kuliongoza tangu tarehe 27 Novemba 2010 hadi tarehe 11 Februari 2019 alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza. Tarehe 4 Julai 2021 Askofu mteule Simon Chibuga Masondole atawekwa wakfu na kukabidhiwa Jimbo Katoliki la Bunda, ili kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu. Tukio hili muhimu linatanguliwa na Mapokezi mazito kwa Askofu mteule pamoja na ugeni kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Bunda. Haya ni mapokezi ya kukata na shoka yatakayofanyika Jumamosi tarehe 3 Julai 2021 kwenye mpaka wa Jimbo Katoliki la Bunda na Shinyanga, yaani kwenye Parokia ya Chamgasa inayopakana na Parokia Mama ya Kanisa kuu la Jimbo la Bunda. Jioni, Askofu mteule atakabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo Mtume na baadaye kutafanyika masifu ya jioni. Katika Ibada hii, Askofu mteule atakiri Kanuni ya Imani na Kula Kiapo cha Utii na Uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Historia inaonesha kwamba, Askofu mteule Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki Bunda, alizaliwa tarehe 2 Oktoba 1972 huko Bukiko, Kisiwani Ukerewe. Kunako Mwaka 1998 alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi, kwa ajili ya masomo ya Falsafa na kuhitimu masomo yake mwaka 2001. Baadaye mwaka 2001 aliendelea na masomo ya Taalimungu Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 2006. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, tarehe 2 Julai 2006 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Mwanza. Tangu wakati huo kama Padre, amewahi kuwa Paroko-usu Parokia ya Kahangara, Jimbo kuu la Mwanza, Mkurugenzi Msaidizi wa Kamati ya Liturujia Jimbo kuu la Mwanza na baadaye kati ya Mwaka 2006 hadi mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Paroko-usu kwenye Parokia ya Nansio-Ukerewe, Jimbo Katoliki la Bunda.

Baadaye kunako mwaka 2008 alitumwa na Jimbo Katoliki la Bunda kujiendeleza zaidi katika masomo ya Liturujia ya Kanisa kwenye Taasisi ya Shughuli za Kichungaji Kiliturujia ya “Santa Giustina”, Jimbo Katoliki la Padua, nchini Italia. Baada ya kupata msingi wa Liturujia, alijiendeleza zaidi kwenye Taasisi ya Kipapa ya Liturujia, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselmi kilichoko mjini Roma ambako alijipatia Shahada ya Uzamivu katika Liturujia ya Kanisa kunako mwaka 2016. Kati ya mwaka 2015 hadi mwaka 2018 alitoa huduma ya kichungaji Jimboni Tortona, Italia. Na kunako mwaka 2018 alirejea tena kwa shughuli za kichungaji, Jimbo Katoliki la Bunda, hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bunda amekuwa akifundisha Liturujia ya Kanisa na mlezi, Seminari kuu ya Segerea.

Bunda Kumenoga

 

02 July 2021, 16:34