Tafuta

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam: Ukweli mzito ni kuhusu mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache! Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam: Ukweli mzito ni kuhusu mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache! 

Ukweli Mzito kwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Nchini Tanzania!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi aligusia kuhusu ukweli mzito kwamba, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Kumbe, waamini wanayo dhamana na wajibu wa kumwomba Bwana wa mavuno azidi kuwaita, kuwajenga na kuwatuma vijana: wema na watakatifu, wenye afya na utayari ili kujisadaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema! Yaani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Jimbo kuu la Dar es Salaam nchini Tanzania, tarehe 7 Julai 2021 limeandika ukurasa mpya katika historia, maisha na utume wake, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuwateuwa Maaskofu wasaidizi wawili kwa ajili ya Jimbo kuu la Dar es Salaam. Maaskofu wateule ni Stephano Musomba, wa Shirika la Waugustiani, OSA, hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mavurunza, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Mwingine ni Askofu msaidizi Henry Mchamungu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Jaalimu wa Sheria za Kanisa Seminari kuu ya Karol Lwanga, Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam na Rais wa Mahakama ya Kanisa na Katibu wa Tume ya Sheria za Kanisa, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Lakini kabla ya hapo, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam O.F.M. Cap. Alitoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 14. Kati yao 9 ni kwa ajili ya Jimbo kuu la Dar es Salam na 5 ni kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa nchini Tanzania.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi aligusia kuhusu ukweli mzito kwamba, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Kumbe, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanayo dhamana na wajibu wa kumwomba Bwana wa mavuno azidi kuwaita, kuwajenga na kuwatuma vijana: wema na watakatifu, wenye afya na utayari ili kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Familia ni chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Kumbe, wanafamilia wanapaswa kutambua kwamba, familia na watoto wao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanapaswa kuwapokea kwa mapendo watoto wanaopewa na Mwenyezi Mungu kama zawadi na kuwalea kama ilivyo sheria ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Wawajengee watoto wao msingi thabiti wa maisha; wawape uhuru wa kupembua na hatimaye, kufuata wito wanaotiwa na Mwenyezi Mungu. Ni wajibu wa familia ya Mungu kuwaombea Mapadre wote katika hali zao, ili waweze kuchota nguvu, furaha na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu asili ya wema wote, ili waweze kuimarika katika wito wao mtakatifu hadi mwisho.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, amewakumbusha Mapadre wapya kwamba, Jimbo kuu la Dar es Salaam limebahatika kuwa na Parokia 126, lakini bado kuna umati mkubwa wa watu wa Mungu ambao unahitaji uinjilishwaji wa awali. Mapadre wawe tayari kutumwa, kufanya kazi watakazopaswa kufanya; wawe ni mitume na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na Kanisa lake. Mapadre wakitaka kuwa na furaha, amani na utulivu wa ndani, wajibidiishe kushughulikia: Ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha na wito wa Kipadre na Kitawa. Watafute kutenda kazi ya Kristo Yesu na kulijenga Kanisa lake. Kamwe wasiwe wababe au makamanda jeuri. Mapadre waoneshe na kushuhudia katika maisha na utume wao Uso wa huruma ya Mungu na Kristo Yesu. Watekeleze dhamana na utume wao kwa upendo thabiti, huruma na furaha.

Mapadre wazingatie masharti ya utangazaji wa Habari Njema kama yanavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu. Katika maisha yao wajitahidi kumhubiri na kumshuhudia Kristo Yesu, kujenga na kuimarisha Ufalme wa Mungu hapa duniani. Wajitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao kwa kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza. Kamwe wasitegemee vitu na watu. Wasiwe ni watu kupenda kuchagua chagua. Wawe tayari kutumwa na kwenda popote kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, yaani mahali popote pale palipo na watu wa Mungu. Hakuna sababu ya kudhani kwamba, mtu kwa kupangiwa pembezoni mwa Jimbo ni dalili za kusetwa, kubaguliwa wala kudharirishwa, kwani watu wote, mahali walipo, wanahitaji kusikia Habari Njema ya Wokovu!

Ukweli Mzito
08 July 2021, 16:01