Tafuta

Askofu mkuu Gervas Nyaisonga tarehe 11 Julai 2021 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja takatifu ya Upadre. Askofu mkuu Gervas Nyaisonga tarehe 11 Julai 2021 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja takatifu ya Upadre. 

Askofu Mkuu Nyaisonga Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu Ya Upadre

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rasi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, tarehe 11 Julai 2021 akiwa ameungana na watu wa Mungu Parokia ya Mt. Patrick Vwawa, Jimbo kuu la Mbeya wamemwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa: maisha, wito na zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre! Mbeya Kumenoga!

Na Thompson Mpanji, Jiji la Mbeya, Tanzania.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre ni kipindi muafaka cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Huu ni muda wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza katika kupanda, kupalilia, kukuza na hatimaye kukomaa kwa mbegu ya Daraja Takatifu ya Upadre ambayo ni Daraja ya Uaskofu kama wanavyofundisha Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Askofu amekabidhiwa huduma ya Jumuiya pamoja na msaada wa Mapadre na Mashemasi kuongoza kwa niaba ya Mwenyezi Mungu, akiwa kama Mwalimu wa mafundisho matakatifu; kuhani wa ibada takatifu na mhudumu wa uongozi. Kumbe, Maaskofu, kwa namna bora na dhahiri, wanashika nafasi ya Kristo Yesu mwenyewe aliye Mwalimu, Mchungaji na Kuhani mkuu, na kutenda katika nafsi yake “In Eius persona.” Rej. LG 20- 28.

Daraja Takatifu ya Upadre inawawezesha Mapadre kupokea chapa ya Roho Mtakatifu ili kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Hapa ni mahali ambapo, imani inapyaishwa tena kadiri Padre anavyojiweka mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa toba na wongofu wa ndani, jambo ambalo linamwezesha kuzaa matunda ya ajabu katika maisha na utume wa Kanisa. Yote haya yanawezekana ikiwa kama Padre ana imani thabiti na anatambua kile anachopaswa kutenda na anakitenda kwa ari na moyo mkuu. Mapadre watambue kwamba, wao kimsingi ni watu wa imani, waliopewa dhamana ya kuwaimarisha ndugu zao katika Kristo ndani ya Kanisa kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Mapadre ni wahudumu wa Neno la Mungu Sakramenti za Kanisa na ni Mashuhuda wa huduma na Injili ya upendo.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, tarehe 11 Julai 2021 akiwa ameungana na watu wa Mungu Parokia ya Mtakatifu Patrick Vwawa, Jimbo kuu la Mbeya wamemwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wito na zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre aliyopewa na Hayati Askofu James Sangu wa Jimbo Katoliki la Mbeya, akiwa ni Shemasi wake wa mwisho kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, kabla ya kufikwa na mauti! Maadhimisho haya kijimbo yatafanyika tarehe 12 Septemba 2021, kwa kuwashirikisha Mapadre wengine kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, waliosoma na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre na Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kunako mwaka 1996.

Katika hali ya ugonjwa, huku Askofu James Sangu akiwa ameambatana na daktari wake binafsi, walifika Parokiani Vwawa tarehe 10 Julai 1996 na hatimaye akampatia Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 11 Julai 1996. Askofu mkuu Nyaisonga amewashukuru watu wote wa Mungu waliofika kujumuika pamoja naye, ili kumshukuru Mungu kwa wito na zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre. Amewashukuru wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza katika kupanda, kutunza, kupalilia na hatimaye kukomaa kwa mbegu ya wito huu. Anawashukuru wale wote wanaomsaidia kutekeleza vyema wito wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Anawaomba, waendelee kumsindikiza kwa sala na sadaka zao, ili aweze kutekeleza utume wake kikamilifu kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Katika mahubiri yaliyotolewa na Abate Pambo Martin Mkolwe, OSB wa Abasia ya Mvimwa, Jimbo Katoliki la Sumbawanga, amempongeza Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kwa kuwa ni mtu wa watu; kwa kujikita katika fadhila ya upole, huruma, unyenyekevu na upendo. Ni kiongozi anapenda kuona haki, amani na maridhiano yakitawala kati ya watu wa Mungu. Ni mchungaji mwema na hodari, anayejitahidi kuwakusanya watu wa Mungu ili kuwapeleka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Askofu mkuu Nyaisonga daima anajitahidi kuongozwa na kauli mbiu yake ya Kiaskofu “Nalikuja ili wawe na uzima tena wawe nao tele.”. Abate Pambo Martin Mkolwe, OSB amewataka waamini kuchapa kazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo ya familia zao na taifa katika ujumla wake. Watambue kwamba, uvivu ni dhambi. Waamini wajitahidi kuifahamu na hatimaye, kuitangaza imani yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamempongeza Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Katika kipindi hiki cha Miaka 25, matendo makuu ya Mungu yamejidhihirisha katika maisha na utume wake kama mchapakazi; mpenda haki na amani. Askofu mkuu Nyaisonga alizaliwa tarehe 3 Novemba 1966. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 11 Julai 1996 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Tarehe 9 Januari 2011, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma na tarehe 19 Machi 2011 akawekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na hatimaye, kusimikwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma.

Tarehe 17 Februari 2014, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda na kusimikwa tarehe 4 Mei 2014. Tarehe 21 Desemba 2018 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Mbeya na kusimikwa rasmi tarehe 28 Aprili 2019 katika maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu. Ibada hii ya Misa Takatifu ilihudhuriwa pia na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa awamu ya tano aliyewashangaza watu wa Mataifa kwa kukusanya sadaka kutoka kwa “vigogo” waliokuwa wamehudhuria Ibada hii ya Misa Takatifu. 

Askofu Mkuu Nyaisonga
15 July 2021, 16:33