Tafuta

Askofu Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda tarehe 25 Julai 2021 anatarajiwa kutoa Daraja takatifu ya Upadre. Askofu Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda tarehe 25 Julai 2021 anatarajiwa kutoa Daraja takatifu ya Upadre. 

Jimbo Katoliki Mpanda, Tanzania Kumenoga! Mwenye Macho...!

Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda anatarajia kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Shemasi Emili Nestory Sibomana wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Shemasi Emili Nestory Sibomana kama Padre anataka kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwani amemtendea makuu na jina lake ni takatifu. Rej. Lk 1:49.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Mapadre wanashiriki kikamilifu katika huduma ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wamewekwa wakfu kama makuhani wa kweli wa Agano Jipya, kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kuwachunga waamini na kuadhimisha Ibada kwa Mwenyezi Mungu. Wanashiriki kazi ya Mpatanishi, aliye mmoja Kristo Yesu. Mapadre katika daraja ya huduma yao, wanawahubiria watu Neno la Mungu na kutekeleza jukumu hili katika Ibada na Liturujia ya Kanisa, huku wakitenda kwa nafsi ya Kristo Yesu, na wakiunganisha na Fumbo lake, huunganisha matoleo ya waamini na sadaka ya Kichwa chao na katika sadaka ya Misa Takatifu huidhihirisha na kuitekeleza, hata Bwana ajapo! Hii ndiyo sadaka moja iliyotolewa na Kristo Yesu aliyejitoa Nafsi yake mara moja tu kwa Mungu Baba Mwenyezi kuwa ni sadaka isiyokuwa na mawaa. Kwa ajili ya waamini ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu au wagonjwa, hutimiza kwa nguvu yote ya huduma ya upatanisho na faraja, na kumtolea Mwenyezi Mungu mahitaji na sala ya waamini.

Mapadre wanatekeleza huduma za Kristo Yesu aliye Mchungaji na Kichwa kwa kadiri ya mamlaka yao. Huikusanya familia ya Mungu kama jumuiya ya ndugu iliyopenywa na roho ya umoja, na kwa njia ya Kristo katika Roho huiongoza kwa Mungu Baba Mwenyezi. Hatimaye, hujitaabisha kwa kuhutubu na kufundisha, wakisaidiki waliyoyasoma na kuyatafakari katika Sheria ya Bwana, wakifundisha waliyoyasadiki na kuyafuata waliyoyafundisha. Mapadre, washiriki wenye busara wa Daraja ya Uaskofu na msaada na chombo chake, waitwa kutumikia taifa la Mungu, wanakuwa umoja “presbiterio” (presbyterium), pamoja na Askofu wao. Mapadre chini ya Mamlaka ya Askofu, hutakatifuza na kuongoza kundi la Bwana walilokabidhiwa, hulifanya Kanisa lote zima lionekane wazi mahali pao na kutenda kazi ifaayo hata Mwili mzima wa Kristo Yesu ujengwe. Mapadre wanapaswa kuangalia daima mema ya watoto wa Mungu, wajitahidi kuchangia matendo yao katika kazi ya uchungaji ya Jimbo zima, na zaidi, ya Kanisa lote. Askofu aoneshe fadhila za kibaba na Mapadre wamtii na kumpatia heshima yake. Askofu ajenge urafiki na udugu wa kibinadamu na Mapadre wake.

Kwa nguvu ya Upadrisho Mtakatifu na ya utume ulio sawa mapadre wote hufungamana katika udugu wa ndani, unaopaswa kujionesha kwa hiari na kwa moyo katika kusaidiana katika mambo ya kiroho na ya kimwili, ya kichungaji na ya binafsi, katika mikutano na katika ushirikiano wa maisha wa kazi na wa upendo. Mapadre katika maisha na utume wao wawangalie vyema waamini wao waliowazaa kiroho kwa Ubatizo na mafundisho. Wawaongoze watu wa Mungu kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu, daima wakijitahidi kushuhudia sura ya huduma ya kikuhani na ya kichungaji. Wajibidiishe kuwatafuta wale waliopotea na kukengeuka; waamini ambao wameacha kupokea Sakramenti za Kanisa na hata pengine kukosa imani. Mapadre wakiwa wameungana na Maaskofu wao pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu wa Mataita, ili kusudi binadamu wote kwa pamoja waongozwe kwenye umoja na mshikamano wa familia ya Mungu. Rej. LG 28.

Huu ndio wito, maisha na utume wa mapadre unaomsukuma Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Tanzania kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Shemasi Emili Nestory Sibomana wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Ibada hii ya Misa Takatifu itaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Immakulata. Shemasi Emili Nestory Sibomana kama Padre anataka kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwani amemtendea makuu na jina lake ni takatifu. Rej. Lk 1:49. Padre Mtarajiwa Emili Nestory Sibomana alizaliwa tarehe 25 Juni 1990, Kigango cha Kalungu, Parokia ya Katumba, Jimbo Katoliki la Mpanda. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, toka Seminari kuu ya Mtakatifu Augostino, Peramiho, Jimbo kuu la Songea na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko mjini Roma, tarehe 31 Oktoba 2020 akapewa Daraja Takatifu ya Ushemasi wa mpito na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.

Padre Mtarajiwa Emili Nestory Sibomana tangu mwaka 2018 hadi mwaka 2021 alikuwa amejichimbia katika masomo ya Taalimungu ya Maandiko Matakatifu na kujipatia Shahada ya Uzamili. NB. Kwa wale watakaochelewa Sherehe za Upadrisho tarehe 25 Julai 2021, wanaweza kujipanga “kivyao” na hivyo wakashiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya Shukrani tarehe 1 Agosti 2021 itakayoadhimishwa kwenye Parokia ya Katumba, Jimbo Katoliki la Mpanda. Fursa ya Pili ni Misa ya Shukrani itakayoadhimishwa kwenye Sikukuu ya Wakulima, Nanenane, yaani tarehe 8 Agosti 2021 kwenye Kigango cha Kalungu, Parokia ya Katumba, Jimbo Katoliki la Mpanda.

Jimbo Katoliki Mpanda
23 July 2021, 16:24