Tafuta

2021.06.24 Kongamano la vijana jimboni Kayanga-Tanzania kutoka majimbo 8 ya Kanda ya ziwa, tarehe 17-21 Juni 2021 2021.06.24 Kongamano la vijana jimboni Kayanga-Tanzania kutoka majimbo 8 ya Kanda ya ziwa, tarehe 17-21 Juni 2021 

Tanzania:Mwenyeji wa Kongamano la vijana Jimboni Kayanga

Fursa ya Kongamano la vijana katolikini huko Kayanga si tu kutafuta mahali pazuri penye ardhi nzuri na rutuba,bali iwe ni fursa ya kumtafuta Bwana kwanza atakaye waelekeza njia.Amesema hayo Askofu Mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo Kuu la Mwanza wakati wa kufunga Kongamano la Viwawa tarehe 20 Juni Jimboni Kayanga,Karagwe Tanzania ambalo limewaona vijana 1162 kutoka majimbo 8 ya Kanda ya Ziwa.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Kuanzia  tarehe 17 hadi 21 Juni 2021, Jimbo katoliki la Kayanga, wilaya ya Karagwe  Tanzania limekaribisha Kongamano la Vijana katoliki (VIWAWA) kutoka majimbo mbali mbali 8 yanyaounda Kanda ya Mwanza au Kanda ya Ziwa ambayo ni jimbo katoliki la: Rulenge - Ngara, Geita, Bunda, Shinyanga, Musoma, Bukoba, Kayanga na Jimbo Kuu la Mwanza. Kongamano hili limeongozwa na kauli mbiu “kijana nakwamba inuka”, iliyotolewa katika Injili ya Luka 7, 14. Jumla ya vijana 1162 waliudhuria kuongamano hili muhimu kwao kuwawakilisha hata wengine ambao hawakuweza kufika, pamoja na wenyeji vijana wa jimbo la Kayanga 557. Kongamano hilo lilifunguliwa na Misa Takatifu tarehe 18 Juni 2021 likiongozwa na Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo la Kayanga. Katika mchakato wa kongamano hilo watoa mada mbali mbali waliweza kuwasaidia vijana kutafakari kwa kina masuala mbali mbali pia waliweza kufanya hata maandamano ya Km 10 kutoka kituo cha Hija cha  Bikira Maria cha Jimbo kilichopo karibu na Kanisa katoliki la Bugene ambapo waliweza  kusali kwa Mama Bikira Maria wa Lourdes na kutembea  hadi Kanisa Kuu Kayanga.

Katika Misa ya kufunga kongamano hilo iliyoadhimishwa tarehe 20 Juni na kuongozwa na Askofu Mkuu Renatus Nkwande, akishirikiana na Askofu Almachius Rweyongeza mwenyeji wa Kongamano hilo, na uwepo wa mapadre walezi wa Viwawa katika majimbo hayo yote, wamewaasa vijana kutokata taamaa na kutofuata mitindo mbali mbali isiyo adili katu inayojitokeza kila wakati kutoka sehemu mbalimbali za nchi za Magharibu na nyinginezo huku akiwatolea mifano hai ya maisha yao, kutokana na kuona na kufanya uzoefu wa nchi hizo mwenyewe. Mfano halisi alioutoa pia mo ule wa watu wa nchi zilizo endelea kukaa meza ya chakula na kula bila hata ya kufanya ishala ya msalaba. 

Picha ya Pamoja Askofu Mkuu Nkwande,Askofu Rweyongeza ,mapadre,mashemasi na watoa huduma
Picha ya Pamoja Askofu Mkuu Nkwande,Askofu Rweyongeza ,mapadre,mashemasi na watoa huduma

Hata hivyo katika mahubiri yake kuhusiana na masuala ya uchumba na ndoa Askofu Mkuu Nkwande amesema: “Wengine mnafikiri kuoa ni kutimiza wajibu, bila kujua kuwa ni mpango wa Mungu. Katika kuunda familia ni lazima kwanza kujiandaa vizuri”. Ametoa mfano wa hotuba ya Papa ya hivi karibuni yaani ya (tarehe 14 Mei 2021) wakati wa Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia lililoanzishwa tangu 1992 kwa ajili ya kuhamasisha msingi wa maisha ya kifamilia nchini Italia, kama nguzo msingi ya jamii na ili  kuendelea kujizatiti katika kulinda, kudumisha na kutegemeza familia. Na hii ni kwa sababu Italia inakabiliwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wanaokula pensheni, ikilinganishwa na vijana wanaozalisha na kutoa huduma. Watoto ni matumaini ya jamii kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa maana hii inalipa kuwekeza kwa watoto. Kwa sasa Italia inakabilia na uhaba mkubwa wa watoto na hivyo imefikia wakati wao kuweza kuwekeza katika sera bora za familia, ili kupata watoto zaidi. Ili kufanya hivyo Baba Mtakatifu Francisko alihimiza kufanya mabadiliko makubwa katika: miundombinu ya familia, kwa kuwekeza katika uzazi na kupandikiza mbegu ya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Hakuna sababu ya kukata tamaa kutokana na hali ngumu ya uchumi.

Askofu Mkuu Nkwande kwa maana hiyo hakukosa kuwaeleza vijana juu ya tabia za vidhibiti mimba  ambavyo kwa kizazi vimepelekea hali ngumu na kwamba watu wengi katika nchi zilizoendelea wanaangaika sana kwani hawana watoto na serikali zinafanya kila njia kutoa ahadi ya kuweza kusaidia vijana iwapo watazaa watoto, lakini kwa bahati mbaya hawawezi tena kupata watoto hao! Kutokana na hilo ndipo Askofu Mkuu Nkwande amsisitiza zaidi na amewaasa vijana kuwa makini juu ya uthibiti mimba huo na ili kumcha Mungu kwa kufuata mpango wake Mungu. Vile vile Askofu Mkuu amezungumzia juu ya kumtafuta Kristo kwanza kabla ya kutafuta fursa, baadaye fursa hizo zitakuwapo maana ni Bwana ambaye atawaongoza.

Vijana wakiwa wanasikiliza mada mbali mbali wakati wa Kongamano
Vijana wakiwa wanasikiliza mada mbali mbali wakati wa Kongamano

Kwa kutoa mfano halisi, askofu Mkuu Nkwande amesema: “Fursa ya kufika kwenye Kongamano la vijana huko Kayanga si tu katika kutafuta mahali pazuri penye ardhi nzuri na rutuba, bali ni katika kumtafuta Bwana kwanza ambaye baadaye atawaelekeza njia ya maisha yao”. Akiendelea na mahubiri yake na amewaomba vijana hao wajikite kutimiza hayo yote waliyofundishwa kwa kipindi cha kongamano ili waweze kuwa mfano wa ukristo mwema mahali popote watakapokuwa. Pamoja na changamoto nyingi ambazo wanakumbana nazo vijana, lazima wakabiliane na hali hiyo kwa umakini na kuwa mfano katika familia zao na kuudhuria katika jumuiya ndogo ndogo. Ni jambo jema kwa vijana kujijengea imani na matumaini ya leo na kesho ambayo yatawafanya kuishi vema maisha ya kweli ya kikristo.

24 June 2021, 14:59