Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 13 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Mateso na mahangaiko ya mwanadamu yanapata jibu lake katika Fumbo la Msalaba. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 13 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Mateso na mahangaiko ya mwanadamu yanapata jibu lake katika Fumbo la Msalaba. 

Tafakari Jumapili 13 ya Mwaka B: Imani kwa Yesu na Uponyaji Wake!

Kristo Yesu anatukumbusha umuhimu wa kusikiliza, kuitikia na kujibu mahitaji ya watu. Kanisa lijikite katika uponyaji: kwa kuwaondolewa watu dhambi zao; kwa kuponya majeraha ya watu kutokana na kinzani za kijamii kwa sababu Kanisa ni chombo cha upatanisho na Sakramenti ya Wokovu wa watu wa Mataifa. Kanisa linaendesha: Shule, Hospitali na Nyumba za huduma!

Na Padre Nikas Kihuko, Mwanza

Karibu ndugu yangu katika Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 13 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Leo ningependa kutafakari pamoja nawe kuhusu imani thabiti kwa Kristo Yesu na matunda yake ni uponyaji wa ndani. Katika Maandiko Matakatifu kwa hakika, Yesu ameponya watu wengi wenye imani. Maeneo mengine aliwaponya watu hata ambao siyo wa imani yake. Katika ujumla wake Imani ni muhimu katika uponyaji. Kuna mifano mingi ya watu ambao kwa Imani yao waliponywa. Katika Maandiko Matakatifu, Yesu anapita Ziwa la Galilaya kuelekea upande wa pili.  Upande wa Mashariki wa Ziwa la Galilaya ulikaliwa na watu wa Mataifa, walio abudu miungu wengi, mungu wa uzazi, mungu wa mali, mungu wa vita. Na kila mungu alikuwa na mashariti yake, taratibu zake na mambo muhimu yanayoendana naye. Upande wa Magharibi ulikaliwa na Wayahudi wao walimwabudu Mungu mmoja, Mungu wa kweli Yahweh. Yesu amefanya utume katika maeneo yote mawili. Ameanzia kwa watu wa Mataifa na sasa anaenda kwa Wayahudi. Anatukumbusha kwamba Yesu aliwahudumia watu wote, wakila kabila, jinsia na rika ili kuwatangazia na kuwashuhudia Habari Njema ya Wokovu. Akiwa katika eneo la watu wa Mataifa waliwaponya wengi (Marko 5:1-20) Na anaporudi Uyahudi anakuta kundi kubwa la watu wanamsubiri. Yesu alikuwa ana wapinzani wengi kati ya viongozi wa Kiyahudi. (Mark 1:21-27; 3:1-6,.)

 Yairo ni mfano wa kuigwa. Alikuwa mtu maarufu, mhudumu wa Sinagogi, mlinzi wa Maandiko Matakaifu, anayepanga watu wanaohudumu. Katika wadhifa mkubwa hivi na mamlaka aliyokuwa nayo si kitu akampigia magoti Yesu. Mgeni aliyetembea hakuwa na cheo katika jumuiya ya waamini kama alivyo Yairo, ameweka pembeni wadhifa wake akamnyenyekea Yesu. Haombi Yesu kama anaweza kumponya mwanaye bali kwa ujasiri anamwambia naomba umrudishie mwanangu afya kwa kumnyoshea na kumwekea mkono. Yesu akaacha kundi kubwa akaenda na baba mwenye uchungu na mwanae, kutimiza hitaji la baba anayeuguliwa na mwanae. Kristo Yesu anatukumbusha umuhimu wa kusikiliza, kuitikia na kujibu mahitaji ya watu. Kanisa lijikite katika uponyaji: kwa kuwaondolewa watu dhambi zao; kwa kuponya majeraha ya watu kutokana na kinzani na mipasuko ya kijamii kwa sababu Kanisa ni chombo cha upatanisho na Sakramenti ya Wokovu wa watu wa Mataifa. Ili kusaidia yatima kuna nyumba za kuwatunza: kwa wagonjwa kuna zahanati, vituo vya afya, hospitali. Na kwa kumkomba mtu kutoka katika balaa la ujinga na umaskini kuna shule, vyuo na elimu ya maadili. Huo ndiyo utume alotuachia Yesu.

Akiwa safarini kuelekea kwa Yairo anakutana na mama anayeumwa kwa kutokwa na damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. “Stori juu ya stori”. Yairo anaona kikwazo sasa.  Kwa desturi ya Wayahudi, huyo, mama hatakiwi kuungana na watu katika kuabudu, ametumia pesa yote kwa matibabu asipone. Yoyote aliyejifanya kuwa ni rafiki yake alihesabika kuwa najisi katika jamii ya Wayahudi (Walawi 15:25-30). Hakuweza kuolewa ilikuwa ni sababu tosha ya kupewa taraka (Mathayo 5:31) Sio rahisi kutafuta kazi akapata. Alikata mawasiliano na jamii. Lengo ya sehemu hii ya Injili ni kuonesha nguvu ya Mungu inayoganga, kutibu na kumwokoa mtu katika shida na mahangaiko yake mbalimbali.  Pale akili ya kibinadamu inapo ishia, inapo fikia katika ukomo, ndipo nguvu ya Mungu husubiriwa. Pale wataalamu wote waliojitahidi wakashindwa ndipo Yesu alipoonesha nguvu yake ya kutibu, kutakasa na kuokoa!  Yairo alimfuata Yesu na kumwambia uso kwa uso. Huyu mama alimfuata kwa nyuma, kwa siri, kwa imani na hofu kuu. Aliamini akigusa tu pindo la vazi atapona. Kwa muda wa miaka 12 amejiepusha kugusana na watu, leo amethubutu kumgusa Yesu. Kuepuka kuwafanya wengine wasiwe najisi eliepuka vingi lakini alithubutu unajisi umpate Yesu. Cha kushangaza Yesu anamkaribisha amguse vizuri.

Uhusiano wa imani na uponyaji. Nguvu ya uponyaji ni ya Mungu. Imani ya mtu inahitajika katika kupokea uponyaji. Yesu kusema binti imani yako imekuponya anarudi katika tamaduni za kiyahudi neno binti lina gusa utambulisho wa mwanafamilia, mpendwa katika familia. Katika mtazamo huu binti, neno lenye nguvu ya uponyaji. Binti yako ameshafariki usimsumbue mwalimu (Marko 5:35). Anaturudisha kwenye simulizi la Martha, Mariam na Lazaro katika injili ya Yohane 11.  “Yesu kama ungekuja mapema ungenusuru maisha ya kaka yetu. Wapoteza matumaini, walipoteza Imani. Imani ilihitajika katika uponyaji. Mwinjili Marko hajasema Yairo alikuwa anaongea nini kwa kuchelewa kwa Yesu. Lakini Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane (Marko 5:37). Hawa watatu ndio walishuhudia hata kubadirika kwa sura Yesu, mateso ya Yesu Gethemane (14:33). Kwa nini mnalia mtoto hajafa amelala tu (Marko 5:39). Ni ngumu kukubali, kuipokea na kuelewa. Hii sasa ni namna ya kumfufua na sio kumponya. Kulala ni tukio la muda tu na aliyefariki ni la moja kwa moja. Maana wazee wa kimila wamejiridhisha kwamba tayari amefariki.

Yesu akawachukua wazazi na Mitume watatu kwenda katika tukio la uponyaji, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa ukuu na utakatifu wa Mungu. Imani inahitajika katika uponyaji. Alipofika akamwambia Talitha kumi ni Kiaramayo, Lugha ya Wayahudi wa kipato cha chini, watu wa kawaida kabisa. Lugha inayoendana na Kihebrania. Lakini Kihebrania ilikuwa ni Lugha ya dini ya Kiyahudi, inatumiwa na serikali, pia inatumika na Wayahudi wa hadhi ya juu. Mwinjili Marko ametafsili Talitha cumi kigiriki kwa ajili ya Wakristo wa kwanza ambao hawajui Kiaramaiki. Yesu akamshika mkono kijana, kumshika mototo kwa mkono, kumgusa binti umevunja Torati. Mtu aliye gusa mwili ulokufa atakuwa najisi mpaka jioni (Walawi 11:39) au kwa siku saba (Hesabu 19:11), au atengwe kwa muda (Hesabu 5:2-3). Lakini yote yalikuwa katika nia njema. Hakuna aliyemwambia kuwa umekuwa najisi kwa kuguswa na mama mwenye Imani wakati mama amepona mardhi yake. Hakuna aliye mwabia Yesu najisi kwa kugusa jeneza kwani aliyefariki amefufuliwa na sasa anaomba uji na anatembea. Hii inamaana kuwa utume wote wa Yesu ulijikita katika mahitaji ya mtu kiroho, kimwili, kisiasa na kiuchumi. Mama sasa ameanza maisha mapya ya kuungana na jamii. Binti alikuwa na umri wa miaka 12, mama aliteseka kwa muda wa miaka 12 (Marko 5:12) Kwa desturi ya Kiyahudi ni umri unaokaribia kuolewa au kuanza maisha mapya na mama ana maliza maisha ya zamani.

25 June 2021, 07:43