Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 12 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Imani thabiti katika shida na magumu ya maisha. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 12 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Imani thabiti katika shida na magumu ya maisha. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 12 ya Mwaka B: Imani Thabiti

Masomo ya dominika ya 12 ya Mwaka B wa Kanisa yatatupatia mwongozo wa namna ya kukabiliana na matatizo na mahangaiko katika maisha. Mwongozo huu sio mwingine bali ni kumtumainia Mungu aliye nguvu za watu wake na ngome ya wokovu kwa Kristo wake. Yeye huwaokoa watu wake, huwabariki urithi wake, huwachunga na huwachukua milele yote (Zab.26:8-9). Imani Thabiti.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Karibu katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 12 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yatatupatia mwongozo wa namna ya kukabiliana na matatizo na mahangaiko katika maisha. Mwongozo huu sio mwingine bali ni kumtumainia Mungu aliye nguvu za watu wake na ngome ya wokovu kwa Kristo wake. Yeye huwaokoa watu wake, huwabariki urithi wake, huwachunga na huwachukua milele yote (Zab.26:8-9). Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Ayubu (38:1,8-11); ni jawabu la Ayubu ya kwanini anateseka licha ya kumwamini na kumtumaini Mungu. Ayubu, aliyeishi kitakatifu, alishindwa kufahamu kisa cha mateso yake. Hii ni kwa sababu, kadiri ya mawazo na fikra za kiyahudi, Mungu hulipa haki juu ya matendo ya mtu hapa duniani kabla hajafa. Ayubu mtu tajiri na mchamungu, daima alibaki mwaminifu kwa Mungu licha ya majaribu mengi aliyoyapata. Ayubu alipoteza watoto wake na mali yake yote kwa ghafla na kisha alipata ugonjwa wa ngozi ulioambatana na majipu mwili mzima kutoka utosini hadi kwenye unyayo. Katika hali hiyo, Ayubu alimlalamikia Mungu akimuuliza; Je, ni haki kumwacha mtu mwenyehaki kama mimi niteseke namna hii? Licha ya kuwa rafiki zake walimwambia kuwa sababu ya mateso yake ni dhambi zake mwenyewe, na kwamba Mungu hawezi kumwokoa, lakini yeye alibaki mwaminifu kwa Mungu.

Uaminifu wake ukamfanya Mungu aingilie kati. Kwanza anamuuliza Ayubu kama anaweza kueleza jinsi mambo yanavyokwenda katika maisha, jinsi radi na ngurumo vinavyotokea, jinsi bahari inayojaa na kupwa na namna nyota zinavyozunguka angani. Ayubu hakuweza kutoa jibu lolote kwa maswali aliyoulizwa na Mungu. Hii ilimuonyesha jinsi akili ya mwanadamu isivyoweza kutambua mipango ya Mungu. Kisha Mungu mwenyewe akamwongoza afike hitimisho yakini akimwambia; kama huwezi hata kueleza jinsi vitu unavyoviona kwa macho vinavyofanya kazi, unawezaje au rafiki zako wanawezaje kujifanya kutoa majibu kwa maswali ambayo hakuna mwanadamu alishawahi kutoa jibu sahihi jinsi gani Mungu anashughuika na wanadamu! Ayubu akatambua kuwa hajui kitu na akamwomba Mungu msamaha. Somo hili linatusaidia tuwe na ujasiri wa kupokea majaribu ya kimaisha tukitumainia hekima ya Mungu na wema wake. Ayubu anatufundisha kuwa; Njia ya hekima ya kutatua matatizo yetu na kujikwamua katika mateso si kumwuliza Mungu maswali kwanini haya yanatokea, bali ni kujikabidhi katika mipango yake, tukitumainia hekima, uwezo na upendo wa Mungu. Kama zawadi kwa uaminifu wa Ayubu katika mateso yake, Mungu alimpa familia mpya, kubwa zaidi kuliko ile ya awali aliyoipoteza na kumbariki kwa kumjalia mali nyingi kuliko alizokuwa nazo awali. Kumbe tunaona kuwa kila tulichonacho ni zawadi kutoka kwa Mungu na hakuna mtu anayeweka matumaini yake kwa Mungu wakati wa mateso, Mungu akamwacha.

Somo la pili la Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (2 Kor. 5:14-17); latufndisha umoja na uhusiano uliopo kati ya Yesu na wafuasi wake kwamba; Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, nasi tumekufa na kufufuka pamoja naye katika imani na ubatizo. Kama sasa tu viumbe vipya, basi tuishi kwa ajili ya yule aliyekufa na kufufuka kwa ajili yetu, Yesu Kristo, Bwana na mwokozi wa maisha yetu alikufa na kufufuka ili sisi nasi tufe kuhusu dhambi na kuamkia uzima wa milele. Katika Injili ilivyoandikwa na Marko (Mk. 4:35-40); Yesu anatuliza dhoruba. Kadiri ya imani ya Agano la Kale, hii ilikuwa kazi ya Mungu peke yake. Hivyo Yesu kutuliza dhoruba ni dhahiri kuwa yeye ni Mungu, nafsi ya pili.  Katika tukio hili, Yesu anatufundisha namna ya kupambana na majaribu kama mtu binafsi na kama jumuiya. Mashua inawakilisha Kanisa. Wakristo wa mwanzo waliona ile mashua pamoja na Yesu na mitume wake kama ishara ya Kanisa. Yesu alitumia mashua ya Petro kuwahubiria makundi ya watu (Lk 5:3); ni kwa njia ya Kanisa anaendelea kufanya habari njema ienee duniani kote. Kanisa ni kama mashua ambalo kazi yake ni kutuvushi kutoka upande mmoja wa ziwa yaani dunia na kutupeleka upande mwingine wa ziwa yaani mbinguni. Ili tuweze kuvuka salama sharti tuwe na Yesu ndiyo maana aliahidi; mimi nipo pamoja nanyi siku zote mpaka ukamilifu wa dahari (Mk 28:20).

Mwinjili Marko anatuambia; “Yesu alikuwa amelala” (Mk 4:38), fofofo hata kutoisikia dhoruba ilipoipiga mashua kwa mawimbi yake. Yawezakuwa ni kwasababu alihubiri siku nzima hivyo alichoka. Hii inatuonyesha jinsi Yesu alivyoshiriki shida na mahangaiko yetu kwa kutwaa mwili wetu wa kibinadamu. Lakini kwa upande mwingine imani na matumaini makubwa yake kwa Mungu Baba yalimfanya alale kwani kuwa mikononi mwa Mungu ni salama na mashua isingeweza kuzama bila matakwa ya Mungu. Mitume kwa upande wao nao walichoka lakini hawakuweza kulala kwa hofu na mashaka ya dharuba kuweza kutokea baharini. Na ilipotokea walijaribu kwa nguvu zao zote kuondoa maji yaliyoingia katika mashua bila mafanikio. Hofu na mashaka vikazidi kuwaingia na ndipo wakakumbuka kuwa kati yao yupo Mungu nafsi ya pili muweza wa yote, wakaomba msaada kwake naye akawaokoa. Hivi ndivyo ilivyo hata kwetu sisi kuwa kila mara tunakuwa na mashaka na kukata tamaa nyakati za matatizo baada ya kujaribu kwa nguvu zetu zote kuyatatua na kushindwa na kufikiri kwamba Mungu ametusahau kabisa.

Tukumbuke kuwa Yesu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu yupo nasi daima. Yale yanayozidi uwezo wetu tukate rufaa kwake kwa moyo wa imani naye atatuokoa na taabu zetu zote. Nyakati zingine sala na maombi yetu yanakuwa ya malalamiko kama walivyofanya mitume wakisema; “Bwana haujali kwamba tunaangamia?” (Mk 4:39). Ilikuwa kana kwamba kumwambia; Bwana tupo hapa tukihangaika kuokoa maisha yetu na yako na wewe unaendelea kulala? Unatujali sisi kweli? Wakati mwingine imani yetu kwa Mungu inapotetereka tunaanza kuona mashaka. Mungu anakaa kimya licha ya sala zetu tunaanza kumlaumu kwa kutotujali. Lakini Yesu akainuka akaituliza dharuba na mawimbi akisema; “kimya, tulia” (Mk 4:39) ni maneno aliyoyatumia pia kumtoa mtu pepo mchafu (Mk 1:25). Kisha akawakemea mitume wake akisema; “Kwa nini mliogopa, imani yenu iko wapi?” (Mk 4:40). Basi tuushikilie ushauri wa Paulo katika somo la pili akisema; Ukweli kwamba Yesu alikufa na kufufuka kutoka wafu kwa ajili yetu kunafanya imani na matumaini yetu kwake yasitetereke. Tunapaswa kujisikia nyakati zote kuwa tumezungukwa na upendo wa Kristo, tumeunganishwa na Kristo kwa njia ya upendo wake kama kwa kamba imara, kiasi kwamba hatupaswi kuruhusu ikatike hata kama tutakumbwa na mateso makali kiasi gani. Kama Kristo amekufa na kufufuka kwa ajili yetu, basi tunapaswa kuishi na kufa kwa ajili yake; katika mipango ya upendo wake, na majaribu yetu ni njia tu ya kufikia ufufuko wetu na furaha ya milele mbinguni.

Jumapili 12
18 June 2021, 16:09