Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 11 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Mwenyezi Mungu anatenda kazi zake kwa kushirikiana na binadamu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 11 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Mwenyezi Mungu anatenda kazi zake kwa kushirikiana na binadamu! 

Tafakari Jumapili 11 ya Mwaka B: Ukuu wa Ufalme wa Mungu!

Liturujia ya Neno la Mungu inatualika kuutafakari ukuu wa Ufalme wa Mungu. Mungu hufanya kazi kati yetu na ndani yetu kwa njia ya hatua ndogo ndogo ambazo mwishoni huwa na matokeo chanya. Sisi ni watenda kazi pamoja na Mungu katika kuujenga ufalme wake na mbegu ya ufalme wa Mungu imepandwa ndani yetu na hakika itazaa na kukomaa ikiwa tutaipa nafasi stahiki!

Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya 11 ya mwaka B wa Kanisa ambapo masomo yanatualika kuutafakari ukuu wa Ufalme wa Mungu. Mungu hufanya kazi kati yetu na ndani yetu kwa njia ya hatua ndogo ndogo ambazo mwishoni huwa na matokeo makubwa ajabu. Sisi ni watenda kazi pamoja na Mungu katika kuujenga ufalme wake na mbegu ya ufalme wa Mungu imepandwa ndani yetu na hakika itazaa matunda ikiwa tutaipa nafasi stahiki ya kukua na kukomaa! TAFAKARI: Nabii Ezekiel katika somo la kwanza anapata maono ya kurejeshwa kwa Ufalme lakini si tu ufalme ambao watu wa taifa teule waliupoteza bali ni ule ambao utaletwa na Masiha mwenyewe. Na hilo liweze kufanyika Mungu anaanza na kilicho kidogo sana, kitawi laini ambacho anakiweka katika udongo juu ya mlima mrefu. Nabii anatangaza kwa watu walio uhamishoni kwamba Mungu ataruhusu uumbaji mpya juu ya magofu ya Israeli. Hii ni ahadi ya matumaini. Ukuu wa Mungu hujidhihirisha katika mambo ambayo mwanzo wake ni mdogo na wa kawaida sana, huanza kidogo kidogo, hatua kwa hatua na baadae huzaa matunda mengi sana. Ndivyo lilivyo fumbo la ufalme wa Mungu.

Dhamira ya ukuu wa Mungu unaojidhihirisha kupitia mambo madogo madogo inaendelezwa tena katika somo la pili na tunaweza kuitafakari vizuri kwa kutazama nafsi ya Mtume Paulo mwenyewe anayewaandikia Wakorintho. Ni katika waraka huu wa pili kwa Wakorintho ambapo Paulo Mtume anasema wazi kuwa nguvu yake iko katika udhaifu. Mtume Paulo alikutana na vikwazo vingi ikiwemo kupingwa katika utume wake. Hata hivyo hakati tamaa bali anaweka bidii zaidi akiamini ya kuwa ni katika yote hayo anayopitia uweza wa Mungu unajidhihirisha. Aidha, anaishi katika imani na tumaini la kuunganika na Bwana. Paulo Mtume anatukumbusha ya kuwa tutapata thawabu kwa bidii tunayoiweka katika kumtumikia Bwana kwa hali zote maana ni katika hayo ukuu wake hujidhihirisha. Mwinjili Marko anaweka mkazo kuwa Mungu yu kati yetu na anaitenda kazi yake pasipo hata sisi kujua anaitenda namna gani. Kwa mifano aliyoitoa Yesu anafundisha kwamba ufalme ni matokeo ya kitendo cha Mungu mwenyewe. Mbegu ni neno la Mungu na ndani yake mna nguvu isiyopingika. Neno likishatangazwa linapenya akili na mioyo na kuleta mabadiliko kwa wale wanaolipokea hata kama juhudi binafsi kutoka kwao ni kidogo. Changamoto haziwezi kuliondoa tumaini la kwamba ufalme wa Mungu unakua na kuwa utawala wa Mungu kwa ulimwengu mzima.

KATIKA MAISHA: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatikani, kwa masomo haya tunaalikwa kuwa na ufahamu kwamba katika matendo madogo madogo ya kila siku kuna mbegu ya Ufalme wa Mungu. Ni katika watu, vitu, matendo, matukio na mambo mengine madogo madogo ndiko iliko siri ya ukuu wa ufalme wa Mungu. Tunakutana na Mungu katika hatua ndogo ndogo za maisha yetu ya kila siku. Ndivyo ilivyompendeza Mungu kutenda. Tunachopasika kufanya ni kufungua macho na mioyo yetu tupate kuona na kupokea kile ambacho Mungu anatupatia. Aidha, kama ilivyo kuwa kwa Mtume Paulo, tu watenda kazi pamoja na Mungu na tusichoke kuweka bidii hata katika changamoto. Imani na tumaini letu kwake vitutegemeze. Tujiaminishe katika mikono ya Mungu na hakuna anachoshindwa kukikuza na kukifanya kizae matunda na kuwa na matokeo makubwa. Kazi hata kama ni ndogo sana au inazongwa na magumu mengi. Ikiwa tunaifanya kwa ajili ya Mungu basi si kazi bure. Lazima izae matunda.

Historia ya Ukristo ni ushuhuda tosha wa namna mbegu ya ukuu wa ufalme wa Mungu huzaa matunda. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo, Wamisionari na wale wote waliofanya kazi ya kueneza Habari njema ya Ufalme wa Mungu, watakatifu, mashahidi, waungama imani, watawa, wamonaki na watu wa ndoa n.k. wanatoa ushuhuda wa namna Mungu anavyotenda kazi katika mambo madogo madogo ambayo mwishoni huwa na matokeo chanya. Hivyo basi ndoto na mipango yetu yote tuiaminishe kwa Mungu. Tuombe fadhila ya unyenyekevu na kutembea na Mungu katika kila hatua ndogo tunayopiga katika maisha. Nakutakia Dominika Njema.

Liturujia J11
11 June 2021, 15:35