Tafuta

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani na Mashuhuda wa Upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; Umoja na tofauti zao msingi. Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani na Mashuhuda wa Upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; Umoja na tofauti zao msingi. 

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Umoja na Tofauti Zao Msingi

Sherehe ya watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani. Petro aliikiri Imani kwa kumwambia Kristo Yesu “wewe ndiwe Kristo mwana wa Mungu aliye hai” (Mathayo 16:16) na Mtume Paulo baada ya kuongoka alitangaza na kushuhudia Imani kwa Mataifa. Petro na Paulo ni mfano wa umoja na utofauti katika Kanisa katika muktadha wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Na Padre Nikas Kihuko, - Mwanza, Tanzania.

Kila mwaka ifikapo tarehe 29 mwezi Juni, Kanisa huadhimisha Sherehe ya watakatifu Petro na Paulo. Miamba ya Imani.  Petro aliikiri Imani “wewe ndiwe Kristo mwana wa Mungu aliye hai” (Mathayo 16:16) na Paulo aliwahubiria watu hiyo Imani kwa mataifa. Petro na Paulo ni mfano wa umoja na utofauti katika Kanisa katika muktadha wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Maana watakatifu na wafia dini wote huwa na siku yao maalumu ya kusherehekea. Lakini Petro na Paulo hufanyika siku moja.  Kwani imewekwa tarehe moja? Ukiangalia wito wao tofauti, Petro aliitwa katika shughuli zake za uvuvi. Yesu akamwambia kuanzia leo utakuwa mvuvi wa watu (Marko 1:16) Mtume wa Mataifa Paulo aliitwa na Kristo mfufuka akiwa safarini katika kulitesa Kanisa (Matendo 9:1-19). Kwanini  tusherehekee leo? Tarehe zao na namna ya kifo inatofautiana. Mtume Petro alisulubiwa, lakini walimsulubu kichwa chini miguu juu ili kumtofautisha na Kristo. Paulo mtume wa mataifa aliuwawa kwa upanga. Umoja wao unaonekana katika mateso waliyo yapata katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu na kama kielelezo cha upendo wao kwa Kanisa.

Mateso yao yanatukumbusha sisi kuwa kumfasa Kristo lazima kupitia magumu na changamoto katika kumwamini Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Jambo la msingi ni kudumu katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu! Petro kwa kutwaliwa miongoni mwa wa wavuvi anakua msimamizi wa wavuvi wote.  (Luka 5). Hivyo sherehe hii ni kubwa hasa kwa wavuvi wanapomkumbuka msimamizi na mwombezi wao, lakini aliitwa pia kuwa ni mvuvi wa watu! Paulo shughuli zake zilikuwa kushona mahema (Matendo 18:1-4) Hivyo anakuwa msimamizi wa mafundi mahema na mwombezi wao.  Kumbe tuwaombe hawa miamba wa imani watuombee katika kazi zetu za kila siku tuweze kufanikiwa na kama sehemu ya ushuhuda kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Injili.  Wao ni wasimamizi wa waandishi wote maana wameandika nyaraka mbalimbali (Paulo inaaminika kaandika nyaraka 14 katika Biblia) hivyo ni waombezi wa waandishi wote. Lakini kwa nini ifanyike katika siku moja?

Tunajua kuwa tarehe 22 Februari kila mwaka tunasherehekea Ukulu wa Mtakatifu Petro, kama ni mtume wa kwanza, aliyepewa funguo dhamana na mamlaka ya kuliongoza Kanisa. Lakini hakuna sherehe ya Petro na siku yake kama ilivyo kwa mitume wengine. Tarehe ya 25. Januari kila mwaka tunasherehekea kwa kuongoka kwa Mtume Paulo. (Matendo 9:1-31). Kuna sababu nyingi za kuunganisha hawa mitume wakuu wawili ifanyike siku moja. Mapokeo ya Kanisa yanasisitiza kuwa Petro na Paulo inaunganishwa ili kuheshimu wafia dini wa Roma.  Wote waliuwawa kikatili kama wafia dini ndiyo maana sherehe yao inafanyika siku moja.  Petro alisurubiwa kichwa chini miguu juu na Paulo aliuwawa kwa upanga. Mtakatifu Augustino anasema, sherehe hii ni kubwa na wameunganisha mitume hawa wakubwa pamoja iwe siku moja kwa sababu walikuwa wamoja hata katika tofauti zao msingi. Hata kama hawakuuwawa siku moja, imewekwa pamoja kwa sababu walikuwa wamoja.  Mtakatifu Augustino anasema kuwa tarehe hii ndiyo kumbukumbu ya siku waliyo hifadhi masalia yao.

Tofauti zao zilikuwa za kiutendaji lakini waliitunza Imani, (Nimevipiga vita vilivyo vizuri mwendo nimeumaliza, Imani nimelinda 2Timoteo 4:6-8) waliishi Imani, walieneza Imani kwa mataifa kama Paulo na kuitwa mtume wa mataifa, na mwalimu. Pia kwa Wayahudi Petro alitumia Maisha yake yote kueneza na kumkiri Kristo Yesu kwa Wayahudi wote.  Tutunze Imani tuliyoachiwa, tuirithishe kwa Watoto wetu tunu zilizo njema na tusiogope kuwatumikia wengine kama Petro na Paulo walivyojitoa, nyakati za furaha na za mateso.

29 June 2021, 16:28