Tafuta

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni muhtasari wa imani na mapendo ya Kristo Yesu kwa Kanisa lake! Fumbo la Ekaristi Takatifu ni muhtasari wa imani na mapendo ya Kristo Yesu kwa Kanisa lake! 

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Muhtasari wa Imani na Upendo!

Mababa wa Kanisa wanasema, Fumbo la Ekaristi Takatifu ndio jumla na muhtasari wa imani ya Kanisa. Ekaristi Takatifu ni ishara ya upendo. Ni alama ya upendo wa Mungu kwetu na chemchemi ya upendo wote. Katika Sakramenti hii ya upendo, tunaalikwa kuushiriki upendo huu, na kuwashirikisha upendo huu, ndugu zetu. Yaani kwa kuwa Ekaristi kwa wengine katika ushuhuda angavu!

Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Neno la Mungu tunapoadhimisha sherehe ya mwili na damu ya Kristo. Yesu Kristo anatulisha mwili na damu yake kama chakula cha roho zetu. Hiki ni kielelezo cha mapendo yake kwetu sisi. Aidha kwa kujitoa yeye mwenyewe kikamilifu anafanya agano kati yetu na Mungu na kuwa mpatanishi wetu anayeuhisha roho zetu. Mwaliko tunaopewa katika sherehe hii kubwa ni kuwa mashuhuda wa upendo huo na wa agano analolifanya nasi. Tutayashuhudia mapendo hayo na agano hilo kwa kujitoa kikamilifu kwa Mungu na kwa wenzetu. MASOMO NA TAFAKARI: Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha Kutoka, Mungu, kupitia kwa Musa anafanya agano na watu wake kwa maneno na kwa sadaka ya amani ya ndama waliochinjwa. Watu wanaahidi kuyashika yale yote yaliyonenwa na Bwana. Damu ya ndama hawa inatumika kufunga na kuthibitisha agano hilo. Maneno na sadaka ni ishara ya agano. Hata hivyo ni hizi ishara za nje ambazo katika hatua ya awali zilitumika kuthibitisha maagano ambayo Mungu alifanya na watu wake ingawa waliyakiuka mara nyingi.

Katika somo la pili la Waraka kwa Waebrania tunaona muendelezo wa dhamira ile ya kuwepo agano kati ya Mungu na watu wake. Lakini katika hatua hii sadaka inayotolewa si kwa damu ya wanyama isipokuwa kwa damu ya Kristo Yesu aliyejitoa mwenyewe kama kuhani na mwanakondoo. Si tena ishara ya nje bali ni uzima wake Yesu mwenyewe ambaye anautoa uhai wake kwa kumwaga damu yake. Ni damu yake na ni uzima wake ndivyo vinavyowagusa waamini na kujenga muunganiko na Mungu. Yeye amekuwa mpatanishi kati yetu sisi na Mungu na huzisafisha dhamiri zetu na kutuweka wakfu kwa ajili ya Mungu. Katika Injili, Mwinjili Marko anaturejesha katika Karamu ya mwisho aliyokula Yesu na wanafunzi wake ambapo aliweka sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Katika karamu hii ya mwisho Yesu aliadhimisha Pasaka na wanafunzi wake. Ilikuwa ni desturi ya Wayahudi kuila Pasaka wakikumbuka kukombolewa kwa kutoka Misri na jinsi walivyosalimika kwa njia ya damu ya mwanakondoo iliyopakwa katika milango yao.

Katika karamu hii ya mwisho Yesu haadhimishi tu Pasaka ya Kiyahudi bali anaadhimisha Pasaka yake mwenyewe. Anafanya ukamilifu wa kile kilichofanyika katika Agano la Kale. Anajitoa mwenyewe anaposema huu ni mwili wangu na hii ni damu yangu. Hili ndilo Agano hasa lenye ukamilifu maana halifanyiki kwa kutoa kitu au kiumbe kingine bali kwa kujitoa mwenyewe. Ndugu mpendwa, iko tofauti kubwa kati ya mkataba na agano. Wakati mkataba uhusisha ahadi na kubadilishana vitu, agano uhusisha viapo na kubadilishana nafsi. Katika mkataba ni vitu nje yetu vinavyothibitisha makubaliano yetu lakini katika Agano ni sisi wenyewe tunajitoa na kwa kujitoa kikamilifu tunathibitisha agano. Mungu amefanya agano nasi kwa kujitoa mwenyewe kuwa kwetu chakula cha roho zetu apate kuzigusa kabisa nafsi zetu. Huo ndio upendo mkubwa alioonesha kwetu. Sisi nasi tunapasika kujitoa kwake na kwa wenzetu kama mashuhuda wa upendo huo. Hii ndiyo inapaswa kuwa sala yetu katika sherehe hii kama tunavyoimba: Pokea moyo wangu ee Mungu wangu, niweze kukupenda kwa pendo lako. Unipe moyo wako ewe Yesu mkombozi wangu shinda mwangu nami daima mwako.

Ndugu mpendwa, kwa njia ya adhimisho la Ekaristi Takatifu, waamini wanaungana tayari wao wenyewe na Liturujia ya mbinguni na wanaanza kutangulia kushiriki uzima wa milele Mungu atakapokuwa yote katika wote! Kwa ufupi kabisa, Fumbo la Ekaristi Takatifu ndio jumla na muhtasari wa imani ya Kanisa. Kumbe, namna ya waamini kufikiri hulingana na Fumbo la Ekaristi Takatifu na Ekaristi kwa zamu yake huimarisha namna yao ya kufikiri. Rej. KKK 1324 – 1327. Ekaristi Takatifu ni ishara ya upendo. Ni alama ya upendo wa Mungu kwetu na chemchemi ya upendo wote. Katika Sakramenti hii ya upendo, tunaalikwa kuushiriki upendo huu, na kuwashirikisha upendo huu, ndugu zetu. Yaani kwa kuwa Ekaristi kwa wengine! Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, anatufundisha akisema: “upendo tunaouadhimisha katika sakramenti si jambo la kubaki nalo sisi wenyewe. Kwa tabia yake inadai kushirikishwa kwa wote. Kile ambacho ulimwengu unahitaji ni upendo wa Mungu; unahitaji kukutana na Kristo na kumwamini. Ekaristi ni chemichemi na kilele si tu cha uhai wa Kanisa, bali cha utume wake pia: Kanisa halisi la kiekaristi ni kanisa la kimisionari.”

Ndugu mpendwa, katika sherehe hii kubwa hufanyika maandamo na Yesu wa Ekaristi huzuru katika mitaa yetu akitubariki. Sisi tunaompokea katika maumbo ya mkate na divai tunapokea utume huo wa kuendelea kumtembeza kila siku katika mitaa yetu na kumfanya akutane na watu na kuwapa baraka zake. Hilo tunaalikwa kulifanya kwa kujitoa kwa mapendo kwa Mungu na kwa wenzetu. Hivyo basi, kuiishi kimamilifu Ekaristi Takatifu lazima tujifunze upendo. Hatuwezi kuuonja utamu wa Ekaristi Takatifu kama hatujitoi katika mapendo. Hata hivyo, upendo ni hatua. Upendo ni mchakato. Mama Theresa wa Calcutta anasema: “Penda mpaka uumie, endelea kupenda mpaka uone kwamba hauumii tena.” Basi na tukawe mifano ya Upendo; tukajimege bila ya kujibakiza ili kuwa Ekaristi kwa ajili ya wengine.

Sakramenti Kuu
04 June 2021, 16:01