Tafuta

Kumbukumbu ya Moyo Safi wa Bikira Maria: Ushuhuda wa imani katika matendo! Kumbukumbu ya Moyo Safi wa Bikira Maria: Ushuhuda wa imani katika matendo! 

Kumbukumbu ya Moyo Safi wa Bikira Maria: Ushuhuda wa Imani

Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa ameshiriki kwa namna ya pekee kabisa katika kazi ya Ukombozi. Kwa mpango wa maongozi ya Mwenyezi Mungu amekuwa hapa duniani Mama Mtukufu wa Mkombozi aliye Mungu, mwenye moyo mkuu kuliko wote, mtumishi wa Bwana mnyenyekevu aliyeshiriki mateso ya Mwanaye wa pekee tangu mwanzo hadi mwisho, mfano wa Utii na Imani.

Na Padre Ferdinand Lukoa SDS, - Roma.

Yafuatayo ni mahubiri yaliyotolewa na Padre Ferdinand Lukoa Msalvatorian kwa Jumuiya ya watanzania wanaosoma na kuishi mjini Roma kama sehemu ya utamaduni wa watanzania kunogesha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa hasa wanapokuwa ugenini huku, Bondeni kwenye machozi!  Tarehe 12 Juni 2021 ilikuwa ni siku ya pekee sana kwa watanzania kuweza kukutana tena baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona kutinga na kusababisha maafa makubwa sehemu mbalimbali za dunia. Baada ya chanjo, watu wanaweza kukutana tena kama ilivyokuwa hapo awali. Sasa endelea na mahubiri. Wapendwa Taifa la Mungu, Ndani ya wiki hii mitandaoni kumezagaa video ya bint aliyejifungua mtoto na kumtupa kwenye chaka la miiba lililojaa wadudu. Sijui kwa undani ni wapi na nini kilimpata yule dada mpaka kufikia kufanya kitendo kile. Mwenyezi Mungu ni mwaminifu, katika video ile nilisikia sauti ya mwanaume akifoka kwa ukali na ujasiri mkubwa akisema: “Wewe unaona raha kuja kumtupa mtoto porini? Haya mtoe, mtoe, mtoe wadudu! Sasa unamuogopa wakati wa kwako na umemtupa mwenyewe porini? Pumbavu wewe. haraka tumvalishe nguo tumuwahishe hospitali. Mungu kakusaidia umejifungua vizuri salama kabisa. Na Mungu atamsaidia huyu mtoto atapona…”

Sikuamini nilipoiona ile video na hasa kuona ile sura nzuri ya kale katoto kenye afya ilivyochafuka kwa tope na wadudu huku akilia! Nilibaki mdomo wazi! Nilijiuliza maswali mengi mno bila majibu: Hivi huyu bint ana akili timamu? Kubeba mimba miezi tisa na kujifungua salama haikuwa tabu ila kumpeleka mtoto nyumba ya yatima au hata kumtelekeza mlangoni kwa mtu ambaye angehakikisha uhai wake nalo ni jambo gumu? Kwa nini kuua ni kitu rahisi sana siku hizi? Hata kama baba wa mtoto kakimbia majukumu, lakini mama mzazi kufikia hatua ya kudiriki kuua mtoto wako mwenyewe, sasa ni nini kitakachomzuia huyu binti asiue watu wengine? Mungu huona kila kitu tufanyacho maishani mwetu, na ndiyo maana haikuwa siri, kwamba wapo waliomuona akifanya kitendo kile na wakamnasa!  Simuhukumu, lakini mahangaiko yangu ya moyo yalinifanya niende mbali kifikra na nikawaza kama bint yule anaweza kupata usingizi mtulivu maishani mwake na hasa Mungu akijalia mtoto yule akue na kupata habari ya kuwa alifanyiwa kitendo kile na mama yake mzazi!

Wapendwa, Katika kujiuliza haya, nikaguswa na mahangaiko ya Mama Bikira Maria wakati mtoto Yesu alipopotea kwenye msafara na kumtafuta kwa siku tatu! Nina hakika Mama Maria hakulala usingizi, hakula, hakunywa! Mawazo mchanganyiko na yenye hofu yalimtawala moyoni na kumtafakarisha mengi! Moyo wake uliteseka! Waswahili wanasema “Toto baya zuri kwa mama”. Nimejiuliza: je, swali la Mama Maria kwa Yesu lilikuwa na hasira? Sidhani! Maria alijua pia kuwa hasira ni sawa na kula sumu huku ukitegemea adhurike mwingine! Na ingekuwa ni mazingira yetu ya Kitanzania, nini lingekuwa jambo la kwanza kufanyiwa huyu mtoto? Labda viboko, maneno makali, nk. Mtakatifu Yosefu ndio kabisaaaa hasemi chochote! Moyo wa mwanadamu huchafuka kwa mawazo, maneno na matendo! Huwezi kumzuia binadamu asiwaze, lakini si kila unalowaza lazima uliseme na ulitende! Tutunze usafi wa mioyo yetu dhidi ya mawazo, maneno na matendo yasiyompendeza Mungu. Naamini Mama Maria ana mahangaiko pia kwetu sisi wanawe hasa tunapopita njia ya upotovu au kutupwa nje na mifumo gandamizi ya ulimwengu au dhambi zetu!

Pamoja na changamoto zote alizopata tangu kumchukua mimba Bwana wetu Yesu Kristo, hakupoteza uaminifu kwa Mungu. Ndiyo maana amevishwa ‘mavazi ya wokovu na kufunikwa vazi la haki, kilemba cha maua, na kupambwa kwa vyombo vya dhahabu, akawa mtu wa kusifiwa’ kwa uadilifu wake kama alivyosema Nabii Isaya katika somo la kwanza. Katika hali ya mtoto yule aliyetupwa, nikatafakari ile kanga, nikaona ni kama vazi la haki ambalo Mwenyezi Mungu amemvika kupitia binadamu wenzake kwa kuhukumiwa na mama yake bila kosa! Akaombewa dua njema kuwa “Mungu atamsaidia huyu mtoto atapona”, - na ‘kumwinua kutoka mavumbini’ kama usemavyo wimbo wa katikati wa leo. Katika kutimiza mapenzi ya Mungu na mapendo kwa jirani, Mama Maria hakutoa kisingizio chochote cha kutotimiza wajibu wake. Sasa hivi tunaishi kwenye hali ya sintofahamu ya UVIKO-19. Japo ni kweli hali tete lakini bahati mbaya sana sasa imekuwa kama kisingizio cha kufanyika hata baadhi ya mambo au tabia ambazo hatukuwanazo huko nyuma. Kwa mfano: ukiuliza kwa nini hufiki kanisani siku hizi? Korona!

Wakati wa Misa hatutakiani amani tena? Watu wanasema korona! Kwa nini hatutembeleani majumbani? Korona! Kwa nini wengine hawakufika kwenye mkutano leo? Korona! Nimekwama bwana naomba msaada kidogo…utasikia hivi hujui kama kuna korona?  Nk. korona, korona, korona. Korona ni sababu ya kila kitu. Bahati mbaya wengine tunasahau kabisa kuwa bado tuna asili ya watu ambao husalimiana hata kama hatufahamiani! Siku hizi huko mabarabarani tunapitana tu, na barakoa hizi ndio kabisaaaa, zinavutwa kufunika mpaka uso! Lakini tunakutana porta potese, tunakutana huko Kidimbwi, tunakutana darasani, tunakutana kwenye maharusi, kwenye pambano la Simba na Yanga kwa Mkapa, tunajaa tele! Nadhani hata jana mmeshuhudia hali hiyo hapo Stadium, hata kama si kwa kuwepo kimwili labda hata kwa Luninga! Wachoyo, wavivu wa dini, na antisocial wamepata sababu! Makasisi kwa walei, katika kutimiza wajibu wetu kwa Mungu na jirani tuache visingizio!

Uadilifu wa Maria na moyo wake usio na doa si sifa pekee ya Maria. Ana fadhila nyingi mno! Ni wewe tu kuchagua ni ipi hasa unaona umevikwa na Mungu na unaitumiaje fadhila hiyo katika kumtumikia. Siku moja nikiwa darasani huko Wisconsin, Profesa wetu mmoja alisema kila mtu ataje walau sifa moja ya Bikira Maria anayoijua! Basi pale ni kama ilikuwa “copy and paste” ya Litania! Bahati nzuri au mbaya nikawa wa mwisho kuulizwa, na litania ikawa imeisha! Kila mmoja akawa na hamu kusikia nitasema nini! Nikakumbuka kuwa mwalimu wangu wa Mafundisho sadikifu ya Kanisa Chuo Kikuu cha Jordan pale Morogoro hakuwa mzembe! Nikasema kwa ujasiri mkubwa: “She is the eschatological icon of the Church”. Profesa wangu na kila mmoja darasani alitumbua macho na kuniangalia kwa mshangao! “Wow! Huh, where did you learn that?” Kisha si mimi niliyefafanua hilo tena bali ikawa ni nafasi kwa Profesa! Kwamba sisi sote tunaishi kwa imani na matumaini makubwa mwishoni mwa nyakati kukipata kile alichokwisha kukipata Mama Bikira Maria tayari! Mama ametangulia kutuonesha fahari ya mbingu na nchi mpya!

Je, ni jambo gumu sana kuishi fadhila za Mama Bikira Maria? Naamini kwa msaada wa Mungu kila jambo linawezekana. Mtume Paulo ametuambia vizuri tu, kwamba “upendo wa Mungu utubidishe”. Maria alijua kuwa hekaluni yumo Bwana, alimpeleka na Mwanawe Yesu, hakumuacha aende peke yake, wala hakumtupa kama masimulizi tuliyosikia. Mwenyezi Mungu ametujalia mfano wa pekee wa moyo safi katika nafsi ya Mama Bikira Maria. Na tunajisikia amani sana kumuita Mama na kuamini bila kigugumizi kuwa daima anatuangalia hata tunapotupwa vichakani kwa dhambi za ulimwengu! Tunatembea kwa kwendo wa farasi, “galloping” na tuna sababu ya kumheshimu kwa kwendo huo” Galloping Mariology” – kwa kuwa na ibada kwake. Lakini swali la msingi pia ni kujiuliza: Kwa kuwa tunabebwa na mama, Je, tubweteke? Ni lazima na sisi tujishikilie, kwa sababu tunajua mtoto usipomtelemsha mgongoni hatatembea mwenyewe kamwe!

Sisi tunaoishi huku nje tunafahamu vizuri sana tabia za wenzetu wa Magharibi wakikukaribisha chakula majumbani mwao! Ikitokea ukasifu uzuri wa chakula alichokutayarishia, utasikia “my mom taught me that recipe”. Kwamba hawezi kumwangusha mama yake hata kama alikuwa hajui kupika! Na kweli, japo si nyakati zote chakula chao ni kizuri. Katika Moyo Safi wa Maria, ni “recipe” gani wewe na mimi tunachukua kunogesha maisha yetu ili tukue katika hekima na kimo kama Bwana wetu Yesu Kristo?  Mwenyezi Mungu atuvike kwa moyo safi, wema, haki, upendo, umoja na uaminifu kwa kwake na kwa binadamu wenzetu. Tuendelee kushikamana kwa upendo katika Utanzania wetu na utu wetu bila kujali tofauti zetu za kidini, kisiasa, kiitikadi, kiimani, kiuchumi, nk. Tuliombee taifa letu na ulimwengu kwa ujumla kuishi maisha ya adili na haki. Kipindi hiki cha UVIKO-19 ni kama tumezongwa na wadudu katika chaka la miiba kila mahali ulimwenguni, kana kwamba tulikuwa tumetupwa! Tukalia kwa sauti na Mungu akasikia! Tuko salama mpaka leo! Tumshukuru Mama Maria kwa kutukumbatia kwa mapendo makuu na moyo wake wa kimama na tumrudishie Mungu shukrani.

19 June 2021, 07:40