Tafuta

Vatican News
Bado kuna ukimya wa familia kuficha unyanyasaji wa kijinsia na unyonyaji wa ajira za watoto na ukeketaji wa watoto wa kike katika badhi ya jamii. Bado kuna ukimya wa familia kuficha unyanyasaji wa kijinsia na unyonyaji wa ajira za watoto na ukeketaji wa watoto wa kike katika badhi ya jamii. 

Tanzania:Mpango wa Kanisa wa kupambana na suala la nyanyasaji wa watoto

Kanisa Katoliki nchini Tanzania limezindua kampeni dhidi ya unyanyasaji wa watoto kama sehemu ya utume wake katika jamii.Linaungwa mkono na serikali,mashirika ya kijamii,shule na taasisi za umma.Mkurugenzi wa Tume ya Kichungaji ya Baraza la Maaskofu(TEC),Padre F.Rutaihwa amesema hali ya unyanyasaji wa watoto nchini Tanzania kwa miaka 25 iliyopita imekua tatizo kubwa la kitaifa.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Serikali, mashirika ya kijamii, shule, taasisi za umma wamezindua mipango mbali mbali ya ulinzi wa watoto nchini Tanzania, ikizingatiwa kwa kiwango kikubwa cha unyanyasaji wa watoto ambacho kimevutia maoni ya umma. Kwa mujibu wa  “Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania” iliyochapishwa na “Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu” (LHRC) inaonesha kuongezeka kwa kasi za ukiukwaji dhidi ya watoto katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kutoka kesi 10,551 za unyanyasaji zilizoripotiwa mnamo 2016, zimefikia hadi 14,419 mnamo 2018 na takwimu zinakua kwa kasi. Kutokana na hali hii, Kanisa Katoliki nchini Tanzania limezindua kampeni dhidi ya unyanyasaji wa watoto kama sehemu ya utume wake katika jamii. Mkurugenzi wa Tume ya Kichungaji ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padre  Florence Rutaihwa, ameeleza katika Shirika la habari za kimisionari Fides kwamba: “Hali ya unyanyasaji wa watoto nchini Tanzania katika miaka 25 iliyopita imekuwa tatizo kubwa la kitaifa. Kanisa nchini Tanzania liko karibu na watoto ambao ni waathiriwa wa dhuluma nyingi, za mwili, kihemko au kutelekezwa na kutengwa. Ili kuweza kutoa usalama na ustawi wa kudumu kwa ajili ya watoto, Kanisa Katoliki nchini Tanzania limeunda hatua ya kichungaji madhubuti ambayo itasaidia kuweka mazingira salama kwa watoto wetu wadogo”.

Miongozo iliyochapishwa na kusambazwa katika jumuiya zote za Wakatoliki zinaelekeza dalili dhidi ya aina zote za unyanyasaji na kutelekezwa kwa watoto, huku ikitoa njia kwa ujumla  ya kulinda watoto, ikithibitisha ushirikiano muhimu na kamili na mamlaka za umma  nchini kote.  Akiendelea Padre Florence amebainisha kuwa: “Mapambano dhidi ya unyanyasaji wa watoto yanahitaji juhudi za pamoja. Kanisa linafanya kazi pamoja na serikali kupitia semina kadhaa na kazi ya kuhamasisha utamaduni, iliyofadhiliwa na serikali na mashirika ya kijamii ya kimataifa kama vile UNICEF. Wazo ni kufanya kampeni za uhamasishaji kwa viongozi wa dini, watu wenye ushawishi na viongozi wa kisiasa ili kuhamasisha kanuni nzuri na maadili ambayo hulinda watoto na watu walio katika mazingira magumu,kwa  kuhimiza mabadiliko ya kijamii na kuunda dhamiri”.

Mkurugenzi vile vile  anabainisha: “Walakini katika sehemu nyingine za Tanzania mila za kienyeji zinafuatwa kama vile kukeketa wanawake katika makabila mengine, au ile ya ndoa za utotoni: kuna wasichana wadogo wanalazimishwa kuolewa, wakati katika hali nyingine kuna ukimya katika familia ambazo huficha unyanyasaji wa kijinsia. Kumeenea unyonyaji wa ajira ya watoto katika maeneo mengine, kama ilivyo mazoea ya kuwachapa viboko watoto kama njia ya kuwaadabisha, wakati katika sekta nyingine za kijamii na siasa bado haijahakikishwa kabisa kwamba wanapiga marufuku kabisa mazoezi haya ya unyanyasaji wa mwili” amebainisha. Tanzania ni moja mojawapo ya watia saini  ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Mtoto (CRC),1989, Mkataba wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa 1990; na kutangazwa Sheria ya Utoto ya 2009. Katika msingi wa mikataba hii, Jumuiya Katoliki inatoa mchango wake kwa ajili ya ulinzi na kuhamasisha haki za watoto.

ULINZI WA WATOTO TANZANIA
13 May 2021, 16:37