Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili VI ya Kipindi cha Pasaka Mwaka B wa Kanisa. Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Kristo kwa binadamu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili VI ya Kipindi cha Pasaka Mwaka B wa Kanisa. Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Kristo kwa binadamu! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili VI ya Pasaka: Shuhuda wa Upendo

Huu ni upendo unaonafsishwa katika uhalisia wa maisha ya watu: kiroho na kimwili na kwa hakika ndio utambulisho wa wafuasi wa Kristo Yesu wanaojitahidi kila kukicha kujenga na kudumisha umoja, upendo, udugu na mshikamano. Yesu ni kielelezo cha upendo usiokuwa na mipaka unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ninapenda kuchukua fursa hii, kukukaribisha ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka ya Bwana. Kristo Yesu ni chemchemi ya wokovu kwa wale wote wanaolipokea Neno lake na Kubatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu. Kristo Yesu anatualika kulitafakari kwa kina na mapana pendo lake ambalo ni chimbuko la Amri Kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani. Ili kuzamisha mizizi katika pendo la Kristo, anatualika kuzishika Amri zake. Huu ni upendo unaonafsishwa katika uhalisia wa maisha ya watu: kiroho na kimwili na kwa hakika ndio utambulisho wa wafuasi wa Kristo Yesu wanaojitahidi kila kukicha kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kristo Yesu ni kielelezo cha upendo usiokuwa na mipaka unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu. Na Kristo Yesu anasema, “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.” Yn. 15:13-15.

Huu ndio upendo uliowapigisha watu butwaa kuona kwamba, hata “Wapagani” waliolisikia Neno lililotangazwa na kushuhudiwa na Mtume Petro wakishukiwa na Roho Mtakatifu. Na huo ndio mwanzo wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika ukweli, haki na upendo thabiti. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni jibu muafaka la mwendelezo wa upendo wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ndugu msikililizaji wa Radio Vatican, Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka ya Bwana ni mwaliko wa kutafakari kwa kina na mapana kuhusu upendo wa Kristo Yesu. Huu ni upendo wa Kimungu, au “Agape” tofauti kabisa na upendo wa kidugu “Filia” au upendo kati ya bwana na bibi “Eros”. Huu ni upendo wa “kula na kulipa, et indio mtindo wa kisasa”. Kanisa katika hekima na busara yake kama Mama na Mwalimu, katika Vipindi Maalum vya maisha na utume wa Kanisa yaani: Noeli na Pasaka, anaweka mbele ya macho ya waamini Injili kama ilivyoandikwa na Yohane. Si haba kwamba, Yohane anapewa kipaumbele cha pekee, kwa sababu ni shuhuda amini wa kile alichoona na kusikia kutoka kwa Kristo Yesu. Mtume Yohane, tangu mwanzo amekuwepo kwenye matukio muhimu sana kwa maisha na utume wa Kristo Yesu.

Yeye ni kati ya wale walioitwa mwanzo kabisa, akashuhudia Kristo Yesu alipogeuka sura, ili kuwaimarisha katika imani dhidi ya Kashfa ya Fumbo la Msalaba. Alipokuwa Bustanini Gethsemane akasali hadi kutokwa jasho la damu na kwamba, Yohane ni kati ya mashuhuda wa Ufufuko na kwamba, huyu ndiye yule mwanafunzi aliyependwa zaidi na Kristo Yesu. Kimsingi Yohane ni shuhuda wa upendo wa Kristo usiokuwa na mipaka. Huu ni upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka. Hili ni tukio ambalo Kristo Yesu aliliandaa kwa ubunifu mkubwa kama kielelezo cha upendo wa Kimungu: “Agape”. Karamu ya mwisho. Kulikuwa na ugumu wa kuyafahamu maneno ya Yesu, lakini zaidi Mafumbo ya maisha na utume wake. Ndiyo maana akawaahidi kuwapelekea Roho Mtakatifu akisema, “Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.” Yn. 16:15-16.

Kristo Yesu alitaka wafuasi wake kumwilisha upendo katika huduma kama kielelezo cha uwepo wake endelevu kati pamoja na wafuasi wake. Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani ni wosia uliotolewa na Kristo Yesu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha wanafunzi wake miguu na kuwataka kuoshana miguu wao kwa wao kama alivyowafanyia. Kwa kupendana wao kwa wao, wafuasi wa Kristo wanaendeleza utume wa huduma ambayo Mwana wa Mungu alikuja kuitekeleza hapa duniani, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wake kwa binadamu. Akaweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kumbukumbu ya mateso, kifo na ufufuko wake; Sakramenti ya Upendo! Kumbe, Ujio wa Roho Mtakatifu ulipania kufafanua Mafumbo ya maisha ya Kristo, kuwakumbusha na kuwaimarisha katika ukweli na imani.

Mwinjili Yohane anapembua upendo na kuuweka katika ngazi kuu tatu: Upendo wa Mungu kwa Mwanaye Kristo Yesu. Pili ni Upendo wa Kristo Yesu kwa binadamu wote. Tatu ni upendo wa Baba na Mwana unaomwilishwa katika upendo kwa jamii. “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Yn. 15:19. Hiki ndicho kipimo cha upendo wa Kristo, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Kukaa katika pendo la Kristo Yesu maana yake ni kuwa waaminifu katika Sheria na Amri zake, ambazo amezipatia muhtasari kwa kuzikita katika upendo kwa Mungu na jirani. Hiki ndicho kiini cha Amri Mpya ya upendo kwa Mungu na jirani. Huu ni upendo unaobubujika kutoka kwa Mungu kwa sababu Mungu ni upendo. Asiyejua kupenda anabaki katika kifo. Rej.1 Yn. 3:14.

Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa, anafafanua kwa kina maana ya upendo katika utenzi wake wa upendo kwa kusema: “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika”. IKor 13:4-8. Ili kupendwa, mwamini hana budi kwanza kujifunza kupenda kwani Kristo Yesu amewapenda wao kwanza. Upendo wa dhati unathubutu. Kwa wale ambao hawakuonja upendo katika safari ya maisha yao, wamekuwa wakikabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbalimbali za maisha. Kwa mwamini upendo wa Kimungu unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo inayomwezesha mwamini kupata fadhila ya upendo. Upendo, umoja na mshikamano wa kidugu ni kielelezo na utambulisho wa wafuasi wa Kristo Yesu. Rej. Yn. 17: 23.

Upendo ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa binadamu inayomsukuma kumtafuta mdhambi. Upendo hauna budi kumwilishwa katika matendo: “Watoto wadogo tusipende kwa neno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wakweli…” 1 Yn. 3:18. Hiki ndicho kielelezo cha Kanisa la Mwanzo kama linavyosimuliwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume. Kwani wote walikuwa na moyo na roho moja kwa sababu walikuwa wamejazwa na Roho Mtakatifu aliyewawezesha kujenga na kudumisha: umoja, upendo na udugu wa kibinadamu na hivyo kuwa ni marafiki wa Kristo Yesu. Lakini, kielelezo kikuu cha upendo huu ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Tumwombe Kristo Yesu atusaidie kuzishika Amri zake ili kweli tuweze kuwa ni marafiki zake na mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo.

Liturujia J6 Pasaka

 

07 May 2021, 15:44