Tafuta

2021.05.13 Siku ya Wauguzi Duniani 12 Mei: Wauguzi wa Hospitali ya Biharamulo,Kagera Tanzania na teule ya Wilaya inayoendeshwa na Watawa wa Mtakatifu Bernadetta. 2021.05.13 Siku ya Wauguzi Duniani 12 Mei: Wauguzi wa Hospitali ya Biharamulo,Kagera Tanzania na teule ya Wilaya inayoendeshwa na Watawa wa Mtakatifu Bernadetta. 

Siku ya Wauguzi duniani 2021:Timiza ahadi ya kiapo na zingatia kanuni na sheria za uuguzi

Wauguzi wa Hospitali ya Jimbo la Rulenge-Ngara,Biharamulo,Tanzania wameshauriwa kufanya kazi kwa weredi katika utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa ili kutimiza ahadi ya kiapo chao kwa kuzingatia kanuni na sheria za uuguzi.Amesisitiza hayo Muunguzi Mkuu wa Hospitali hiyo Sr. Evodia Salvatory katika fursa ya Siku ya Wauguzi Duniani 2021,Mei 12 kwa mada"Wauguzi ni sauti inayoongoza Dira ya Huduma ya Afya".

Na Sr. Angela Rwezaula –Vatican & Joseph Sekiku - Fadeco.

Katika fursa ya siku ya Wauguzi duniani tarehe 12 Mei wauguzi wa hospitali teule ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, Tanzania wameungana na wenzao nchini na ulimwenguni kote katika kuadhimisha siku hii, hasa wakimuenzi mwasisi wa uuguzi Bi Florence Nightingale (Firenze, 12 Mei 1820 – London, 13 Agosti 1910). Kwa njia hiyo Wauguzi hao katika fursa ya siku hii wamerudia viapo vyao vya pamoja na kutoa zawadi kwa wagonjwa katika wodi mbali mbali za  hospitali hiyo. Hospitali hiyo ni ya Jimbo Katoliki la Rulenge -Ngara, Tanzania ambayo inaendeshwa na watawa wa Shirika la Mtakatifu Bernadetta na ambayo  hivi karibuni imekuwa Hosptiali  teule ya Wilaya ya Biharamulo. Kwa mujibu wa Kaimu Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo Bi. Pili Fanueli Ngoriga akizungumza na Radio Fadeco amethibitisha jinsi ambavyo wanafurahi kuona kwamba huduma yao inayotolewa inatambulika na kuheshimiwa.

WAUGUZI WA HOSPITALI YA BIHARAMULO WAKIADHIMISHA SIKU YA WAUGUZI DUNIANI
WAUGUZI WA HOSPITALI YA BIHARAMULO WAKIADHIMISHA SIKU YA WAUGUZI DUNIANI

Hata hivyo, amewaasa wauguzi wenzake mahali popote walipo kuheshimu kazi hiyo kwani amesema ni wito hivyo ni wajibu wa kutimiza wito huo. Katika fursa siku hii haikushia hapo kwani mchana waguzi wote katika hospitali hiyo wameshiriki kuwatembelea wagonjwa katika wodi na kuwapa zawadi waliozo waandaliwa wagonjwa. Kwa kuongozwa na kauli mbiu ya Siku ya Wauguzi dunani 2021 isemayo “Ni sauti inayoongoza Dira ya Huduma ya Afya”, wauguzi hao wameandamana wakiimba na kujipongeza kwa kazi bzuri wanayoifanya na ambapo sherehe hizo zimefanyika katika ukumbi wa Kanisa la Kianglikana mjini Biaharamulo. Akizungumzia kuhusiana na siku hii, naye Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo Sr. Evodia Salvatory amewashauri wauguzi wote kufanya kazi kwa weredi katika utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa na ili kutimiza ahadi kulingana na viapo vyao kwa kuzingatia kanuni na sheria za uuguzi. Tusikilize Sr. Evodia Salvatory:

SIKU YA WAUGUZI DUNIANI 2021

Hata hivyo katika fursa ya siku hii ya wauguzi, Shirika la Afya ulimwenguni, (WHO) linaeleza, licha ya jukumu muhimu wanalofanya wauguzi  katika huduma ya afya, kuna uhaba wa wafanyakazi hao ulimwenguni, uhaba ambao unatarajiwa kuongezeka kadiri idadi ya watu inavyoongezeka.Shirika la Afya (WHO) limesema kuwa wauguzi wana jukumu muhimu katika huduma za afya na mara nyingi ni mashujaa wasiojulikana katika vituo vya huduma za afya na huduma za dharura.  Mara nyingi wao ndio wa kwanza kugundua dharura za kiafya na hufanya kazi katika mstari wa mbele kuzuia magonjwa na utoaji wa huduma ya msingi ya afya, ikiwemo kukuza afya, kuzuia maginjwa, na kutibu.  Takwimu za WHO zinaonesha kuwa wauguzi na wakunga ni takribani asilimia 50 ya wafanyakazi wa afya ulimwenguni lakini pia wanawakilisha asilimia 50 ya uhaba wa wahudumu wa afya ulimwenguni, pengo ambalo linakadiriwa kuwa la wauguzi milioni 4 na ili kufikia lengo la huduma ya afya kwa wote itahitaji juhudi kubwa kupunguza uhaba wa wafanyakazi wa afya ulimwenguni.  Siku hii ni ya muhimu sana hasa kufuatia janga la Covid-19 ambalo limedhihirisha umuhimu wa kazi ya wauguzi wote.

PICHA YA PAMOJA YA WAUGUZI WA BIHARAMULO,KAGERA TANZANIA
PICHA YA PAMOJA YA WAUGUZI WA BIHARAMULO,KAGERA TANZANIA

Ikumbukwe kuwa Siku ya wauguzi duniani, huadhimishwa kila tarehe 12 Mei  ya kila mwaka, ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa taaluma hii  ya uuguzi wa kisasa, Florence Nightingale ambaye angekuwa anatimiza miaka 201. Alikuwa muuguzi wa Uingereza na anayejulikana kama “mwanamke aliye na taa”. Anachukuliwa kama mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa, kwani alikuwa wa kwanza kutumia njia ya kisayansi kupitia utumiaji wa takwimu. Alipendekeza pia shirika la hospitali za kambi.

13 May 2021, 13:14