Tafuta

Vatican News
Sherehe ya Pentekoste: Ni mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa. Ni Sikukuu ya Waamini walei wanaohamasishwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Sherehe ya Pentekoste: Ni mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa. Ni Sikukuu ya Waamini walei wanaohamasishwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.  (Vatican Media)

Sherehe ya Pentekoste: Ushiriki Mkamilifu wa Walei Katika Kanisa

Roho Mtakatifu ni Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya Manabii.Hii ni siku ambayo Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume; mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa. Ni Sikukuu ya waamini walei wanaotumwa kuyatakatifuza malimwengu kwa karama na matunda ya Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji katika Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Sherehe ya Pentekoste “Πεντηκοστή (Pentēkostē)” inayohitimisha kipindi cha Siku 50 za Pasaka ya Kristo Yesu, kwa kummimina Roho Mtakatifu. Huyu ni Roho Mtakatifu ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya Manabii.Hii ni siku ambayo Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume; mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Hii ni Sikukuu ya waamini walei wanaohimizwa kutoka kifua mbele, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa karama na matunda ya Roho Mtakatifu. Waamini walei watambue kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa. Kwa kutambua umuhimu wao, Baba Mtakatifu Francisko ameamua kuwashirikisha kikamilifu katika mchakato wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Sinodi zitaanza kuadhimishwa kwenye Makanisa mahalia, Mabaraza ya Maaskofu, Mashirikisho ya Maaskofu Kikanda na hatimaye, wajumbe watakaochaguliwa wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro wataadhimisha Sinodi hii mjini Vatican.

Sherehe ya Pentekoste inalifunua kwa ukamilifu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ule Ufalme wa Mungu uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu sasa uko wazi kwa wale wanaomwamini na kumsadiki. Katika unyenyekevu wa mwili na katika imani, wanashiriki Fumbo la Utatu Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni paji la Mungu na Mungu ni upendo na chanzo cha uzima mpya katika Kristo Yesu. Sherehe ya Pentekoste inapata chimbuko lake katika Agano la Kale na iliadhimishwa siku 50 baada ya Pasaka ya Kiyahudi “Shavuot” yaani Sikukuu ya Mavuno na shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Katika Agano Jipya tunaambiwa kwamba, pale ilipotimilika kazi Baba aliyomkabidhi Mwana afanye duniani (taz. Yn 17:4), basi Roho Mtakatifu akatumwa siku ya Pentekoste ili kulitakatifuza Kanisa siku hadi siku, na waamini wapate njia ya kumkaribia Baba kwa Kristo katika Roho mmoja (taz. Efe 2:18). Huyo ndiye Roho wa uzima au chemchemi ya maji yabubujikiayo uzima wa milele (taz. Yn 4:14; 7:38-39). Kwa njia yake Baba anawahuisha wanadamu, walio wafu kwa sababu ya dhambi, mpaka atakapofufua ndani ya Kristo [pia] miili yao iliyo katika hali ya kufa (taz. Rum 8:10-11).

Roho Mtakatifu hukaa ndani ya Kanisa na ndani ya mioyo ya waamini kama katika hekalu (taz. 1Kor 3:16; 6:19); naye huomba ndani yao na kushuhudia ya kuwa walifanywa kuwa wana (taz. Gal 4:6; Rum 8:15-16 na 26). Naye huliongoza Kanisa kwenye kweli yote (taz. Yn 16:13), hulifanya kuwa moja katika ushirika na huduma, na kulifadhili vipawa mbalimbali vya kihierarkia na vya kikarama, ambavyo kwavyo huliongoza na kulipamba kwa matunda yake (taz. Efe 4:11-12; 1Kor 12:4; Gal 5:22). Kwa nguvu ya Injili hulitia tena Kanisa ujana wake, hulitengeneza upya daima na kuliongoza lipate kuunganika kikamilifu na Bwanaarusi wake. Maana Roho na Bibiarusi wamwambia Bwana Yesu, “Njoo!” (taz. Ufu 22:17). Hivyo Kanisa zima ulimwenguni linajionesha kuwa “taifa lililokusanywa na umoja wa Baba, wa Mwana na wa Roho Mtakatifu”. Rejea. LG 4.

Sherehe ya Pentekoste ni Sikukuu ya waamini walei ndani ya Kanisa. Hawa ni wale waliokusanyika katika Taifa la Mungu na kuwekwa katika Mwili mmoja wa Kristo chini ya kichwa kimoja, wawao wote waitwa, kama viungo vyenye uhai, kutolea nguvu zao zote walizopewa na ufadhili wa Muumbaji na neema ya Mkombozi, ili kulikuza Kanisa na kulitakatifuza daima. Utume wa walei ndio kushiriki utume wa Kanisa lenyewe uletao wokovu; na kuutimiza utume huo ni agizo ambalo wote wanapewa na Mungu mwenyewe kwa njia ya Ubatizo na Kipaimara. Kwa Sakramenti, hasa kwa Ekaristi takatifu, mapendo kwa Mungu na kwa watu, yaliyo roho ya utume wote, yanashirikishwa na kulishwa. Lakini waamini walei wanaitwa kwa namna ya pekee kuonesha uwepo wa Kanisa na utendaji wake mahali pale na katika mazingira yale ambamo lenyewe haliwezi kuwa chumvi ya dunia, isipokuwa kwa njia yao tu. Hivyo kila mwamini mlei, kwa sababu ya karama na vipaji vyenyewe alivyopewa, anakuwa shuhuda na wakati huohuo chombo hai cha maisha na utume wa Kanisa lenyewe “kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo” (Efe 4:7).

Licha ya utume huo uwahusuo moja kwa moja waamini wakristo wote, walei wanaweza kuitwa kwa njia mbalimbali kuushiriki kwa karibu zaidi utume wa Hierarkia, kadiri ya mfano wa wanaume na wanawake wale waliomsaidia Mtume Paulo katika kuishindania Injili, na kutenda kazi katika Bwana (taz. Flp 4:3; Rum 16:3 nk). Aidha wana uwezo wa kuwekwa na Hierarkia ili kutimiza kazi kadhaa za Kanisa kwa ajili ya shabaha ya kiroho. Basi, waamini walei wote wametwishwa mzigo wenye heshima wa kufanya kazi ili azimio la wokovu la Mungu liwafikie zaidi na zaidi watu wote wa nyakati zote na wa mahali pote duniani. Kwa sababu hiyo wafunguliwe kila njia ili wao nao wapate kushiriki kwa bidii tendo la wokovu la Kanisa kadiri ya nguvu zao na kwa kuendelea kusoma alama za nyakati! Rej LG 33. Roho Mtakatifu ni msingi wa umoja katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mhimili wa umoja na mshikamano katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa.

Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine. Sinodi ya XVI ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2022 itaongozwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume”. Mchakato wa maadhimisho ya Sinodi hii utaanza kuwashirikisha waamini walei kwa undani zaidi, ikilinganishwa na maadhimisho ya Sinodi zilizopita, ili kuendelea kukazia umuhimu wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa.

Roho Mtakatifu ni Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana. Maadhimisho ya Juma la “Laudato si” yalianza tarehe 16 Mei 2021 na yanafikia kilele chake tarehe 25 Mei 2021 sanjari na kufunga rasmi “Mwaka wa Laudato si.” Kipindi hiki kimekuwa ni muda muafaka wa kupima mafanikio yaliyopatikana katika Maadhimisho ya Mwaka wa “Laudato si” katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia. Ni muda wa kufanya upembeuzi yakinifu kuhusu madhara yaliyosababishwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ili kujiandaa vyema kuweza kukabiliana na majanga kama haya kwa siku za usoni. Huu ni muda uliokubaliwa wa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini, wanaohitaji msaada na uwajibikaji ili hatimaye, kuleta mageuzi makubwa yanayofumbatwa katika wongofu wa kiekolojia, kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya dunia ambayo inaendelea kuchakaa kwa kasi kubwa.

Wanasayansi wanasema, tabia ya ulaji wa kupindukia, matumizi mabaya ya rasilimali za dunia na uchafuzi wa mazingira umevuka kiwango cha dunia kuweza kustahimili, kiasi kwamba, kwa sasa kinachofuatia ni majanga asilia kama yanavyoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Kuna hatari kubwa ya kukiachia kizazi kijacho: mashimo ya machimbo ya madini, jangwa na ukame wa kutisha na lundo kubwa la takataka kutokana na ulaji wa kupindukia! Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, tumwombe Roho Mtakatifu atukirimie mapaji yake saba, atusaidie kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa uinjilishaji unaofumbatwa katika uhalisia wa maisha. Tusimame kidete kulinda na kutunza mazingira kama ushiriki wetu katika Injili ya Uumbaji!

Liturujia Pentekoste
21 May 2021, 14:59