Tafuta

Padre Godfrey Denis Gwang'ombe Jimbo Kuu la Mbeya aliyefariki dunia tarehe 13 Aprili 2021; Mei Mosi 2021 mwili wake ukawasili Dar es Salaam na tarehe 4 Mei 2021 akazikwa Jimboni Mbeya. RIP. Padre Godfrey Denis Gwang'ombe Jimbo Kuu la Mbeya aliyefariki dunia tarehe 13 Aprili 2021; Mei Mosi 2021 mwili wake ukawasili Dar es Salaam na tarehe 4 Mei 2021 akazikwa Jimboni Mbeya. RIP. 

Padre Godfrey Denis Gwang'ombe Aliyefia Italia, Azikwa Mbeya!

Padre Godfrey Denis Gwang’ombe alizaliwa tarehe 10 Agosti, 1976. Tarehe 18 Februari 2006 alipewa Daraja ya Ushemasi, Jimboni Cuneo, nchini Italia na hatimaye, tarehe 3 Agosti 2006 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Parokiani Mwanjelwa, Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania. Tarehe 13 Aprili 2021 akakutwa amefariki ghafla chumbani mwake. Amezikwa 4 Mei 2021 Mwanjelwa, Mbeya.

Na Thompson Mpanji, - Mbeya, Tanzania.

Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanawahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya imani na matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania, Jumanne tarehe 4 Mei 2021 amewaongoza watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Mbeya kumsindikiza Marehemu Padre Godfrey Denis Gwang’ombe katika usingizi wa milele, huku akiwa na matumaini ya ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Nyaisonga, amewasihi waamini kuendelea kumtegemea na kumtumikia Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kwani hajawahi kuwaacha pweke. Amewaalika kutenda na kutekeleza yote kwa sifa na utukufu wa Mwenyezi Mungu, asili ya wema na utakatifu wa maisha. Mwenyezi Mungu ndiye anayestahili kupewa heshima, sifa na utukufu na wala kazi yake haina makosa!

Kwa upande wake, Padre Olivarius Kalupale wa Jimbo Kuu la Mbeya anayefanya utume wake nchini Italia, ameushukuru Ubalozi wa Tanzania nchini Italia chini ya uongozi wa Balozi George Kahema Madafa. Mchango wake wa hali na mali umefanikisha mchakato mzima wa kusafirisha mwili wa Marehemu Padre Godfrey Denis Gwang’ombe kutoka nchini Italia hadi kwenye maziko yake Jimbo kuu la Mbeya. Mwili wa Marehemu Padre Godfrey Denis Gwang’ombe ulisafirisha kutoka Roma tarehe 29 Aprili 2021. Kutokana na Ndege kuchelewa kuwasili mjini Addis Ababa, Ethiopia, maiti haikuweza kuondoka kama ilivyotarajiwa na badala yake, mwili uliondoka tarehe 30 Aprili 2021, na kuwasili Jijini Dar es Salaam Jumamosi, Mei Mosi, 2021 na hatimaye, kusafirishwa kwenda Mbeya Jumapili tarehe 2 Mei 2021 na maziko yake kufanyika tarehe 4 Mei 2021.

Marehemu Padre Godfrey Denis Gwang’ombe alizaliwa tarehe 10 Agosti, 1976 katika Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mwanjelwa, Jimbo kuu la Mbeya. Wazazi wake ni Mzee Denis Gwang’ombe na Mama Agnes Kazimoto. Alipata Sakramenti ya Ubatizo tarehe 29 Agosti 1976. Tarehe 9 Juni 1985 akapokea komunyo ya Kwanza na hatimaye, kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara tarehe 29 Oktoba 1989 parokiani kwake Mwanjelwa! Amesoma Shule ya Msingi Muungano-Mbeya: Kuanzia mwaka 1984 hadi mwaka 1990. Na mwaka 1991 alijiunga na Seminari ndogo ya Kaengesa na mwaka 1994 alihitimu masomo ya kidato cha IV. Mwaka uliofuata alikwenda kujiunga na Sekondari ya Wavulana ya Songea kwa ajili ya kuendelea na kidato cha tano na mwaka 1997 alihitimu kidato cha sita.

Mwezi Januari mwaka 1998 alijiunga na Kituo cha Malezi Irambo na mwezi Julai mwaka 1998 alijiunga na Seminari kuu ya Mtakatifu Augustino Peramiho, Jimbo kuu la Songea kwa ajili ya masomo ya falsafa. Na Kunako mwaka 1999 alijiunga na Seminari ya Jimbo la Cuneo nchini Italia, ambako aliendelea na masomo ya falsafa hadi 2002 mwaka huo huo wa 2002 alijiunga na Seminari Kuu ya Fossano kwa ajili ya masomo ya Taalimungu na Malezi ya Kipadre na kuhitimu mwaka 2006. Tarehe 18 Februari 2006 alipewa Daraja ya Ushemasi, Jimboni Cuneo, nchini Italia na hatimaye, tarehe 3 Agosti 2006 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Parokiani Mwanjelwa, Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania.

Katika maisha na utume wake, Marehemu Padre Godfrey Denis Gwang’ombe aliwahi kuwa Paroko-usu na Mhudumu wa maisha ya kiroho kwenye Hospitali ya Mwambani, Jimbo Kuu la Mbeya na baadaye aliteuliwa kuwa Paroko kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2010. Kunako mwaka 2010 alitumwa tena nchini Italia ili kujiendeleza zaidi kwa masomo na akiwa masomoni, alipata pia fursa ya kutekeleza dhamana na wajibu wake wa Kipadre kwenye Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Fossano, Italia, tangu mwaka 2018 hadi mauti yalipomfika. Alikuwa ni Paroko-usu wa Parokia ya Mtakatifu Antony Abate “San’Antonio Abate” Jimbo Katoliki la Fossano, Italia.

Padre Godfrey Denis Gwang’ombe alikutwa amefariki dunia akiwa chumbani kwake, tarehe 13 Aprili 2021 usiku. Katika maisha na utume wake wa Kipadre ataendelea kukumbukwa kwa ushujaa wa imani, upole, uvumilivu na ucheshi alioushuhudia kwa kuwapenda watu wa Mungu; akajitoa sadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto wadogo na vijana! Ni katika muktadha huu, Chama cha Skauti Jimbo Kuu la Mbeya, kimekuwa mstari wa mbele katika shughuli nzima ya maandalizi hadi kumpokea Marehemu Padre Padre Godfrey Denis Gwang’ombe aliporejeshwa nchini Tanzania, tayari kwa mazishi. Alikuwa ni Gwiji na mwalimu mzuri wa muziki mtakatifu. “Alipokuwa akicharaza kinanda; wanakwaya walidemka kwa machozi ya furaha” Wengi wao wanasema, “hakika watamkosa Padre Godfrey Denis Gwang’ombe”. Jimbo Kuu la Mbeya linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya uhai, utume na Daraja takatifu ya Upadre aliomkirimia Mtumishi wake Padre Godfrey Denis Gwang’ombe” si tu kwa huduma ya shughuli za kichungaji nchini Tanzania, bali pia kwa kumwezesha kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kati ya watu wa Mungu nchini Italia.

Jimbo Kuu la Mbeya linawashukuru wazazi, ndugu na jamaa kwa: kumzaa, kumtunza na kumlea hadi kufikia Daraja Takatifu ya Upadre. Jimbo Kuu la Mbeya, linawashukuru Maaskofu wa Jimbo Katoliki la Cuneo na Fossano kwa kumsomesha na hatimaye, kumshikirikisha katika maisha na utume wa Kimisionari. Shukrani zinawaendea pia wale wote walioshirikiana naye katika maisha na utume wake kama Padre sehemu mbalimbali hadi mauti yalipomfika. Jimbo linawashukuru watu wa Mungu wote waliofanikisha mchakato wa kumsafirisha Marehemu Padre Godfrey Denis Gwang’ombe kutoka Italia hadi Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania kwa Ibada ya Misa takatifu na mazishi yaliyofanyika Jumanne tarehe 4 Mei 2021. “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda” 2Tm 4:7.

Padre Godfrey

 

05 May 2021, 15:03