Tafuta

Wazazi na walezi wanachangamotisha kuhamasisha na kukoleza miito mitakatifu katika familia kwa kuwasaidia watoto wao kufikia  utimilifu wa ndoto zao. Wawe ni mfano bora wa kuigwa! Wazazi na walezi wanachangamotisha kuhamasisha na kukoleza miito mitakatifu katika familia kwa kuwasaidia watoto wao kufikia utimilifu wa ndoto zao. Wawe ni mfano bora wa kuigwa! 

Wazazi na Walezi Jitahidini Kuhamasisha Miito Mitakatifu!

Wazazi na walezi wanamahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, familia zao zinakuwa ni vitalu kwa kuotesha na kukuza mbegu ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwa kusaidia kutfasiri vyema ndoto na matamanio halali ya watoto wao katika maisha. Wazazi na walezi tangu mwanzo washirikiane na Kanisa katika kulea miito mbalimbali kwa watoto ni chanzo cha baraka.

Na Ndahani Lugunya, - Dodoma, Tanzania.

Imeelezwa kwamba hakuna kilicho kikubwa zaidi ya baraka wapatazo wazazi na walezi pindi mtoto wao anapokuwa Padri au Mtawa. Hayo yameelezwa na Padri Yohana Kalisti na Padre Jerome Manyahi Wakurugenzi wa miito wa Mashirika ya Wamisionari wa Consolata na Shirika la Wajesuiti nchini Tanzania wakati wa kuhamasisha maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni, iliyoadhimishwa Jumapili, tarehe 25 Aprili 2021, umenogeshwa na kauli mbiu “Mtakatifu Yosefu Ndoto ya Wito”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amekazia umuhimu wa: Ndoto, huduma na uaminifu; mambo msingi katika kukuza na kudumisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Miito Ulimwenguni yamekwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu uliozinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2020 na yanatarajiwa kufungwa kwa kudema hapo tarehe 8 Desemba 2021.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa. Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yasaidie kunogesha Ibada kwa Mtakatifu Yosefu, Mlinzi wa Kanisa.

Padri Yohana Kalisti, Mkurugenzi wa Miito wa Shirika la Wamisionari wa Consolata nchini Tanzania amesema kuwa, endapo wazazi au walezi watawaruhusu watoto wao kwa kuwatakia neno la baraka, kadhalika baraka hizo hujerea kwao tena. “Wao wakimruhusu mtoto kwa baraka ile ya nenda mwanangu tunakubariki ile baraka itawarudia wao, ni kwa sababu tu wakati mwingine tunakuwa wazito kuamini kwahio tungekuwa wepesi kuamini kwamba baraka nimeitoa itarudi nyingi zaidi. Kwa hiyo wazazi msihofu katika kuwatoa watoto wenu kwa kuogopa labda hali ya kifamilia na vitu kama hivyo, hayo mengine yote kama mtoto ameguswa na anakwambia kabisa Mama au Baba ninaguswa katika hili nawewe kama mzazi Baba au Mama umemfuatilia mtoto wako na umeona kweli kuna hiyo nia mpe nafasi,” amesema Padri Kalisti.

Aidha amewaomba wazazi na walezi katika familia za Kikristo kutokujiweka mbali na watoto wao wanapoona wana nia ya kujiunga na maisha ya Kipadre na Kitawa, ikiwa ni pamoja na kukemea vitendo vinavyoenda kinyume na matamanio ya maisha yao. “Inawezekana wakati mwingine wazazi huwa tunajiweka mbali ninachoomba kwa wazazi tusipoteze uwezo wetu wa kukemea tunapoona watoto wetu ambao wanaotamani jambo fulani wanaishi kinyume na hicho wanachokitamani. Mwanao amekwambia mimi nataka kuwa Padri lakini unavyoona maisha yake anavyoishi ni kinyume kabisa na maisha ya Kipadri mzazi usikae kimya na ni vizuri mzazi uwe tayari hata kumshirikisha hilo mkurugenzi wa miito anapokuja kwako kukwambia mwanao ametuma maombi kujiunga na shirika letu,” amesema Padri Kalisti. Mkurugenzi huyo wa Miito wa Shirika la Wakonsolatha Tanzania amesema kwa kufanya hivyo wazazi na walezi wataweza kuponya watoto wengi na kuliponya Kanisa ambalo baadhi ya watu wamelifanya liwe na vidonda vingi kutokana na matendo yao maovu wanayoyafanya.

Kwa upande wake Padre Jerome Manyahi Mkurugenzi wa Miito wa Shirika la Wajesuiti Tanzania amesema kuwa, kupungua kwa ari ya miito ya Upadre na usista kama ilivyokuwa awali kunatokana na familia kutolea watoto wao katika maadili mema ya kiroho. Padre Manyahi amesema kuwa wazazi na walezi wengi kwa sasa hawana mpango wa kukaa na kusali kwa pamoja kama familia, na badala yake kila mmoja yupo “bize” na shughuli zake. Amesema kibaya zaidi hivi sasa katika familia nyingi watoto wanalelewa na wadada wa kusaidia kazi za nyumbani, jambo linalopolekea watoto kushindwa kupata mafundisho ya kiimani na kijamii ambayo walipaswa kupewa na mzazi. Aidha Padre Manyahi amesema kuwa ili Kanisa liweze kupata miito mingi ya upadri na utawa inayotokana na Ndoa Takatifu, familia za Kikristu zinapaswa kujikita zaidi katika malezi bora ya misingi ya imani. Hata hivyo amefafanua kuwa shule nyingi za Seminari kwa sasa zimekuwa kama Sekondari za kawaida, hivyo mafundisho msingi ya Kanisa yamepungua jambo lililopelekea majimbo mengi kuendelea kukabiliwa na uhaba wa Mapadri.

Naye Padre Philo Nguruwe wa Shirika la Wajesuit hivi karibuni akitoa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika Parokia ya Mwenyeheri Maria Teresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Jimboni Dodoma, ametoa wito kwa waamini nchini Tanzania kuweka kipaumbele kwenye sala zao katika kuombea Miito  mitakatifu ndani ya kanisa. Katika mahubiri yake Padri Nguruwe amesema kwa sasa waamini wanapaswa kujizatiti katika kuendelea kuombea miito mbalimbali katika Kanisa, ikiwa ni pamoja na upadri na utawa ili kuondokana na uhaba wa mihimili ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya kibinadamu.

04 May 2021, 15:05