Tafuta

Halmashauri ya Walei Wakatoliki Tanzania katika ujumbe wao kwa Sherehe ya Pentekoste 2021 wanatafakari kuhusu Mt. Yosefu na Utume wa Walei katika uongozi wa Roho Mtakatifu. Halmashauri ya Walei Wakatoliki Tanzania katika ujumbe wao kwa Sherehe ya Pentekoste 2021 wanatafakari kuhusu Mt. Yosefu na Utume wa Walei katika uongozi wa Roho Mtakatifu. 

Halmashauri Walei Tanzania: Ujumbe wa Pentekoste 2021!

Halmashauri ya Walei Katoliki Tanzania katika Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2021, wanawaalika waamini kumjifunza Mtakatifu Yosefu huku wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Mtakatifu Yosefu ni Mume wake Bikira Maria na Baba Mlishi wa Mtoto Yesu. Ni mwangalizi mwaminifu na mlinzi wa tunu kubwa zaidi yaani Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria.

Na Halmashauri ya Walei Katoliki Tanzania, - Dar es Salaam.

Tunapoadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu (08.12.2020 hadi 08.12.2021) kama ulivyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko, kwa namna ya pekee tungependa kuchukua nafasi hii kutafakari nafasi ya Utume wa Mtakatifu Yosefu katika Kanisa, na hivyo kutoa fursa ya sisi Waamini Walei kujifunza kwake, tukiongozwa na Roho Mtakatifu. Mt. Bernadin wa Siena (1380-1444) alisema kwamba, pale ambapo Mungu humchagua mtu kwa utume fulani, humjaza mtu huyo na karama za kipekee za Roho Mtakatifu zinazohitajika katika kuutimiza utume husika. Upendeleo huu pia huonekana katika utume wa Mt. Yosefu, Baba mlishi wa Bwana wetu na mume wa Malkia wa ulimwengu, aliyewekwa juu ya malaika wote. Mt. Yosefu alichaguliwa na Mungu Mwenyezi kama mwangalizi mwaminifu na mlinzi wa tunu kubwa zaidi, yaani, Mwana wa pekee wa Mungu na Maria, mke wa Yosefu. Aliubeba utume huu kwa uaminifu wa hali ya juu hadi pale Mungu alipomwita, akimwambia: “Vyema mtumwa mwema na mwaminifu, ingia katika furaha ya bwana wako.” (Mt 25:23).

Nafasi hii ya Mt. Yosefu, wito na utume wake ni katika mukhtadha uleule anaosema Mt. Paulo kwamba “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe” (Efe 4:11-12).  Mungu huita na kuchagua watu mbalimbali ili kutenda utume fulani ndani ya Kanisa wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Mtakatifu Yosefu ni mfano halisi wa ukweli huu. Na kwa namna ya pekee ukweli huu ni halisi kwa kila mmoja wetu katika Kanisa na utume wake. Hivyo basi, kama alivyochagulia Mt. Yosefu na kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, sisi sote, na hasa Waamini Walei, wakiongozwa na Roho Mtakatifu wanatumwa kutimiza utume wao kwa kutumia karama na vipaji vyao mbalimbali. Wapendwa katika Kristo, tunapoadhimisha Sherehe hii ya Pentekoste, huku tukitafakari nafasi yetu sisi Walei katika Familia ya Mungu, na hususani katika Maadhimisho ya Mwaka huu wa Mtakatifu Yosefu, tungependa kwa pamoja, tukiangazwa na Roho Mtakatifu, kumwangalia Mt. Yosefu kama mfano wetu kwa maisha ya fadhila.

Moja ya sifa kubwa ya Mt. Yosefu ni utii kwa sauti ya Mungu. Yosefu akitambua kwamba mchumba wake Mariamu alikuwa mjamzito hata kabla hawajakaribiana, aliazimu kumwacha kwa siri. Lakini hata kabla hajatimiza uamuzi huo Malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto na kumjulisha kwamba mimba ya Mariamu ilikuwa ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Mt. Yosefu akitambua nafasi ya Mungu na mpango mzima wa historia ya wokovu, akiongozwa na Roho Mtakatifu alisikiliza sauti hii ya Malaika, akaitimiza na kumchukua Mariamu kama mkewe. Kuongozwa na Roho Mtakatifu maana yake ni kuyatambua matakwa ya Mungu na kuyatekeleza kwa utii. Tunapoadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, na hasa katika Sikukuu hii ya Pentekoste, Walei tunaalikwa kumsikiliza Roho Mtakatifu ili atuongoze kuyasikiliza na kuyatiii matakwa ya Mungu yanayofika kwetu kwa njia ya Mama Kanisa na waandamizi wake. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema kwamba, katika Yosefu tunakutana na mfano wa utii uliokubali mapenzi ya Mungu.

Sifa nyingine ya Mtakatifu Yosefu, ni kulinda na kuheshimu zawadi ya uhai. Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Mt. Yosefu, Walei na hasa wazazi wanaalikwa kutambua na kuthamini uhai wa watoto na watu wote. Mungu alimkabidhi Mt. Yosefu mtoto Yesu kwa ajili ya uangalizi na matunzo ya kibaba. Mt. Yosefu amekuwa mtunzaji wa karibu wa Yesu katika hali ya kibinadamu na mahitaji yake yote, akimwokoa katika hatari zote za maisha ya utoto na hasa pale Herode alipotishia uhai wa mtoto. (Rej. Mt 2:13-15). Wajibu huu wa Mt. Yosefu unaonekana pia hata pale mtoto Yesu alipobaki hekaluni huku wazazi wake wakimtafuta kwa hofu kwamba amepotea. (Rej. Lk 2: 41-51).

Mtakatifu Yosefu anatufundisha kuthamini, kuipenda na kuilinda zawadi ya uhai na hasa uhai wa watoto ambao mara nyingi hawana mtetezi. Ndicho aliochofanya Mt. Yosefu alipomwokoa mtoto Yesu dhidi ya mikono ya muuaji Herode. Akimwongelea Mt. Yosefu kama baba aliyejali, Mt. Augustino wa Hippo anasema: “Licha ya kwamba Mt. Yosefu si Baba wa Yesu kimwili, ni baba halisi wa Yesu kwa maana kwamba alishiriki kikamilifu, kimamlaka, kiupendo na kiimani katika malezi ya Yesu.” Mt. Yosefu anatupatia mfano bora wa jukumu la kulea, kutunza na kufundisha mtoto katika mila na desturi zetu sahihi hata kiasi cha kusema kwamba “Naye akazidi kuendelea katika kimo na hekima, akimpendeza Mungu na wanadamu” (Lk 2:52). Wazazi na walezi wana wajibu wa kuulinda uhai wa watoto waliokabidhiwa tangu wakiwa tumboni. Haya yote yatawezekana tu iwapo tutamsikiliza Roho Mtakatifu ambaye ni “Sauti ya Mungu” iliayo ndani mwetu. Tutamwenzi Mt. Yosefu kwa kutimiza wajibu huo tuliokabadhiwa.

Fadhila ya Imani: Ndugu wapendwa, tunapoadhimisha Mwaka wa Mt. Yosefu na kwa namna ya pekee katika Sherehe hii ya Pentekoste, tungependa pia tujifunze fadhila ya imani ambayo Mt. Yosefu aliionyesha katika maisha yake. Mt. Yosefu ni mfano bora wa imani kwetu; maisha yake yote yaliongozwa na imani. Kwa imani Mt. Yosefu alimchukua Mariamu kuwa mke wake. (Rej. Mt 1:20). Kwa imani Yosefu alikabidhi maisha yake yote katika Fumbo la Umwilisho; na kwa namna hiyo Yosefu anakuwa wa kwanza kuwekwa na Mungu ili kumsindikiza Mariamu katika safari yake ya kiimani. Kwa wazazi wa Kikristo hawana budi kutambua kwamba wamekabidhiwa watoto ili wawalee kiimani kwa wao wenyewe kuiishi imani. Wazazi wa siku hizi wameacha wajibu wao wa kulea watoto wao na hasa kiroho. Tunamhitaji Roho Mtakatifu ili atujalie paji hili la imani litakalotuwezesha kujikabidhi bila kusita katika mapenzi ya Mungu na pia kutufanya kuwa walimu wa dini kwa wale tuliokabidhiwa kuwalea na kuwatunza.

Mtakatifu Yosefu mchapa kazi. Wapendwa katika Kristo, tumeitwa ili kuifanya dunia mahali pazuri pa kuishi. Moja ya namna ya kuitengeneza dunia pawe mahali pazuri pa kuishi ni kwa kufanya kazi. Kwa njia kazi yake, useremala Yosefu alimwingiza Yesu katika ulimwengu halisi wa mazingira yake ya wakati wake. Akitambua utakatifu wa kazi, Mt. Yohane Paul II katika Waraka wake wa Kitume “Laborem Exercens” anafundisha kwamba kwa njia ya kazi zetu tunashiriki kazi ya uumbaji pamoja na Mungu. Yosefu na Yesu walishiriki kazi hii kikamilifu hata kuwafanya watu wa kwake kumshangaa Yesu kwa kusema “Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala?” (Mt 13: 54-55). Kimsingi, tunaweza kuona kwamba Yesu alitumia muda mwingi zaidi kufanya kazi akiwa na Yosefu kuliko kazi ile ya kuhubiri. Kwa namna hiyo Yosefu pamoja na Yesu walishiriki katika “kuutakatifuza ulimwengu” kwa njia kazi ya useremala. Tunapoadhimisha Mwaka huu wa Mt. Yosefu, tunaalikwa kuona thamani ya kazi katika maisha yetu; kwani kwa njia ya kazi zetu tunamtukuza Mungu na kujipatia utakatifu.

Mtakatifu Yosefu mwenye haki. Wapendwa katika Kristo, kati ya fadhila ngumu za maisha ni ile fadhila ya haki. Mt. Yosefu anatambulika kuwa ni mtu wa haki. (Rej. Mt 1:19). Mwinjili Mathayo anapomtaja Yosefu kuwa ni mwenye haki anamtambulisha kwetu kuwa ni mtu aliyeishi agano la Mungu kwa ukamilifu. Kwa maneno mengine, Mt. Yosefu alishiriki haki na utakatifu wa Mungu. Kimsingi Mungu pekee ni mwenye haki na anatenda haki. Hivyo mtu anatambulika kuwa ni mwenye haki na anatenda haki iwapo mtu huyo anatenda kadiri ya “haki ya Mungu,” anaishi na kutenda kadiri ya agano la Mungu. Kwa kuishi agano la Mungu kwa ukamilifu, Mt. Yosefu alistahili kuitwa mwenye haki. Wengi wetu tumeshindwa kushika agano la Mungu na hivyo kulishika agano hilo, agano ambalo linatokana na ahadi zetu za ubatizo. Matokeo yake tunakosa haki mbele ya haki. Katika Sherehe hii ya Pentekoste, tumwombe Mungu atujalie mwanga wa Roho Mtakatifu ili tujaliwe fadhila ya haki ili tuweze kustahilishwa haki kama ilivyokuwa kwa Mt. Yosefu.

Mtakatufu Yosefu alitenda kwa ukimya. Wapendwa katika Kristo, yapo mengi ambayo katika kuadhimisha Mwaka huu wa Mtakatifu Yosefu na kwa namna ya pekee katika Sherehe hii ya Pentekoste tunaweza kujifunza kwake. Ukimya wa Mt. Yosefu ambao ulimfanya kutenda yote kimya kimya pasipo kujitangaza ni kinyume chetu wengi wetu ambao tunatenda ili tuonekane, tutangazwe na tushabikiwe. Mt. Yosefu aliongea machache lakini alitenda mengi. Yosefu mnyenyekevu. Unyenyekevu wake pia ni kitu cha kujifunza katika maisha yetu kama Walei. Unyenyekevu wake ni ushahidi mkubwa wa utakatifu wake. Ikumbukwe kwamba “Unyenyekevu ni mama wa fadhila zote.”  Maisha yake ya kujitoa kwa ajili ya familia yake ni jambo la msingi katika utume wetu katika Kanisa. Mt. Yosefu alitoa maisha yake yote kwa ajili ya Maria na Yesu; kwa kuwapenda na kuwahudumia kwa mapendo ya kibaba. Yosefu anatufundisha kujitoa kikamilifu kwa ajili ya utume wetu wa kumpenda Mungu na watu. Yosefu anatufundisha kwamba maisha yetu si kwa ajili yetu bali ni kwa ajili ya wengine. Yosefu “Amekuwa mkuu kwa kuwa mtumishi” (Mk 10:43-44).

Wapendwa katika Kristo, tunapoadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu na tukitambua uwepo wa Roho Mtakatifu katika utume wake, hatuna budi nasi tutambue kwamba, kwa kutumia kikamilifu karama na matunda ya Roho Mtakatifu tuliyokirimiwa katika maisha; tuongozwe katika utakatifu wa maisha.  Tuwe mashuhuda wa kazi njema zilizounganishwa katika huduma zetu, ili kuujenga na kuudumisha Ufalme wa Mungu na kwamba, kila mwamini anayo nafasi ya pekee katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Tunapoadhimisha Sherehe hii ya Pentekoste katika Maadhimisho ya Mwaka wa Mt. Yosefu, hatuna budi kutambua kwamba, tuna wajibu na dhamana kama wabatizwa, waliozaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu wa kuutangaza na kuusimika Ufalme wa Mungu katika mazingira na kazi zetu kama alivyofanya Mt. Yosefu. Tumwombe basi Mt. Yosefu aliye mlinzi, msimamizi na mtetezi wa kisheria wa nyumba ya Mungu atuombee ili kama alivyosema Papa Pius XII (1955) kwamba, “Ikiwa unataka kuwa karibu na Kristo, narudia ‘Ite ad Ioseph,’ nenda kwa Yosefu.”

Walei Tanzania
20 May 2021, 16:30