Tafuta

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Baraza la Maaskofu Katoliki Canada na Maaskofu wa Ireland wanawahimiza waamini kuwa ni mashuhuda wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati ili kumtangaza Kristo Yesu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Baraza la Maaskofu Katoliki Canada na Maaskofu wa Ireland wanawahimiza waamini kuwa ni mashuhuda wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati ili kumtangaza Kristo Yesu. 

Ujumbe wa Pentekoste kwa Mwaka 2021: Imani, Umoja na Upendo!

Sherehe ya Pentekoste: Waamini wawe na ujasiri wa kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu. Roho Mtakatifu awaimarishe waamini katika fadhila, karama na mapaji, ili yaweze kutumika kwa ajili ya maendeleo na mafao ya wengi. Kwa njia ya Roho Mtakatifu waliyempokea wakati wa Ubatizo awakirimie waamini ujasiri wa kuwa na: nia moja na moyo mmoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Pentekoste ni hitimisho la Kipindi cha Pasaka ya Bwana. Ni siku ambayo Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume; mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hii ni Sikukuu ya waamini walei wanaohimizwa kutoka kifua mbele, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa karama na matunda ya Roho Mtakatifu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, katika ujumbe wake wa Pentekoste kwa Mwaka 2021 linasema, “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.” Mdo 2:1-4. Huo ulikuwa ni mwanzo mpya wa maisha na utume wa Kanisa, Hata wakati huu, Mwenyezi Mungu bado anamtuma Roho Wake Mtakatifu wanaumba na kuufanya upya uso wa nchi.

Huu ni muda muafaka wa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni mwaliko kwa kusimama na wale wote wanaoteseka kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hili ni janga ambalo limepelekea kutikisika kwa masuala ya kijamii, kiuchumi pamoja na kuporomoka kwa haki msingi za binadamu. Huu ni muda ya kupyaisha: imani, matumaini na mapendo, kwa kuendelea kujikita katika sera na utunzaji bora wa Mazingira, kwa kuwekeza katika Injili ya Uhai, Upendo na Huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Sherehe ya Pentekoste iwe ni nafasi ya kushikamana na maskini, wafungwa, wagonjwa na wale wote wanaoendelea kupekenyuliwa na baa la njaa sehemu mbali mbali za dunia. Hiki ni kipindi mahususi cha kupyaisha na kumwilisha Injili ya upendo katika maisha ya watu!

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Canada “The Canadian Conference of Catholic Bishops (CCCB), linawaalika watu wa Mungu nchini Canada kutangaza na kusimika Ufalme wa Mungu kati ya watu wa Mataifa. Waamini wawe na ujasiri wa kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu. Roho Mtakatifu awaimarishe waamini katika fadhila, karama na mapaji, ili yaweze kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa njia ya Roho Mtakatifu waliyempokea wakati wa Ubatizo awakirimie waamini ujasiri wa kuwa na: nia moja na moyo mmoja. Umoja, upendo na mshikamano wa kidugu ni chemchemi ya matumaini mapya kwa waamini wakati huu wanapoendelea kupambana na athari za janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Waamini waunganishwe na kuwa chini ya uongozi wa Kristo Yesu, Imani moja na Ubatizo mmoja. Rej. Efe 4:5.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland kwa kushirikiana kwa karibu na Kanisa la Kianglikan, linapenda kutoa ujumbe wa matumaini yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka. Watu wa Mungu nchini Ireland wameanza mchakato wa uponyaji na taratibu wanaanza kurejea katika hali ya kawaida baada ya kushambuliwa sana na Virusi vya Ugonjwa wa Korona, UVIKO-19. Huu ni wakati wa kumwendea Kristo Yesu, wale wote waliochoka, waliovunjika na kupondeka moyo, ili aweze kuwaimarisha na kuwapatia pumziko na faraja! Hiki ni kipindi cha kunogesha: huruma, upendo na faraja katika familia, kwa kutumia karama na mapaji ambayo wamekirimiwa na Roho Mtakatifu katika maisha!

WCC Pentekoste 2021
20 May 2021, 16:02